Mradi mkubwa wa umemejua ulivyoanza kutoa neema Dodoma

July 28, 2020 4:32 am · Habel
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni wakazi wa Mtaa wa Michese ambao wamepata fidia ya zaidi ya Sh3 bilioni kupisha mradi wa umemejua.
  • Fidia hiyo wameitumia kujenga nyumba za kisasa na kuingia kwenye ujasiriamali.
  • Serikali yasema itaendelea kushirikiana na wawekezaji kuongeza kasi ya uunganishaji wa umemejua Tanzania. 

Dodoma. Ni kama ndoto. Maisha yao yamebadilika ghafla, sasa angalau tabasamu linaanza kuonekana usoni baada ya kuwa na uhakika wa kipato cha kuboresha maisha yao kwa sasa na baadaye. 

Awali wakazi wa Michese katika kitongoji cha Bwawani kilichopo kilomita 17 Magharibi mwa Jiji la Dodoma walikuwa hawajawahi kufikiria kama umeme ungewafikia siku za hivi karibuni. 

Hata wakati wakisubiri umemejua kufungwa katika eneo lao, tayari wameanza kuonja matunda ya nishati hiyo baada ya baadhi yao kupata fidia kupisha mradi huo. 

“Tumelipwa fidia katika mradi ambao tunaungoja kwa hamu kubwa, kwanza lazima utambue kuwa, mradi huu unakuja kujengwa hapa kwetu mahali ambapo hatujawa na umeme, sasa tunaungoja kwa hamu kubwa kweli,” anasema John Satima, mkazi wa mtaa huo ambaye naye amenufaika na fidia hiyo. 

Wakazi hao waliopisha mradi huo wanaona kama ndoto kwa sababu ingewachukua muda mrefu kwa wao kuboresha maisha kutokana na umaskini wa kipato unaowakabili. 

Idadi kubwa ya wakazi wa eneo hilo ni wakulima na wafugaji ambao walionekana kuwa nyuma zaidi katika maendeleo na kijiji chao kimekuwa  mahali pa kuzalisha walinzi wa maduka ya matajiri katikati ya jiji la Dodoma.

Lakini sasa hali ni tofauti, maisha yamebadilika, wamepata nyumba nzuri za kuishi, wamejiingiza katika ujasiliamali na upangishaji wa nyumba huku wakiwa na matumaini makubwa ya kutumia umemejua utakaozalishwa katika mtaa wao.

Uchukuaji wa ardhi ya wananchi wa eneo hilo ulifanyika kwa makubaliano ambako malipo yalikuwa Sh1,500 kwa kila mita moja ya mraba na Serikali imelipa fidi ya Sh3 bilioni.

Mkazi wa Michese Christina Chibago akiwa nyuma ya nyumba yake mpya aliyoijenga baada ya kulipwa fidia ya shamba lake ili kupisha mradi mkubwa wa umemejua unaojengwa na Serikali. Kushoto ni nyumba ndogo ya tembe alimokuwa anaishi kabla. Picha|Habel Chidawali.

Mkazi mwingine wa mtaa wa Michese, Nichoraus Thadayo anasema licha ya kuwa wamepata fidia hiyo lakini ndoto yao ni kuona wanapata umemejua wa uhakika ili kuondokana na matumizi ya nishati ya mkaa na kuni  ambayo ina madhara kiafya. 

“Tulikubali kulipwa fidia, tumeahidiwa kuwekewa umeme wa uhakika kutokana na mradi utakaofungwa hapa kwetu, matumaini yetu ni makubwa zaidi kuwa ipo siku tutafungiwa umemejua, ngoja tuvute subira,” anasema Thadayo.

Ripoti ya Hali ya Upatikanaji wa Nishati ya Mwaka 2016 ya Tanzania Bara iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaeleza kuwa zaidi ya nusu ay asilimia 54.3 ya kaya za Mkoa wa Dodoma zimeungwanishwa na nishati ya umemejua huku matumizi ya mkaa na kuni yakiwa juu. 

Kaya zinazotumia umemejua katika mkoa huo ziko juu ya wastani wa kitaifa ambao kwa mujibu wa ripoti hiyo robo au asilimia 24.7 ya kaya zote za Tanzania Bara zimeunganishwa na nishati hiyo. 

Huenda ujenzi wa mradi wa umemejua wa Michese ukaongeza idadi ya kaya mkoani humo zinazotumia nishati safi na endelevu ya mwanga inayosaidia katika utunzaji wa mazingira.


