Jinsi ya kujikinga na virusi vya Corona kwenye mikusanyiko ya watu

March 14, 2020 9:21 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Epuka ukaribu uliopitiliza ikiwemo kukumbatiana na kushikana mikono.
  • Kama unaweza kuepuka mikusanyiko ya watu itakuwa vema. 

Umetangazwa kuwa ni janga la dunia. Unaathiri shughuli za kiuchumi, kijamii na kisiasa. Unasambaa kwa kasi katika maeneo mbalimbali duniani. 

Viongozi na Serikali za nchi mbalimbali zinafanya kila liwezekanolo kuwalinda raia wao wasiupate ili maisha yaendelee kama kawaida. Tanzania siyo kisiwa na Watanzania wanapaswa kujikinga usiwapate.

Ni ugonjwa wa virusi vya Corona aina ya COVID-19 ambao chimbuko lake ni katika jimbo la Wuhan nchini China. Hauna dawa lakini wagonjwa wanatibiwa kutokana na dalili wanazopata. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), mpaka jana Machi 13, 2020) watu 132,758 wameambikizwa ugonjwa huo huku 4,955 wakifariki dunia katika nchi 122 duniani. China na Italia ni waathirika wakubwa wa virusi hivyo.

Hatua za haraka za kujikinga na ugonjwa huo ambazo WHO inashauri ni kutogusa mdomo, pua na macho, kuosha mikono mara kwa mara na kutumia tishu wakati wa kukohoa. 

Tahadhari ya juu ambayo imechukuliwa na nchi mbalimbali duniani ni kupunguza muingiliano wa watu, ambapo safari nyingi za kimataifa zimezuiliwa na watu wametakiwa kutulia katika maeneo yao.

Hapa Tanzania, Rais John Magufuli amewataka Watanzania kutosafiri nje ya nchi isipokuwa kama kuna sababu za msingi huku akiwataka watu kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima. 

Ifahamike kuwa hakuna hata mgonjwa mmoja aliyethibitika kuwa na ugonjwa wa virusi vya Corona nchini Tanzania.

Hata hivyo, mikusanyiko ya watu haiwezi kuzuiliwa moja kwa moja kwa sababu inatoa fursa kwa watu kuendelea na shughuli za maendeleo. 


Soma zaidi:


Kama utajikuta uko kwenye mkusanyiko wowote iwe ni kwenye tamasha, sherehe, mgahawa au kongamano, hizi ni miongoni mwa tahadhari unazoweza kuchukua kupunguza uwezekano wa kuambukizwa virusi vya Corona:

Epuka ukaribu uliopitiliza

Ni kawaida kwa marafiki na ndugu kukumbatiana, kushikana mikono na hata kupigana mabusu. Katika kipindi hiki ambacho kuna tishio la Corona unashauriwa usifanye hivyo kwa sababu ugonjwa huo unasambaa kwa hewa na kukaa karibu.

Hiyo haina maana kuwa ukae mbali kabisa na rafiki au ndugu yako wakati wa mikusanyiko, hapana! lakini epuka tabia ambazo umezoea kuzifanya kama kushikana mikono ili kukupunguzia uwezekano wa kupata virusi vya Corona.

Mikusnyiko inaweza kuwa sehemu hatarishi ya kusambaa kwa haraka kwa virusi vya Corona. Picha|Mtandao.

Usikae karibu na mtu anayekohoa au kupiga chafya

Baadhi ya nchi zimechukua hatua ya kusafisha vituo vya mabasi na daladala. Pia magari ya umma nayo yanapuliziwa dawa kabla ya kuanza safari ikiwa ni hatua ya kutokomeza virusi vya Corona. 

Nchini Rwanda, wameweka vifaa vya kunawia mikono kwenye vituo vya mabasi ambapo mtu hutakiwa kusafisha mikono yake kabla ya kuingia kwenye basi.

Lakini bado tunatakiwa tuchukue hatua zaidi. Baadhi ya watu wanasafiri wakiwa na magonjwa ya mafua na kikohozi. Inaweza kuwa ngumu kuwaepuka lakini unaweza kujikinga.

Unashauriwa kuwa kama umegundua mtu anakohoa au anapiga chafya, usikae naye karibu sana au geukia upande mwingine. Lakini ni muda wako muafaka wa kumfundisha kutumia tishu wakati anakohoa na akiitumia aitupe sehemu salama.

Osha mikono na usishike kila kitu

Katika mikusanyiko ya watu hasa kwenye migahawa au vyoo vya umma, yapo maeneo mengi yatakayokulazimisha kushika ili kutimiza lengo fulani ikiwemo vitasa vya milango na koki za bomba.

Kama kuna mtu mwenye virusi akashika vifaa hivyo, inaweza kuwa njia rahisi kuwaambukiza wengine.

Hata hivyo, usihofu! unachoshauriwa ni kunawa mikono ukifika na wakati wa kuondoka katika eneo husika. Kama ni mgahawani osha mikono kwa sabuni kabla na baada ya kula chakula. 

Na ukinawa usipeleke mikono yako usoni hasa kugusa pua, mdomo na macho. Hapo utakuwa umepunguza kwa sehemu kubwa uwezekano wa kupata virusi hivyo.


Tulia nyumbani, usiende kwenye mikusanyiko

Kama unahisi afya yako siyo njema kukuwezesha kukutana na watu, ni vema ukakaa nyumbani. Epuka mikusanyiko ya watu wengi kadri uwezavyo hasa ile inayohusisha watu wa mataifa yaliyoathirika na virusi hivyo.

Kukaa mbali na wagonjwa vya Corona siyo unyanyapaa bali ni hatua muhimu ya kudhibiti kusambaa kwa maambukizi. 

Enable Notifications OK No thanks