Filamu zitakazokusaidia kumalizia wiki kwa furaha

March 28, 2020 12:43 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni za  “City Of Lies” na “Jexi” zilizoanza kuonyeshwa kuanzia jana Machi 27, 2020 hadi Ijumaa ya wiki ijayo.
  • Zimejaa visa na mikasa itakayokuacha mdomo wazi kipindi hiki cha mlipuko wa virusi vya Corona.  

Dar es Salaam. Ni wikiendi nyingine tena kwa wapenzi wa filamu hasa zile zilizojaa mikasa ya kusisimua na mafunzo mbalimbali, kupata furaha hasa kipindi hiki cha kuenea kwa ugonjwa wa virusi vya Corona ambavyo vimeleta hofu duniani. 

Hata kama ugonjwa huo unaendelea kusambaa, bado una nafasi ya kufurahia maisha yako hasa kama filamu zinazoonyeshwa katika kumbi mbalimbali Tanzania ni burudani kwako. 

Nukta (www.nukta.co.tz) inakuletea uchambuzi wa filamu mbili za  “City Of Lies” na “Jexi” zilizoanza kuonyeshwa kuanzia jana Machi 27, 2020 hadi Ijumaa ya wiki ijayo. Filamu hizo ambazo zinazungumzia uhalifu na mapenzi ya vifaa vya kielektroniki, hakika hazikuacha kama ulivyo baada ya kuzitazama.

City Of Lies

Ni filamu iliyoongozwa na muongozaji  Brad Furman inayowakutanisha mastaa Johnny Depp, Forest Whitaker na Toby Huss katika visa vya mapigano katika jiji lililojaa kila namna ya uongo na kusalitiana. Watafanikishaje kazi waliyopewa? Ni Russell Poole na Jack Jackson waliopewa kibarua cha kuchunguza mauaji ya marapa wawili wa Marekani Notorious B.I.G na Tupac Shakur. 

Kazi hiyo waliyopewa siyo rahisi hata kidogo kwani wanatakiwa kupangua kila na namna ya uongo uliojificha katika mauaji ya marapa hao wawili. Ni mapigano na kila namna ya vurugu katika mji ili kuwapata wauaji. 

Nini kitatokea? Usisite kwenda kuangalia filamu hii Mlimani City, Mkuki House na City Mall jijini Dar es Salaam. Kama hutaki fujo inayoumiza basi machozi na kubana mbavu kunakuhusu katika filamu ya Jexi.


Zinazohusiana


Kuna nini kwenye Jexi?

Humu utakutana na waongozaji Jon Lucas na Scott Moore ambao ni vichwa nyuma ya filamu hii ambayo iko katika mtindo wa vichekesho lakini imejaa mafunzo mengi. 

Itakufunza madhara ya kupenda kitu fulani kupita kawaida na jinsi unaweza kupoteza mahusiano na wale uwapendao. 

Inawakutanisha mastaa Adam Devine, Alexandra Shipp na Rose Byrne katika kisa kilichojaa vichekesho ambavyo vinahitaji kuwa na kitambaa cha kujifuta machozi. 

Kinaeleza nini kinachoweza kutokea ikiwa unaipenda sana simu yako kuliko kitu chochote katika maisha yako. 

Usibaki nyumbani wikiendi hii, nenda katika kumbi za senema huku ukichukua tahadhari zote za kujikinga na virusi vya Corona ikiwemo kuepuka kugusana na mikusanyiko isiyo ya lazima. 

Kama unapenda kutazama filamu hizo ukiwa nyumbani unaweza kutumia mtandao wa Netflix.

Enable Notifications OK No thanks