Prof Mkenda: Tanzania haiwezi kuwa mateka wa sukari

Waziri wa Kilimo Prof Adolf Mkenda akihutubia mamia ya wakulima wa miwa wa Wilaya ya Kilombero jana alipotembelea kukagua mwenendo wa kiwanda cha sukari cha Kilombero kufuatia malalamiko ya wakulima miwa yao zaidi ya tani 300,000 kukosa soko na kuharibika wakati nchi ikiwa na upungufu wa sukari. Picha| Wizara ya Kilimo.
- Asikitishwa miwa ya wakulima kutonunuliwa na kiwanda cha sukari cha Kilombero.
- Amevitaka viwanda vya ndani vya sukari viongeze uwekezaji ili kutumia vizuri miwa ya wakulima wadogo.
- Asema hiyo itasaidia kupunguza uagizaji wa sukari nje ya nchi.
Dar es Salaam. Serikali imeutaka uongozi wa kiwanda cha sukari cha Kilombero kilichopo mkoani Morogoro kuhakikisha unaharakisha mchakato wa uwekezaji ili kuongeza uwezo wake wa kuchakata miwa yote inayozalishwa na wakulima ili Tanzania ijitosheleze kwa sukari.
Hatua hiyo inafuatia wakulima wa miwa wa Wilaya ya Kilombero kulalamikia kitendo cha mwekezaji wa kiwanda hicho kushindwa kununua miwa yote takribani tani 800,000 inayozalishwa na wakulima ili kuchakata sukari .
Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda amesema takwimu za uzalishaji miwa zinaonyesha wastani wa tani 350,000 hazijanunuliwa na mwekezaji wa kiwanda hicho ambapo zingetosha kuzalisha sukari tani 35,000.
Amesema hiyo ina maana kuwa nchi ingeagiza nje sukari tani 5,000 pekee kati ya 40,000 za upungufu wa sasa.
“Hatuwezi kuwa mateka katika suala la uzalishaji sukari kwa kumtegemea mzalishaji mmoja.
“Tatizo wakulima wana miwa hainunuliwi na mwekezaji halafu nchi inaendelea kutoa vibali kwa mwekezaji kuagiza sukari nje ya nchi wakati anatakiwa kuongeza uwezo wa viwanda vyake kuchakata miwa ya wakulima,” amesema Waziri huyo alipokutana na wakulima wa miwa wa Kilombero Februari 15, 2020.
Zinazohusiana:
Kufuatia hali hiyo Prof Mkenda ameagiza uongozi wa kiwanda cha sukari Kilombero kuharikisha mchakato wake wa kuongeza uwezo wa kiwanda kuchakata miwa kutoka tani 629,000 mwaka 2018/19 hadi kufikia tani 800,000 msimu huu ili miwa yote ya wakulima wadogo inayozalishwa sasa na kukosa soko itumike kuzalisha sukari.
Miwa imekuwa imekuwa malighafi muhimu kwa ajili ya utengenezaji wa sukari inayotumiwa majumbani na katika shughuli mbalimbali za uzalishaji viwandani nchini Tanzania.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kiwanda cha Sukari cha Kilombero Balozi Mstaafu Ami Mpungwe amesema kiwanda hicho kinategemea miwa ya wakulima wadogo kwa asilimia 50 kuzalisha sukari.
“Kama kuna mtu ana fikra kuwa wakulima wadogo tunawadharau siyo kweli, tunawategemea sana ili viwanda vyetu viendelee na sasa tunalenga kufikia kununua miwa ya wakulima asilimia 60 baada ya upanuzi wa kiwanda mwaka 2023,” amesisitiza Balozi Mpungwe.
Amesema tayari wameanza kushawishi wabia wake kujenga kiwanda kipya kikubwa kitakachowezesha kuongeza uchakati wa miwa yote ya wakulima ambapo jumla ya Sh584 bilioni zinahitajika kujenga kiwanda hicho kiitakachokuwa na uwezo wa kuchakata tani 420 za miwa kwa saa tofauti na sasa ambapo uchakataji ni tani 220 kwa saa.

Latest