Mabinti Watanzania wang’ara kwa kubuni teknolojia ya kupambana na ukame
- Ni baada ya kuibuka na mradi wa kustawisha malisho ya wanyama kwa siku saba.
- Ajabu ni kuwa, mradi huo unastawisha malisho ya wanyama bila kutumia udongo.
- “Hydroponic fodder” ni mradi unaozalisha chakula chenye virutubisho vifaavyo kwenye ukuaji wa wanyama na kukuza uchumi wa mfugaji.
Dar es Salaam. Wakiwa bado mabinti wadogo Glory Joseph na Martha Machumu, wanafunzi wa kidato cha tano kutoka Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Ngaza iliyopo jijini Mwanza, wameanza safari yao kitaaluma katika masuala ya teknolojia na sayansi vizuri.
Mabinti hao, ni miongoni mwa wasichana na wanawake wachache nchini Tanzania wanaothibitisha kuwa masuala ya sayansi na teknolojia hayategemei jinsia ili kuyamudu ipasavyo.
Kwa kipindi kirefu sana kumekuwepo kasumba kuwa mambo ya teknolojia na sayansi yanahusu wanaume pekee, jambo lililofanya wanawake kuwa nyuma katika kufaidi fursa zilizopo katika tasnia hiyo.
Hata hivyo, huenda kwa sasa wahamasishaji wa sayansi na teknolojia kwa wasichana angalau wakapata tabasamu baada ya kuwepo na muamko wa wasichana katika kuibua teknolojia zinazolenga kutatua matatizo mbalimbali katika jamii zikiwemo changamoto za ukame wanazozipata wafugaji.
Kupitia Shirikisho la Wanasayansi chipukizi Tanzania (YST) linaloandaa mashindano ya wanasayansi chipukizi yaliyofanyika hivi karibuni, Glory na Martha waliibuka washindi baada ya kutoa suluhu ya kiteknolojia ya kukabiliana na ukame kwa wafugaji wikiwemo wa ng’ombe na samaki.
Wazo la mabinti hao liliyapiga vikumbo mawazo 604 yaliyowasilishwa kwa ajili ya mashindano hayo na shule mbalimbali nchini na kuyashinda mawazo 123 ambayo yalipenya chujio la kuingia mashindanoni.
Mradi walioibuka nao Glory na Martha unaweza kuwa suluhisho baina ya wakulima na wafugaji. Picha| Shirikisho la Wanasayansi chipukizi Tanzania (YST).
Wazo la Glory na Martha ni mradi unaotumia eneo dogo kwa ajili ya kutengenezea chakula cha kulisha wanyama wengi hasa wakati wa ukame na unalenga kutatua changamoto za migogoro baina ya wakulima na wafugaji katika jamii za kanda ya ziwa na maeneo mengine ya Tanzania.
“Wazo la mradi wetu lilianza baada ya kuona uhaba wa chakula cha mifugo wakati wa vipindi vikali vya hali ya hewa ikihusisha uhaba wa chakula cha kijani kwa ajili ya mifugo na migogoro baina ya jamii za wakulima na wafugaji kwa sababu ya ardhi ndogo ya malisho kwenye baadhi ya sehemu nchini Tanzania zikiwemo Morogoro, Shinyanga na Dodoma,” Glory na Martha wakielezea mradi wao kwa pamoja.
Kwa mujibu wa taarifa ya uchambuzi wa mradi huo wa mabinti hao ujulikanao kwa Kiingereza kama “Hydroponic Fodder for Animal Feeding and Health” endapo utatumika una uwezo wa kuzalisha chakula cha mifugo ndani ya siku sita hadi saba na kumwacha mfugaji bila msongo wa mawazo wa kupata chakula katika kipindi chochote cha mwaka mzima.
