Kampuni, mashirika yafunga ofisi kujikinga na Corona Tanzania
- Waliofunga ofisi ni pamoja na Umoja wa Mataifa (UN), Jamii Forums na Code for Africa.
- Sababu kuu ni kuwalinda wafanyakazi wao na maambukizi ya virusi vya Corona.
- Wameshauri wengine kuchukua hatua hiyo.
Dar es Salaam. Kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Corona unaokabili dunia kwa sasa, baadhi ya mashirika na kampuni nchini Tanzania zimefunga ofisi zao na kuwataka wafanyakazi wao kufanyia kazi nyumbani ili kuwaepusha na maambukizi ya virusi hivyo.
Virusi hivyo ambavyo vimetangazwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kama janga la dunia umesababisha vifo vya watu 5,735 hadi jana (Machi 16, 2020) huku nchi za Italia na China zikiathirika zaidi.
Hatua za kufunga ofisi zilianza kuchukuliwa na taasisi na mashirika ya Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) ambapo Katibu Mkuu wake António Guterres amesema wafanyakazi wataanza kufanyia kazi nyumbani kuanzia leo (Machi16, 2020) hadi Aprili 12 mwaka huu.
Katika barua pepe yake kwa wafanyakazi wa UN mwishoni mwa juma, Guterres, amesisitiza kuwa, “shirika hilo liko wazi likiendelea kufanya kazi zake. Kazi yetu itakuwa inafanyika kutoka kona mbalimbali kwa kutumia teknolojia mbalimbali.”
Baadhi ya kampuni nchini zimefunga ofisi zao na kuwataka wafanyakazi wake kufanya kazi nyumbani.
Miongoni mwa kampuni hizo ni ya Code for Africa (CFA)imesema pia wafanyakazi wake wa nchini Tanzania, Nigeria, Afrika Kusini, Kenya na Uganda wataanza kufanyia kazi majumbani mwao kuanzia leo hadi mwongozo utakapotolewa.
“Tunawashauri na wadau wetu kufanya hivyo, ni kujiweka mbali na jamii na siyo kujiweka mbali na mtandao wa Slack (mtandao wa mawasilianowa kampuni hiyo),” imeeleza taarifa ya CFA katika ukurasa wake wa Twitter na kuongeza kuwa “biashara inaendelea kama kawaida.”
Mbali na Code for Africa, kampuni ya habari ya JamiiForums pia imetangaza kufunga ofisi na wafanyakazi hawatotakiwa kufika ofisini kwa siku 30 na watakuwa wanatekeleza majukumu yao wakiwa nyumbani.
Uamuzi uliofikiwa unachochewa na baadhi ya kampuni hizo kutumia teknolojia ambazo zinawezesha wafanyakazi hao kuendelea kutimiza majukumu yao popote walipo.
Zinazohusiana
- Jinsi ya kujikinga na virusi vya Corona kwenye mikusanyiko ya watu
- Magufuli aagiza safari za nje zipunguzwe kujikinga na virusi vya Corona
Pia baadhi ya wafanyakazi wa kampuni ya mawasilino ya simu ya Vodacom Tanzania leo hawakuingia ofisini, ikiwa ni majaribio ya kutekeleza majukumu yao wakiwa nyumbani.
Meneja Uhusiano Alex Bitekeye wa kampuni hiyo ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa ofisi iliyofungwa ni ya makao makuu iliyopo Morocco jijini Dar es Salaam lakini shughuli za matawi mengine ya kampuni hiyo zinaendelea kama kawaida.
“Sio wafanyakazi wote, ni wa makao makuu tu, unaangalia kama inawezekana kufanya hivyo. Kesho watarudi kazini,” amesema Bitekeye.
Katika maeneo mbalimbali duniani, Serikali zinaendelea hatua mbalimbali kujikinga na virusi hivyo ikiwemo kuzuia watu kusafiri, kukusanyika katika maeneo ya umma na kutakiwa kubaki nyumbani.