Soma zaidi:


Megawati 60 kuzalishwa Michese

Mradi wa umemejua wa Michese ni miongoni mwa miradi mikubwa ya umemejua nchini. 

Meneja Mipango na Mikakati wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Costa Rubagumya anasema wanatarajia kuzalisha megawati 60 katika eneo hilo ingawa vipimo vimethibitisha kuwa wanaweza kuzalisha zaidi ya hapo.

Upembuzi yakinifu wa eneo hilo umekamilika na Rubagumya anasema wamelipa zaidi ya Sh3 bilioni kwa wakazi 296 ambapo walimiliki eneo lenye ukubwa wa ekari 130 zilizochukuliwa kwa ajili ya uwekezaji wa mradi wa umemejua

“Mradi wa umeme wa Michese unakwenda vizuri, tunatarajia kuwa utakamilika ifikapo 2026 au chini ya hapo, bado tunaendelea kujivunia na kufurahia uwepo wa vyanzo vingi vya umeme katika Taifa letu lakini cha msingi ni kuona gharama zake zinakuwa rafiki kwa watumiaji,” amesema Rubagumya.

Anasema mradi huo ni miongoni mwa miradi itakayowaletea ahueni wananchi ambao wanatumia gharama kubwa kupata umemejua unaozalishwa na kampuni za watu binafsi. 

Mradi huo wa umemejua utazalisha umeme utakaoingizwa kwenye gridi ya Taifa ambapo utawanufaisha Watanzania katika shughuli mbalimbali za uzalishaji. 

“Tunajenga miradi mikubwa ya umeme ambayo inasimamiwa na Serikali na kutumia mabilioni ya fedha, lakini kwa namna nyingine hatuwezi kuacha umeme jadidifu kwani nao una mchango wake katika maeneo ambayo hatujafika,” amesema Rubagumya.

Katika bajeti kuu ya Serikali ya mwaka 2020/21, Serikali inataja zaidi ya vijiji 3,000 kuwa bado havijafikiwa na huduma ya umeme na inafanya jitihada mbalimbali kwa kushirikiana na wawekezaji kuhakikisha inafikisha nishati katika maeneo hayo.

John Satima mkazi wa Michese akionyesha mabaki ya nyumba yake ambapo alibomoa ili kupisha mradi wa umemejua unaotarajia kujengwa mahali hapo. Picha|Habel Chidawali.

Serikali ilivyojipanga kuendeleza nishati jadidifu

Serikali imesema itaendelea kushirikiana na wawekezaji binafsi ili kuhakikisha watoa msukumo kuendeleaza nishati jadidifu ikiwemo umemejua ili kuwafikiwa Watanzania wengi kwa nishati. 

Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano wa MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Titus Kaguo anasema ushirikiano wao na watoa huduma za umemejua umeimarika wataendelea kuhakikisha nishati hiyo inaendana na hali za wananchi. 

Kaguo amesema katika kutambua hilo, Waziri wa Nishati Dk Medard Kalemani hivi karibuni atakutana na wawekezaji wa nishati jadidifu ili kujadiliana na namna nzuri ya kuendeleza nishati na kuhakikisha bei wanazotozwa wananchi zinaendana na gharama za uzalishaji.

Naibu Waziri Subira Mgalu amesema Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano mkubwa wawekezaji wa nishati jadidifu ikiwemo umemejua popote wanapoona kuna fursa kwani kuna maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma hiyo. 

Hata hivyo, amewataka kutoza gharama rafiki kwa wananchi ili kuongeza kasi ya wananchi kutumia umemejua.

/
No matches found for this filter
No forex gainers today
No forex losers today
26 May, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
26 May, 2026
No active movers today
Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
MIKOA 5 YA KIPOLISI INAYOONGOZA KWA MAKOSA BARABARANI

MIKOA 5 YA KIPOLISI INAYOONGOZA KWA MAKOSA BARABARANI

Nukta TV

SERIKALI YAKAMILISHA MAZUNGUMZO MRADI WA LIGANGA NA MCHUCHUMA

SERIKALI YAKAMILISHA MAZUNGUMZO MRADI WA LIGANGA NA MCHUCHUMA

Nukta TV

🔴LIVE: KAPINGA AKIWASILISHA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA 2026/2027 BUNGENI.

🔴LIVE: KAPINGA AKIWASILISHA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA 2026/2027 BUNGENI.

Nukta TV