“Vitu vinavyohitajika kutengeneza mradi huu ni pamoja na mabomba ya plastiki, miti ya mianzi, neti kwa ajili ya kivuli na magunia. Ujenzi wa mradi huu ulifanyika kwenye mazingira yenye nyuzijoto 20 hadi 32 na unyevu (humidity) wa asilimia 78 hadi asilimia 89 na mwanga unaodhibitiwa,” mabinti hao wanaeleza katika taarifa za kina za mradi huo.
Utafiti wa awali ulifanywa kwenye maeneo ya shule yao baada ya shughuli za ufugaji wa samaki zinazofanyika shuleni hapo kukumbwa na changamoto ya upatikanaji wa chakula.
Mradi huo ulilenga samaki 400 waliogawiwa kwa usawa (200 kwa 200) huku 200 wa kwanza wakipewa chakula cha kawaida na 200 wengine wakipewa chakula cha mradi wa wanafunzi hao.
Matokeo ya utafiti huo yalibaini kuwa samaki waliolishwa chakula kilichozalishwa kwenye mradi wa mabinti hao waliongezeka uzito na kukua kwa haraka kuliko waliopewa chakula cha kawaida kinachotumika na wafugaji wengi.
“Mradi wa Hydroponic Fodder unachagiza ukuaji wa haraka wa mifugo na ongezeko la uzito wa samaki na mifugo wengine na hivyo kuhakikisha soko na ukuaji wa uchumi kwa mfugaji,” inasomekana sehemu ya taarifa ya YST.
Ushindi wa wasichana hao hautaishia kupata kikombe tu bali wamejinyakulia kitita cha Sh1.35 milioni iliyotolewa na YST huku udhamini wa masomo yao kwa ngazi ya shahada hapa nchini ukitolewa na Taasisi ya Karimjee Jivanjee Foundation (KJF).
Zinazohusiana
- Wasichana vichwa masomo ya Sayansi kidato cha sita 2019
- Ajira zaidi ya milioni 2 zinawasubiri wasichana wanaosoma masomo ya sayansi
- Uhaba wa wanawake sekta ya teknolojia wakwamisha utekelezaji wa ajenda za maendeleo
Mwenyekiti wa Taasisi ya KJF Yusuph Karimjee anasema jukwaa hilo, lililoanzishwa tangu mwaka 2011, limefanikiwa kufikia mikoa yote nchini na kuanzisha misingi imara ya kisayansi.
Karimjee anasema licha ya kukumbwa na changamoto nyingi zilizosababishwa na ugonjwa wa corona, mikakati mingi iliwekwa kuhakikisha vipaji hivyo vya wanasayansi vinazidi kuibuliwa.
Karimjee anaeleza kuwa shughuli za michujo na ushauri zimefanyika kwa njia ya mtandao ikiwa ni kwa kutumia mitandao ya kijamii, programu tumishi pamoja na teknolojia za kidijiatali.
Ushindi wa wasichana hao kutoka shule hiyo ya serikali iliyopo mkoani Mwanza, uliwaacha nyuma wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kisimiri iliyopo Arusha.
Kwa sasa mabinti hao wanaendelea na masomo ili kuhakikisha wanahitimu elimu hiyo.
Uongozi wa shule wanayosoma mabinti umeeleza kuwa ungependa kuona michuano ya kimataifa ya wanasayansi wanafunzi.
Mkuu wa Shule ya Nganza Mageni Nisambo ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa alifurahishwa na ufundi ulioonyeshwa na mabinti zake na kwamba ni funzo kwa jamii kuwa ni vibaya kukata tamaa.
“Ushindi wa hawa vijana wawili unawaongezea morali wengine. Kwa sababu uwezo wa kimasomo unatofautiana sasa ni rahisi kwa wanaoona masomo ya sayansi kuwa magumu kupewa hamasa na hawa kwa kuona yanawezekana,” amesema mkuu huyo wa shule akibainisha kuwa ushindi wao Glory na Martha si wa shule peke yake bali na jamii yote ya Tanzania.