Tecno Spark 5: Simu maalum kwa wapenzi wa picha

June 15, 2020 4:03 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni simu iliyozinduliwa Mei, 2020 huku ikiipiga kikumbo Spark 4 ambayo ni toleo la zamani.
  • Simu hii ina kamera nne za nyuma na moja ya mbele zitakupatia sababu ya kupiga picha popote utakapopata wazo.
  • Inakuwezesha kuwa kumbukumbu nzuri za picha za mnato na video. 

Dar es Salaam. Endapo idadi ya kamera ndiyo sababu inayokufanya ununue simu, basi hakika hautakaukiwa na mshawasha wa kuitafuta simu mpya kutoka kampuni ya Tecno popote ilipo.

Wameingiza sokoni simu mpya ya Tecno Spark 5. Simu hii ina kamera nne za nyuma na moja ya mbele zitakupatia sababu ya kupiga picha popote utakapopata wazo la kufanya hivyo bila kujali yakuzungukayo.

Simu hiyo iliyo na kamera yenye uwezo wa megagapikseli (MP) 13 imeambatana na kamera yenye intelijensia undwa (AI) inayotofautisha kilichopo mbele ya kamera na vile vilivyopo nyuma.

Kwenye simu zingine, teknolojia hii inafahamika kama “potrait mode”.

Kamera yake ya mbele ina ukubwa wa megapikseli 8 sawa na simu nyingi zikiwemo Huawei Honor 8 ya mwaka 2016 na Motorola G5S Plus (2017)

Spark 5 ina rangi nne ili kumpatia mchaguaji nafasi ya kuchagua anayoipenda. Picha| NNX.

Kamera zake za nyuma zinatofautiana matumizi kwani ipo inayopiga picha kwa upana zaidi yaani “Panorama” , yenye “AI” ni kamera ya kawaida na kamera yenye kupiga picha za usiku kana kwamba hakuna giza.

Hata hivyo kama ni kamera, simu hii haijafua dafu kwa Tecno Canon 15 ambayo kamera yakeya nyuma ina ukubwa wa MP48 huku ya mbele ikiwa na MP16.

Mbali na kamera, Tecno Spark 5 ina uwezo wa kuhifadhi vitu vyenye ukubwa wa jigabaiti (GB) 32 na uhifadhi wa ndani (RAM) ya GB2 ambayo hutumika kuhifadhi programu tumishi za simu.

Uhifadhi huo unaweza kutunza hadi picha 1,800, dakika 160 za video, nyimbo 4,000 na na mafaili ya ofisini yenye ukubwa wa GB 16. 

Angalizo! Uhifadhi huu unaweza kuwa tofauti kulingana na ukubwa wa mafaili yako.

Hata hivyo, uwezo wake wa kuhifadhi kumbukumbu hauwezi kushindana na simu ambazo tayari zipo sokoni zikiwemo za Samsung Galaxy A9, Huawei Enjoy Z 5G na hata Tecno Spark4.


Zinazohusiana


Betri la simu hii lina uwezo wa mAh5000 ambayo ni kubwa kulinganisha na toleo lililopita la Tecno spark 4 ambayo ina uwezo wa mAh 4000 hivyo kuwa na uwezo wa kukaa hadi siku tatu bila kuchaji kwa mtu mwenye matumizi ya kawaida.

Toleo hili lililozinduliwa Mei 2020 linakuja na ukubwa wa inchi 6.60 unaotumia uzao wa 10 wa teknolojia ya Android. 

Skrini yake inayoonyesha vitu kwa ubora wa pikseli 720×1600 ni zaidi ya spark 4 huku ikija kwa rangi nyeusi, machungwa, bluu na kijani na hivyo kumpatia mtumiaji nafasi nzuri ya kuchagua.

Spark 5 inakuja na redio huku ulinzi wake ukiwa na teknolojia ya kuskani sura yaani “face unlock” na kuskani alama za vidole. Pia, ina uwezo wa kutumia laini mbili za simu zenye uwezo wa 4G.

Kama unataka picha nzuri kwa ajili ya kumbukumbu zako basi simu hii inaweza kukufaa. 

Kwenye maduka yanayouza simu za Tecno yakiwemo ya Mlimani City, simu hii inauzwa kwa Sh350,000.

Enable Notifications OK No thanks