Buriani Maalim Seif: Mwendo umeumaliza
- Mwili wa aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif umepumzishwa kijijini Mtambwe kwake Pemba.
- Mazishi hayo yamehudhuriwa na maelfu ya wananchi kisiwani Pemba wakiongozwa na viongozi mbalim mbali wa kisiasa.
- Kila mwili wake ilipopita huzuni na vilio vilisikika kutoka kwa waombolezaji.
Dar es Salaam. Hatimaye, Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amepumzishwa katika nyumba yake ya milele katika kijiji cha Mtambwe kisiwani Pemba huku viongozi wakitaka wananchi kuendelea kumuenzi kwa utumishi wake uliotukuka.
Maalim Seif aliyezaliwa mwaka 1949 amefariki dunia jana Februari 17 saa 5:00 asubuhi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaan alikokuwa akipatiwa matibabu.
Mwili wa Hayati Maalim Seif umepokelewa kwa huzuni, simanzi na vilio na wananchi na viongozi wa ngazi mbalimbali kila mahali ulipopita kabla ya kufikishwa kijijini Mtambwe, kudhihirisha kiongozi huyo alikuwa kipenzi cha wengi.
Kiongozi huyo amefanyiwa sala tatu jijini Dar es Salaam, Unguja na Pemba kabla mwili wake haujateremshwa katika kaburi aliloandaliwa kijijini kwake.
Sura zilizojaa huzuni, watu walioshindwa kujizuia kuonyesha hisia huku wakiangua vilio kila mahali msafara uliobeba mwili wa kiongozi huyo ulipopita kabla ya kuwasili kijijini Mtambwe.
Baada ya kufikika kijiji, zilisikika sauti za kila aina kwa wananchi wa kijiji hicho ambao wengi wao walivalia kanzu na kofia wakimuomba Mungu amsitiri kipenzi cha mioyo yao.
Soma zaidi:
Mazishi hayo yameongozwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi na viongozi wengine wa Serikali akiwemo Makamu wa pili wa Rais Hemed Abdallah.
Wengine ni marais wastaafu wa Zanzibar Dk Abeid Aman Karume na Dk Mohamed Ali Shein, wanachama wa Chama cha ACT-Wazalendo wakiongozwa na Ismail Jussa na wengine wengi kutoka vyama vingine vya kisiasa.
Baada ya shughuli mbalimbali ikiwemo sala kwa marehemu, mwili wa Maalim Seif iliteremshwa taratibu katika kaburi lake, ikiashiria ndiyo mwisho wa Wazanzibar kumuona kwa macho.
Wataka akumbukwe kwa uongozi thabiti
Licha ya simanzi na huzuni iliyotawala mazishi hayo, wananchi wametakiwa kumuenzi kivitendo Maalim Seif ili aendelee kuishi katika mioyo yao daima.
Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe akitoa salamu za chama, amesema maneno hayatoshi kumuelezea Maalim Seif. ushujaa wake kisiasa na maisha ya mfano aliyoyaishi yanafaa kueleza Watanzania juu ya mapigano yake aliyopigana wakati akiwa duniani.
“Mimi si mtu wa kukosa maneno lakini leo nakosa maneno ya kumuelezea mwenyekiti wangu Maalim Seif Sharif Hamadi. Nakosa maneno kwa sababu Maalim ni zaidi ya maisha,” amesema Zitto.
Kiongozi huyo wa ACT Wazalendo amewasihi Watanzania kutokuwa na simanzi na badala yake kufurahia maisha ya Maalim Seif kwa sababu ameyaishi maisha yake kikamilifu.
“Tumempoteza mshauri na mpatanishi kwenye vikao vya chama chetu na mtu aliyetupa ujasiri mkubwa wa kusonga mbele hata pale tulipokaribia kukata tamaa kutokana na magumu na madhira ya kisiasa,” amesema Zitto ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Kigoma Mjini.
Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Abdallah amewasihi Wazanzibar kuyaishi kivitendo maneno ya hayati Maalim Seif ili kumfanya apumzike kwa amani.
Hivyo ndivyo, Maalim Seif alivyohitimisha safari yake ya kuishi duniani kwa miaka 78.
Latest