Macho yote TCRA, mamilioni wakizimiwa laini

January 20, 2020 3:18 pm · TULINAGWE ALSON
Share
Tweet
Copy Link

Hatua hiyo ya Serikali kutangaza kuzima laini ambazo hazijasajili usiku wa leo imekosolewa na baadhi ya wadau kikiwemo cha upinzani cha ACT-Wazalendo kimenuia kufungua kesi mahakamani iwapo watu wasiosajiliwa watazamiwa mawasiliano. Picha|Mtandao.


  • Hadi jana ni laini milioni 28.43 au sawa na asilimia 58.2 ya laini zote zilizopo sokoni zilikuwa zimesajiliwa kikamilifu. 
  • TCRA yasema kuna laini zaidi ya milioni 16 ambazo usajili wake haujulikani kwa sababu mbalimbali.
  • Imesema uzimaji wa laini ambazo haujasajiliwa upo pale pale Saa 5:59 usiku.

Dar es Salaam. Macho yote na masikio ya Watanzania leo yatakuwa kwa maofisa wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) watakaokuwa wakizifungia laini ambazo hazijafanikiwa kusajiliwa kwa alama za vidole itakapofika Saa 6:00 usiku.

TCRA imesema kuwa itakapofika Saa 5:59 usiku laini zote ambazo hazijasajiliwa zitakoma kutumika mpaka pale watakapokamilisha usajili unaotakiwa na Serikali, jambo litakalowakosesha mamilioni huduma za mawasiliano.

Kaimu Meneja wa Mawasiliano wa TCRA, Semu Mwakanjala ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) leo (Januari 20, 2020) kuwa mbali na ambao hawajasajili kabisa kwa alama za vidole yapo makundi mengine yatakayoathirika na hatua hiyo ya Serikali. 

Kwa muda sasa kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa vitambulisho au namba za kitambulisho cha Taifa (NIN) jambo lililowafanya wengi kushindwa kusajili laini zao kwa wakati.

Serikali kwa sasa inasisitiza laini zote zisajiliwa na kitambulisho au namba ya utambulisho wa Taifa (NIN) zinazotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida). 

Desemba 27, 2019, Rais John Magufuli aliongeza siku 20 kwa watu wote walioshindwa kusajili laini zao za simu kwa alama za vidole kabla ya Desemba 31 na aliiagiza TCRA kuzima laini zote ambazo hazijasajiliwa baada ya muda huo kupita.

Hadi jana (Januari 19, 2020) ni zaidi ya nusu tu ya laini zilizopo sokoni Tanzania ndiyo zilikuwa zimesajiliwa kikamilifu. 

“Waliokamilisha usajili kwa alama ya vidole wamefika milioni 28.43  sawa na asilimia 58.2 ya jumla ya laini zilizopo sokoni ambazo ni  milioni 48.85. Wengine wamesajili lakini usajili wao haujakamilika,” amesema Mwakanjala.

Mwakanjala amesema mbali na wale ambao hawajajisajili kabisa na kitambulisho cha Taifa yapo makundi mengine yatakayozimiwa laini zao yakiwemo ya wale waliojisajili kwa kitambulisho cha Nida lakini taarifa zao hazijathibitishwa kwa alama za vidole. 

“Ambao wamesajili kwa namba ya kitambulisho cha Taifa lakini hawajathibitishwa kwa alama za vidole wako 318,950. Hawa hawajaweka utambuzi wa kipekee wa alama za vidole,” amesema.


Soma zaidi: 


Baadhi ya watu wengine ambao kuna cha changamoto katika usajili wao, kwa mujibu wa Mwakanjala, ni wale ambao laini zao za simu zilisajiliwa kibometria na majina mawili na tarehe za kuzaliwa za wamiliki yanafanana na majina ya NIDA ambao wanafikia milioni 3.26. 

“Kundi la mwisho ni laini za simu ambazo hali yake ya usajili haijulikani kwa sababu mbalimbali hawa wako milioni 16.19,” amesema.

“Wote ambao hawajakamilisha usajili watahusika kwenye kufungiwa laini.”

Mwakanjala amesema mchakato wa kusajili laini zitakazofungiwa utaendelea kama kawaida kwa wale wote watakaofungiwa.


Hatua hiyo ya Serikali kutangaza kuzima laini ambazo hazijasajili usiku wa leo imekosolewa na baadhi ya wadau kikiwemo cha upinzani cha ACT-Wazalendo kimenuia kufungua kesi mahakamani iwapo watu wasiosajiliwa watazamiwa mawasiliano. 

Katika mkutano wake leo na wanahabari jijini Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu amesema Serikali isitishe mpango huo na itoe fursa kupata nyenzo za kutosha kuwapatia wananchi vitambulisho ambavyo vinahitajika katika usajili wa laini hizo.

Shaibu amesema hatua hiyo itakuwa na athari kwa wananchi na Taifa kwa ujumla kutokana na umuhimu wa mawasiliano katika dunia ya sasa. 

“Uamuzi wa Serikali kuzima laini za simu utakuwa na athari kubwa kijamii na kiuchumi. Mbali na kuathiri mawasiliano baina ya watu, hatua hiyo itaathiri sana hali ya maisha ya watu kiuchumi.” amesema.

Amesema “iwapo serikali itaendelea na  msimamo wake wa kuzifungia laini zisizosajiliwa na zile za waliotuma maombi na hawajapata vitambulisho, sisi ACT Wazalendo tutaenda mahakamani kupinga jambo hili.”

Enable Notifications OK No thanks