Corona yachangia wanafunzi 4,000 kupata mimba Kenya
- Ni wasichana wa shule za msingi na sekondari kutoka kaunti ya Machakos.
- Wamepata mimba hizo kati ya Januari hadi Mei hasa wakiwa nyumbani baada ya mlipuko wa virusi vya Corona.
Dar es Salaam. Kumekuwa na ujumbe unaosambaa kwenye mitandao ya kijamii hasa WhatsApp unaoeleza Kenya imetangaza kuwa wanafunzi wa kike 4,000 wamepata mimba wakati wa janga la virusi vya Corona.
Ni kweli matukio hato yametokea Kenya katika vipindi tofauti, jambo linalokatisha ndoto za masomo za wasichana hao ambao wameripotiwa katika kaunti ya Machakos.
Habari hiyo iliyoandikwa kwa lugha ya Kiswahili kwenye picha hiyo yenye bendera ya Kenya inaeleza kuwa “Kenya -Yatangaza mimba elfu nne (4000) za wanafunzi katika kipindi cha corona”
Huku chini ya picha hiyo kukiwa na swali linalo uliza Je kati ya mzazi na mwalimu ni nani mlezi bora?
Ukweli ni upi
Nukta Fakti imebaini ni kweli nchini Kenya wanafunzi 4,000 wamepata ujauzito katika kipindi hicho cha corona katika kaunti ya Machakos.
Afisa Watoto katika kaunti ya Machakos, Salome Muthama akihojiwa na televisheni ya Citizen amesema wanafunzi hao wa shule za msingi na sekondari wamepata mimba kati ya Januari na Mei mwaka huu.
Pia Muthama alinukuliwa katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Azam cha nchini Tanzania televisheni cha Azam Tv .
“Katika kaunti ya Machakosi wakati wa corona wasichana 4,000 wamepachikwa mimba na hiyo ni namba kubwa sana na ukizingatia ni kuanzia Januaria hadi Mei hiyo ni miezi minne tu watoto wa chini ya umri wa miaka 19 wamepata mimba,” amesema Muthama katika mahojiano hayo.