Daraja la Kigongo Busisi litakavyoinua uchumi kanda ya ziwa
- Linajengwa Ziwa Victoria ili kuunganisha mikoa ya Mwanza na Geita.
- Litakuwa na urefu wa kilomita 3 ili kuwapunguzia wananchi adha ya usafiri wa vivuko.
- Litachochea usafirishaji wa mizigo mikoa ya Kanda ya Ziwa na Afrika Mashariki.
Mwanza. Ujenzi wa daraja la Kigongo Busisi linalojengwa katika ziwa Victoria umefikia asilimia 5.78 huku likitarajiwa kupunguza adha ya usafiri wa majini kwa wakazi wa mikoa ya Geita, Mwanza na nchi jirani za Afrika Mashariki.
Daraja hilo lenye urefu wa kilometa 3.2 na upana wa mita 28.45 litakapokamilika litakaunganisha mawasiliano ya barabara kati ya mikoa ya Mwanza na Geita kwa kukatisha Ziwa Victoria.
Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (CRB), Mhandisi Patrick Balozi amesema ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa daraja hilo linalojengwa kwa gharama ya zaidi ya Sh60 bilioni.
Licha ya kuridhishwa na teknolojia inayotumiwa na wakandarasi wa kampuni ya ujenzi ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) wanaojenga daraja hilo, Mhandisi huyo amesema kukamilika kwa daraja hilo si tu kutafungua fursa za kiuchumi bali pia kutawajengea uwezo wahandisi na wakandarasi wa ndani.
“Ujenzi wa mradi huu utasaidia kufanya maendeleo makubwa kwa mikoa ya Geita, Kagera katika kuvusha bidhaa na abiria na kwamba itapunguza muda kutoka dakika 15 za kwenye vivuko na kufikia dakika nne,”amesema Mhandisi Balozi jana (Oktoba 8, 2020) alipokagua ujenzi wa daraja hilo.
Balozi ambaye aliambatana na kundi la wanazuoni wa uhandisi waliofika kujifunza katika eneo hilo, amesema pia litaongeza idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi za Taifa za Kanda ya Ziwa ikiwemo ya Lubondo.
Desemba 7, 2019 Rais John Magufuli aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja hilo katika eneo la Kigongo, Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza na linatarajiwa kukamilika mwaka 2023.
Hatua za ujenzi wa daraja hilo
Msimamizi wa ujenzi wa daraja hilo, Mhandisi Willium Sanga kutoka ofisi ya Wakala wa Barabara mkoa wa Mwanza (Tanroads) amesema mpaka sasa wamejenga daraja la muda na tayari wamefikia mita 600.
Daraja hilo limejengwa upande wa Kigongo na Busisi na kwamba maendeleo ya mradi huo yamefikia asilimia 5.78.
Amesema muda wa ujenzi wa daraja hilo ni miezi 48 ambapo umeanza Februari 25 mwaka huu na litakuwa na urefu wa kilomita 3 upana wa mita 28.45 likijumulisha barabara nne za mita saba.
Ndani ya hilo daraja kutakuwa na mita 5 kwa ajili ya waenda kwa miguu sambamba na sehemu za kuegeshea magari kwa kila upande wa daraja.
“Pamoja na mafanikio haya lakini kulikuwa na changamoto ya kuwepo kwa ugonjwa wa Corona ambayo ulisababisha baadhi ya wakandarasi kutoruhusiwa kutoka kwenye nchi zao ingawa kwa sasa wanaendelea vizuri kwa kuwa mkandarasi anafanya kazi mchana na usiku,” amesema Mhandishi Sanga.
Soma zaidi:
- Njia za kuepuka foleni kali ya Dar es Salaam kwa kutumia teknolojia
- Majaliwa aagiza ubora wa barabara kuu Tanzania uangaliwe upya
Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Juma Sweda amesema ujenzi wa mradi huo umeleta manufaa makubwa kwani zaidi ya watu 200 kutoka wilayani humo wamepata fursa ya kuajiriwa katika mradi huo.
Mkuu huyo wa wilaya amesema kukamilika kwa mradi huo kutapunguza changamoto ya ucheleweshwaji uliokuwa unasababishwa na vivuko lakini pia kwa baadhi ya watu wasiokuwa na nauli kutembea kwa miguu umbali wa kilomita 3 kwenda na kurudi.