Ahueni, maumivu: Bei ya maharage ikipanda
- Bei ya juu kabisa ya zao hilo imeshuhudiwa katika masoko ya mkoa wa Morogoro ambapo gunia la kilo 100 linauzwa kwa Sh265,000.
- Bei ya maharage ya gunia la kilo 100 inauzwa Sh260,000 katika soko la Kinondoni jijini Dar es Salaam ikiwa imeshuka kutoka Sh280,000 iliyorekodiwa juzi jijini humo.
- Bei ya chini katika mkoa wa Mara kwa Sh100,000 ambayo haijabadilika ikilinganishwa na jumatatu.
Dar es Salaam. Kwa mujibu wa takwimu za bei za jumla za mazao makuu ya chakula nchini zilizotolewa leo Machi 4, 2020 na Wizara ya Viwanda na Biashara, zinaonyesha kuwa bei ya maharage ya gunia la kilo 100 inauzwa Sh260,000 katika soko la Kinondoni jijini Dar es Salaam ikiwa imeshuka kutoka Sh280,000 iliyorekodiwa juzi jijini humo.
Hiyo ina maana kuwa kwa kila gunia moja, mfanyabiashara atapoteza Sh20,000 huku mununuzi ambaye ni mwananchi ataneemeka kwa sababu bei imeshuka.
Ifahamike kuwa utaratibu wa kutoa bei za jumla za mazao makuu ya chakula hufanyika mara tatu kwa wiki yaani Jumatatu, Jumatano na Ijumaa.
Hata hivyo, bei ya juu kabisa ya zao hilo imeshuhudiwa katika masoko ya mkoa wa Morogoro ambapo gunia la kilo 100 linauzwa kwa Sh265,000.
Bei hiyo ya juu mkoani humo haijabadilika tangu ijumaa Februari 28 licha ya kuwa imekuwa ikichuana na Dar es Salaam kuuza maharage kwa bei kubwa kuliko mikoa mingine Tanzania.
Zinazohusiana
Wakati Morogoro ikiuzwa maharage kwa bei juu, zao hilo linauzwa kwa bei ya chini katika mkoa wa Mara kwa Sh100,000 ambayo haijabadilika ikilinganishwa na jumatatu.
Tukiachana na maharage, leo walaji wa chipsi mkoani Mbeya kwao ni kicheko kwa sababu bei ya chini viazi mviringo inauzwa Sh45,000 katika soko la Mwanjelwa huku wenzao wa Lindi wakiuziwa Sh120,000 ikiwa ndiyo bei ya juu kabisa ya zao hilo leo sokoni.