Simu ya LG Velvet: Ni doa kwa matoleo ya simu za LG?

June 29, 2020 8:39 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kati ya simu iliyolalamikiwa kutokukidhi ushindani na matoleo ya mwaka 2020.
  • Muonekano wa simu hiyo hausadifu yaliyomo ikiwemo ubora wa skrini yake.
  • Kamera yake imepata ushindani mkali kutoka simu nyingine ikiwemo Samsung na iPhone.

Dar es Salaam. Ni kawaida kwa kampuni ya LG inayotengeneza vifaa vya kielektroniki vikiwemo simu, majokofu na viyoyozi kuibuka na bidhaa zenye muundo wa aina yake.

Kama wewe ni mfuatiliaji wa bidhaa za simu, bila shaka umewahi kusikia simu ya LG G Flex ambayo ilikuja na muundo wa kupinda kidogo ikiwa ni mapinduzi yaliyofanyika katika teknolojia ya simu janja.

Pia ni miongoni mwa kampuni za simu zilizoanza kutoa simu yenye kamera mbili za nyuma kupitia simu yake ya  LG Optimus 3D.

Kampuni hiyo haijaishia hapo kwani imeendelea kuingiza simu zenye muonekano wa tofauti sokoni zikiwemo LG V20, G7, V40, na G8. Kwa toleo la mwaka huu ambalo limeingizwa sokoni Mei 2020, LG imefanya yasiyotarajiwa na simu yake mpya ya LG Velvet.

Ni dhahiri kuwa muonekano wa simu hiyo inayogharimu Sh1.7 milioni unaweza kukufanya uvunje kibubu chako au hata ukafilisi akaunti yao ya benki kuinunua lakini je yaliyomo yamo?

Ni kawaida kwa kampuni ya LG inayotengeneza vifaa vya kielektroniki vikiwemo simu, majokofu na viyoyozi kuibuka na bidhaa zenye muundo wa aina yake. Picha| Mr phone.

Uhifadhi wa kumbukumbu

Kwa upande wa uhifadhi, LG haijawahi kukuangusha tangu toleo la V Series ambapo hazijawahi kupungua Jigabaiti (GB) 32 kwa simu huku uhifadhi wake wa ndani (RAM) ikiwa ni GB4.

Kwa Lg Velvet, hali ni ile ile kwani ina uwezo wa uhifadhi wa RAM kwa ukubwa wa GB4 huku uhifadhi wa kawaida ukiwa ni GB128.

Uwezo wa betri

Betri la simu hiyo pia limesifiwa kwa ubora wake kwani lina uwezo wa mAh 4300 na hivyo kuwa bora zaidi ya simu zingine zilizopo sokoni zikiwemo Samsung Galaxy C9 Pro na hata Samsng galaxy S20.

Hiyo ni sawa kusema kwa mtu mwenye matumizi ya kawaida, anaweza kutumia simu hiyo bila kuichaji kwa zaidi ya saa tano.


Zinazohusiana


Uwezo wa kamera

Kwa mujibu wa tovuti ya Tech Radar,  LG hawajafanya vizuri katika eneo la kamera.

Siyo kwamba ni mbaya, lakini kamera za simu hiyo siyo nzuri kwa watu wanaopenda kupiga picha wakiwemo watengeneza maudhui ya picha za mnato na video. 

Muonekano wa kamera kwa nje ni mzuri, lakini utendaji kazi wake hauridhishi ikilinganisha na simu zingine zinazokuja na kamera tatu ikiwemo  iPhone 11.

Licha ya kuwa ukubwa wake ni sawa na simu ya Nokia 7.3, bado wadau wa simu janja wakiwemo Tech Radar wamesema kamera yake hairidhishi hasa kwa upigaji wa picha katika maeneno yenye mwanga hafifu.

Mbali na mambo hayo ambayo huenda siyo kitu kwa baadhi ya wadau wa simu za LG, muonekano wa mpangilio wa simu hiyo inapowashwa bado hauridhishi kushindana na simu zilizopo sokoni kama Samsung Galaxy S 20 na iPhone 11.

Hata wakati LG ikisifika kuwa na simu zenye mifumo ya sauti mizuri, kwa Velvet mambo sivyo yalivyo kwani teknolojia yake ya kuongeza uwezo wa sauti (boosting) haijatumika katika simu hii. 

Zaidi ni kuwa, mfumo wa kuskani alama za vidole unaokuja na simu hii unatajwa kufanya kazi taratibu ikilinganishwa na simu nyingine. 

Usikose muendelezo wa chambuzi za simu kupitia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) ambapo makala ijayo, utaweza kuelewa kwanini simu janja matoleo ya “Curve” zikiwemo Samsung Edge zinapata msitari mwekundu kwenye skrini yake.

Enable Notifications OK No thanks