Corona: Njaa kuongezeka zaidi ya mara mbili Afrika Mashariki
- WFP imesema watu wasio na uhakika wa chakula katika ukanda huo wataongezeka kati ya milioni 34 na milioni 43 kuanzia mwezi huu wa Mei hadi Julai.
- Athari za kiuchumi na kijamii za COVID-19 zimechangia tatizo hilo.
- Walio katika hatari ya kupata njaa zaidi ni wakimbizi na watu wanaotegemea ajira zisizo rasmi.
Dar es Salaam. Ripoti mpya iliyotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani (WFP) imeeleza kuwa tatizo la njaa linaweza kuongezeka zaidi ya mara mbili katika nchi za Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika katika miezi mitatu ijayo kutokana na athari za virusi vya Corona.
Ripoti hiyo kuhusu athari za kijamii na kiuchumi za janga la Corona (COVID-19) iliyotolewa jana mjini Nairobi Kenya imesema watu walio katika hatari zaidi ya njaa ni watu wanaoishi mjini ambao wanategemea kipato cha siku kwa ajili ya mlo kutoka kwenye sekta zisizo rasmi.
Pia na wakimbizi wanaoishi katika kambi mbalimbali za wakimbizi walioko katika ukanda huo.
Ripoti hiyo inakadiria kuwa idadi ya watu wasio na uhakika wa chakula katika ukanda huo inatarajia kuongezeka kati ya milioni 34 na milioni 43 kuanzia mwezi huu wa Mei hadi Julai kutokana na athari za kiuchumi na kijamii za COVID-19.
Na endapo idadi hiyo itafikia milioni 43, WFP imesema itakuwa imeongezeka zaidi ya mara mbili katika kipindi hicho.
Zinazohusiana:
- Wakulima wanavyopigania bei nzuri ya mahindi Afrika Mashariki.
- Mnada wa kahawa kuwanufaisha wakulima?
Hata hivyo, WFP imesema takribani watu milioni 20 tayari walikuwa wanakabiliwa na kutokuwa na uhakika wa chakula hata kabla ya COVID-19 kuwasili katika ukanda.
Hiyo ilitokana na mgogoro mkubwa wa chakula, mlipuko wa nzige wa jangwani na mafuriko yanayotishia maisha ya mamilioni ya watu hasa katika nchi za Ethiopia, Sudan Kusini, Kenya, Somalia, Uganda, Rwanda, Burundi, Djibout na Eritrea.
Naibu Mkurugenzi wa kikanda wa WFP Brenda Behan amesema watu zaidi wanatarajiwa kufa kutokana na athari za kiuchumi na kijamii za COVID-19 kuliko virusi vyenyewe huku wakimbizi na watu maskini wanaoishi mjini katika ukanda huo wako katika hatari kubwa zaidi.
Ripoti imesema watu milioni 25 Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika wanaishi kwa kutegemea kipato cha siku wakiishi kwenye mitaa ya mabanda au makazi duni na mamilioni wameshapoteza ajira kutokana na hatua za kutotembea au kusalia majumbani kupambana na COVID-19.
Tayari WFP ina ukurasa wake wa wavuti ambao unaonesha mubashara hali ya njaa katika maeneo mbalimbali duniani ili kuwasaidia watunga sera kuangalia maeneo wanayoweza kupeleka chakula.
Latest