Monster Hunter: Filamu ya kuisindikiza wikiendi yako
- Inamhusu kamanda aliyepoteza kikosi chake chote baada ya kuuliwa na wanyama asiowajua.
- Ni baada ya kupotea wakati wakitafuta wenzao waliopotea katika mazingira ya kutatanisha.
Dar es Salaam. Siku zote kuna sauti ya ndani ambayo hukuonya kutokufanya kitu fulani. Sauti hiyo wengine huichukulia kama nafsi mbili zinazobishana kukushauri ikiwepo moja inayokuambia fanya na nyingine inayokuambia usifanye.
Wewe huwa unasikiliza nafsi ipi? Kama nafsi inayokushauri kufanya kitu ambacho hauna uhakika nacho huchukua nafasi mara nyingi, basi hauna tofauti na kamanda Natalie Artemis ambaye anaongoza kikosi cha watu kama sita hivi kutafuta wanajeshi wengine waliopotea katika mazingira ya kutatanisha.
Kisa hicho kinapatikana katia filamu ya Monster Hunter, basi endelea kufaidi uondo wake hapa chini.
Wakiwa njiani kufanya upelelezi wao, wanaona vitu kama minara midogo ambayo ipo pembezoni mwa barabara na mbele yao ni alama za matairi ya gari ambayo hayana muendelezo.
Wakiwa wanashangaa shangaa, dhuruba kubwa inawaelekea na wanapotaka kuikimbia, wanakua wameshachelewa.
Kelele za kuomba msaada zilizochanganyika na mshangao zinaendelea kusikika wakati wakiwa hawafahamu kinachoendelea.
Loh! Kufumba na kufumbua macho, wapo sehemu tofauti na walipokuwa. Ni jangwani na wanachokiona siyo walichozoea. Mifupa mikubwa ya wanyama, mazingira ya kutisha kwa kutazama na wanyama wakubwa kuwahi kutokea. Ni kama wamesafirishwa kutoka duniani kwenda sehemu nyingine.
Wapo ugenini, hawafahamu mtu yeyote na mazingira pia hawayafahamu. Kabla hata hawajazoea mazingira, wanakaribishwa na mwenyeji ambaye siyo mkarimu.
Soma zaidi:
- Unavyoweza kuepuka magonjwa ya ngozi
- The Archenemy: Filamu inayokupa sababu za kutokumdaharau mtu usiyemjua
- Jinsi ya kununua chaja bora ya simu yako
Ni mnyama Diablo mwenye umbo kubwa na ambaye ujio wa timu ya Artemis haumfurahishi.
Kwa mandhari ya dunia, Diablo unaweza kumpa wasifu wa tembo mwenye sifa za simba sema tu tembo bado ni kama paka kwa umbo halisi la Diablo.
Wakijiandaa kukabiliana na mwenyeji wao, wanaishia kupoteza rafiki zao kwani Diablo siyo wa kuuawa kwa risasi.
Hata hivyo, waliosalia, wanafanikiwa kupata pango ambalo wanajificha humo kusubiri usiku upite lakini ni kama wamejichimbia kaburi lao kwani wote wanauliwa na viumbe wanaofanana na buibui wakubwa na kati ya timu ya watu takriban sita, anabaki Artemis pekee.
Kama kuokota dodo chini ya muembe, Artemis anakutana na Mwindaji ambaye kuua wanyama hao ni kama kunywa kikombe cha chai ya baridi.
Licha ya kuwa Artemis anaonyesha kutokukubaliana na mwindaji huyo, anakua hana namna zaidi ya kushirikiana naye kwani anahitaji kurudi dniani.
Huo ni mwanzo tu wawili hao wanatakiwa kushirikiana kummaliza Diablo huku kifo chake kikimtambulisha Rathalos ambaye ni mara mbili ya Diablo.
Baada ya muda, anagunda kuwa chanzo cha yeye na timu yake kujikuta walipo ni nguvu inayotokana na mnara wa ajabu ambao kuuharibu ni lazima wakutane na walinzi wa mnara huo a Diablo pamoja na Ratalos ni sehemu ya walinzi hao.
Wataweza au ni kama wanazidi kupalilia moto wao hasa ikizingatiwa kuwa mwindaji naye tayari amejeruhiwa vibaya kiasi cha kumlazimu Artemis kumbeba takribani nusu ya safari?
Fuatilia mwanzo na mwisho wa kisa hiki kuona jinsi gani Milla Jovovich, Tony Jaa na Tip “T.I.” Harris wanavyokusogeza na mandhari ya kufikirika kuziteka hisia zako.
Unaweza kuitazama filamu hii kupitia skrini za Century Cinemax zilizopo katima maduka makubwa (malls) zikiwemo mlimani City na Dar Free Market (DFM).