Serikali kurekebisha makosa ununuzi wa pamba Tanzania

May 2, 2020 8:57 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya akiwa ameshika mashine inayotumika kuchambua na kutenganisha pamba mbegu na pamba sufi alipotembela kiwanda cha kuchambua pamba cha Chato. Picha| Wizara ya Kilimo.


  • Serikali yasema itasaidia kuondoa changamoto zilizojitokeza msimu wa 2019.
  • Changamoto hizo ni kuuza pamba kabla haijakomaa na wakulima kutolipwa kwa wakati.
  • Wakulima watakiwa kuongeza uzalishaji wa zao ili kufaidika na soko.

Dar es Salaam. Serikali imesema inafanya tathmini ya hali ya ununuzi wa zao la pamba kwa msimu wa mwaka 2019 ili kuondoa changamoto zilizojitokeza kabla msimu mpya wa ununuzi wa zao kuanza mwaka huu ikiwemo kulipa madeni ya wakulima. 

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya amesema msimu mpya wa ununuzi wa pamba utatangazwa mara baada ya tathmini ya msimu uliopita kufanyika.

“Wizara imegundua kuwa hali ya mazao shambani bado kwani hata vitumba bado havijapasuka kutokana na uwepo mvua nyingi, hivyo baada ya ziara hii kwenye mikoa ya kanda ya ziwa Serikali itakaa na watalaam ili kuamua lini wakulima wataanza kuuza pamba yao kupitia Vyama Vya Ushirika vya Msingi (AMCOS),” amesema Kusaya. 

Amesema tathmini hiyo pia itahakikisha madeni ya wakulima, wanunuzi na ushuru wa AMCOS, halmashauri pamoja na mfuko wa pembejeo yanalipwa.

“Kila mwananchi atalipwa madai yake na jitihada za Serikali ni kuona madeni haya yanalipwa kabla ya msimu mpya wa ununuzi wa pamba kuanza,” ameeleza bois huyo mpya wakati akizungumza na viongozi wa Wilaya ya Chato Mei Mosi, 2020.  


Soma zaidi: Wakulima kuuza pamba kwa bei wanayoitaka


Aidha, Chama Kikuu cha Ushirika Chato (CCU) kimetakiwa kuhamasisha wakulima wengi zaidi kuzalisha zao la pamba ili ipate malighafi za kutosha kutumika kwenye kiwanda chake cha kuchambua pamba.

Kusaya ametoa maagizo hayo kufuatia taarifa ya Meneja Mkuu wa Chama hicho Joseph Masingiri kusema kiwanda kimeshindwa kuendelea na uchakataji marobota kutokana na uhaba wa pamba ambapo msimu wa 2019 ni kilo milioni 13.6 tu ndiyo zilinunuliwa wakati uwezo wake ni kilo milioni 30.

Ili kukabiliana na changamoto za zao hilo, Katibu Mkuu amewataka wataalam wa halmashauri na wa chama kikuu kuhamasisha wakulima kuzalisha mazao ya mkonge na korosho ili kuwa na uhakika wa kipato pale zao la  pamba linapoyumba.

“Tulime pamba na mazao mengine ya biashara kama mkonge na korosho yanayostawi vizuri kwenye mkoa huu wa Geita na kanda ya ziwa yote. Wizara ya kilimo ipo tayari kuleta mbegu bora za mkonge na korosho toka taasisi za utafiti ili zigawiwe kwa wakulima,” amesema Kusaya.

Kusaya alitaja faida za zao la mkonge kuwa katika kipindi cha miaka mitatu  baada ya kupanda mkulima ataanza kuvuna na kuendelea hadi miaka kumi na tano huku akiendelea na kilimo cha mazao mengine .

Pamba inategemewa zaidi na wakulima wa mikoa ya Simiyu, Mwanza, Shinyanga, Geita, Tabora, Mara, Kagera, Singida, Kigoma na Katavi, ambapo ni miongoni mwa mazao saba ya biashara yanayoingiza fedha nyingi za kigeni. 

Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2018 kinaeleza kuwa mwaka 2018, thamani ya mauzo ya katani nje ya nchi ilikuwa dola za Marekani milioni 33.2 (Sh76.8 bilioni) ikilinganishwa na dola milioni 28.7 (Sh66.4 bilioni) mwaka 2017, sawa na ongezeko la asilimia 15.7.

Enable Notifications OK No thanks