Virusi vya Corona vyatibua mechi ya Manchester City na Arsenal

September 3, 2020 12:22 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link

Mmiliki wa timu ya Olympiacos, Evangelos Marinakis amekutwa na maambukizi ya virusi vya Corona jana Machi10. Picha| Vaaju.com.


  • Ni baada ya baada ya wachezaji wa Arsenal kukutana na Evangelos Marinakis ambaye jana ameainisha kukutwa na maambukizi ya ugonjwa huo.
  • Baadhi ya wachezaji wa Arsenal wamelazimika kujitenga majumbani kwao kwa siku 14.
  • Tiketi za mashabiki waliopanga kuhudhuria kutumika pale mechi nyingine itakapopangwa.

Dar es Salaam. Mechi kati ya timu ya Manchester City na Arsenal ambayo ilitarajiwa kuchezwa leo Machi 11, 2020 katika uwanja wa Etihad nchini Uingereza imeahirishwa ikiwa ni hatua ya kujikinga na maambukizi dhidi ya virusi vya Corona ambavyo vinasambaa kwa kasi ulimwenguni. 

Hadi sasa nchini Uingereza ambako mechi hiyo ingechezwa kuna visa vya watu 382 kuambukizwa akiwemo Waziri wa afya na mbunge wa chama cha Conservative nchini Uingereza Nadine Dorries.

Mtanange huo ambao ulikuwa ukisubiriwa kwa hamu na wadau wa ligi kuu ya Uingereza umeahirishwa baada ya baadhi ya wachezaji wa timu ya Arsenal kuhofiwa kuwa na ugonjwa huo unaoogopeka duniani.

Hofu hiyo imezuka baada ya wachezaji kadhaa wa timu ya Arsenal kukutana na mmiliki wa timu ya Olympiacos, Evangelos Marinakis siku 13 zilizopita ambaye Jumanne ya Machi 10 alibainika kukutwa na maambukizi ya virusi hivyo.

Uongozi wa timu hiyo umesema ripoti ya kiafya iliyopokelewa imeainisha uwezekano wa wachezaji wa timu hiyo kuathirika na virusi hivyo ni mdogo lakini haina budi kufuata maelekezo yaliyotolewa na Serikali.

“Tunafuata maelekezo ya Serikali ambayo yanashauri kila mtu aliyekutana na mtu mwenye maambukizi anatakiwa kujitenga nyumbani kwake walau kwa siku moja tangu akutane na mtu huyo,” imeeleza taarifa ya uongozi wa timu hiyo.

Hiyo ina maana kuwa baadhi ya wachezaji wa Arsenal pamoja na stafu wa timu hiyo hawatoweza kufika uwanjani leo kwa kuwa wanatakiwa kubaki majumbani kwao hadi siku 14 zitakapoisha.

Uongozi wa ligi ya kuu nchini humo umesema mechi hiyo itapangiwa siku nyingine.


Zinazohusiana


Aidha, Arsenal imeonyesha kusikitishwa na kuahirishwa kwa mechi hiyo lakini tiketi za mashabiki zitatumika pale mtanange mwingine utakapopangwa.

“Tunaelewa jinsi gani inakatisha tamaa kwa wanaotuunga mkono hasa waliosafiri kuja kwenye Jiiji la Manchester kwaajili ya mechi ya leo. Tiketi zao zitatumika mechi nyingine ikipangwa” imesomeka taarifa iliyotolewa na Arsenal.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya (WHO), watu 113,702 wamekutwa na maambukizi ya virusi hivyo huku watu 4,012 wakipoteza maisha.

Ofisi ya mambo ya nje ya Uingereza imewataka raia kufanya safari zilizo muhimu pekee kwenda Italia, ambayo ina maambukizi makubwa zaidi baada ya China.

Enable Notifications OK No thanks