Magufuli, Watanzania wamlilia Maalim Seif
- Rais John Magufuli ametangaza siku tatu za maombolezo ya kifo chake.
- Viongozi mbalimbali wamlilia kiongozi huyo mashuhuri Tanzania.
- Wataka Watanzania kumuenzi kwa kuendeleza mazuri yake.
Dar es Salaam. Kufuatia kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, Rais John Magufuli ametangaza siku tatu za maombolezo huku viongozi mbalimbali wakimlilia kiongozi huyo mashuhuri Tanzania.
Maalim Seif aliyezaliwa mwaka 1949 amefariki leo Februari 17, 2021 saa 5:00 asubuhi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaan alikokuwa akipatiwa matibabu.
Mpaka mauti inamkuta kiongozi huyo alikuwa pia Mwenyekiti wa Chama Cha ACT-Wazalendo.
Rais Magufuli ametangaza siku tatu za maombolezo kuanzia leo Februari 17, 2021 ambapo ameagiza bendera zipepee nusu mlingoti ili kuomboleza kifo cha makamu huyo wa kwanza wa rais.
Kiongozi mkuu huyo wa nchi amewataka wafiwa wote kuwa na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki cha majonzi huku akimuombea marehemu apumzike kwa amani.
“Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar. Natoa pole kwa Rais wa Zanzibar Mhe. Dkt. Mwinyi, Familia, Wazanzibari, wanachama wa ACT-Wazalendo na Watanzania wote,” amesema Rais katika taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu.
Wakati Rais Magufuli akitangaza siku tatu za maombolezo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi naye ametangaza siku saba za maombolezo ya kitaifa ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti katika visiwa hivyo.
“Taarifa zaidi za msiba huu na maziko yake zitaendelea kutolewa na Serikali kwa ushirikiano wa karibu na familia pamoja na Chama Cha ACT-Wazalendo,” amesema Rais Mwinyi mara baada ya kutangaza kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.#NuktaHabari
pic.twitter.com/gpRinLAOu2— Nukta Tanzania (@NuktaTanzania) February 17, 2021
Muda mfupi baada ya kutangazwa kwa kifo cha Maalim Seif ambaye aliwahi kuwa mwanachama wa Chama Cha Wananchi (CUF) na Chama Cha Mapinduzi (CCM), viongozi mbalimbali na Watanzania wametoa salamu zao za pole kwa wafiwa na kueleza watakavyomuenzi marehemu.
Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema Maalim Seif aliwalea katika misingi ya uongozi na amewataka wanawachama wa chama hicho na Watanzania wandeleze maono yake ya kuimarisha demokrasia Tanzania.
“Maalim Seif Sharif Hamad alitulea kiuongozi kwa namna ambayo tutaweza kuendeleza maono yako, fikra zake na nia yake ya kuiona Tanzania yenye demokrasia na Zanzibar ambayo Wanzibar wanaishi kwa maridhiano,” amesema Zitto wakati akitoa taarifa ya ACT-Wazalendo kuhusu msiba huo.
Zitto ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Kigoma Mjini amesema taratibu za mazishi zitangazwa baada mashauriano ya karibu na Serikali huku akiwataka wanachama kuwa wavumilivu na wenye subira.
“Bado ni ngumu kuamini Maalim Seif Sharif Hamad hayupo nasi, tumepoteza mhimili wa siasa nchini na kiongozi nguli kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Naungana na Watanzania wote kutoa pole kwa familia na kuomboleza msiba huu mkubwa,” ameandika Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bashungwa Innocent katika ukurasa wake wa Twitter.
Soma zaidi:
Kifo hicho pia kimemgusa Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe ambaye katika ukurasa wake wa twitter ameandika, “nikiwa hapa Dubai, UAE, nimeshtushwa na taarifa za kutwaliwa kwa Mhe. Shariff Hamad; Jabali la Mageuzi Tz; Mkt wa Chama cha ACT & Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar. Natoa pole nyingi kwa familia, Chama chake, Wazanzibari & Watanzania wote.”
Naye Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema amepokea kwa huzuni na masikitiko taarifa ya kifo hicho
“Natoa pole kwa familia na Watanzania wote. Namuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu Mahali pema Peponi, Amin,” ameandika Mama Samia.
Taratibu wa mazishi za kiongozi huyo kwa mujibu wa Rais Mwinyi zitatangazwa mara baada ya kufanya mashauriano na familia, chama cha ACT-Wazalengo na Serikali.