Barrick yaanza kuilipa Tanzania mabilioni, makinikia yakiruhusiwa
- Barrick yasema imeshalipa Sh229 bilioni za awali baada ya kuuza makinikia.
- Makontena 1,600 ya mchanga wa dhahabu kusafirishwa.
Dar es Salaam. Hatimaye makontena ya makinikia ya dhahabu yaliyokuwa yamekwama bandarini kwa miaka mitatu yameanza kusafirishwa nje ya nchi huku kampuni ya madini ya Barrick Gold ikieleza kuwa imeshaanza kulipa sehemu ya makubaliano ya zaidi ya Sh680 bilioni iliyokubaliana na Serikali.
Taarifa ya Barrick iliyotolewa Mei 25, 2020 imeeleza kuwa mbali na makinikia imekamilisha asilimia 90 ya madai yote yahusuyo ardhi katika mgodi wa North Mara huku malipo yakitarajiwa kuanza kulipwa leo.
Barrick imesema usafirishaji wa sehemu ya makontena 1,600 ya makinikia kutoka katika migodi ya Bulyanhulu na Buzwagi ulianza mapema Aprili mwaka huu.
“Kiwango cha Dola za Marekani milioni 100 (Sh229 bilioni) zilizopatikana kutokana na mauzo hayo kilipelekwa serikalini,” imeeleza taarifa hiyo ya Barrick.
“Malipo haya ya awali yatafuatiwa na awamu tano za malipo ya Dola za Marekani milioni 40 (Sh91.6 bilioni) kila mwaka,” imeongeza.
Malipo hayo ni sehemu ya Dola za Marekani milioni 300 (zaidi ya Sh684 bilioni) ambazo ni moja ya makubaliano ya kumaliza mgogoro wa muda mrefu ambao Barrick Gold uliurithi kutoka katika kampuni yake tanzu ya Acacia Mining.
Zinazohusiana:
- Magufuli aagiza makinikia yaliyozuiwa bandarini kupigwa mnada
- Rais Magufuli awaweka kitanzini wakuu wa mikoa wasiojenga vituo vya kuuzia madini
- Uzalishaji wa dhahabu Acacia washuka
Rais na Mtendaji Mkuu wa Barrick Gold (NYSE:GOLD) (TSX:ABX0) Mark Bristow amesema matukio hayo ni sehemu za kuimarisha ushirikiano baina yake na Serikali kupitia kampuni ya Twiga Minerals iliyoanzishwa kwa ajili ya kusimamia rasilimali za madini za kampuni hiyo.
Katika kampuni hiyo ya Twiga Minerals, Barrick Gold inamiliki asilimia 84 wakati Serikali ikimiliki asilimia 16.
Mapema leo Katibu Mkuu Wizara ya Madini Prof Simon Msanjila aliieleza Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa Twiga wameruhusiwa kusafirisha makontena hayo ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli mapema Januari mwaka huu.
“Rais aliagiza live (mubashara) kwenye televisheni kuwa makontena yale yaruhusiwe…lilikuwa ni suala la lini tu yaruhusiwe. Wale wanaohusika kutekeleza agizo hilo kwa mujibu wa sheria wameshakamilisha taratibu zote na Twiga wameruhusiwa,” amesema Prof Msanjila.
Kuhusu wachimbaji wengine waliokuwa na makontena yaliyokwama bandarini, Prof Msanjila amesema kila mmoja alijibiwa kwa kadri alivyoomba.