Mambo ya kuzingatia kabla ya kufungua kesi ya madai ya ‘kuchafuliwa’
- Hakikisha mtu aliyekuchafua amekutaja jina lako katika uchafuzi wake.
- Pia onyesha hasara uliyopata baada ya kuchafuliwa.
“Nitakwenda mahakamani, huwezi kunichafua namna hii nimepoteza heshima yangu na nimepata hasara sana, nitaongea na mawakili wangu tutakutana mahakamani lazima nikufundishe adabu”
Hii ni kauli ambayo imezoeleka kusikika kwa baadhi ya watu ambao wanataka kulinda heshima yao kwenye jamii. Unadhani mtu anachafuliwa kwa namna gani?
Hoja au madai ya kuchafuliwa siyo suala geni kwenye maisha yetu ya kila siku. Watu wamekuwa wakichafuana kwa maneno au maandishi.
Suala hili limepewa uzito kiasi kwamba sheria inatambua uwepo wake kupitia sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 (Media Service Act).
Kipengele cha 5 cha Sheria ya hiyo kinafafanua kwa undani kabisa kabisa kuhusu kuchafuana.
Kuchafua ni nini? Kifungu cha 35 cha sheria tajwa hapo juu kinasema kuwa “Defamation” ni ile hali ambayo maneno au maandishi ambayo yamechapishwa moja kwa moja yanaharibu heshima au hadhi ya mtu kwenye taaluma au biashara yake na kusababisha mtu huyo ambaye amechafuliwa kupata hasara kutokana na kitendo icho.
Nchini Tanzania pia kumekua na kesi nyingi za madai ya fidia baada ya mtu kuchafuliwa, lakini kesi nyingi sana zimekua zikigonga mwamba mbele ya mikono ya sheria na kumuacha mdai akiondoka mikono mitupu na mdaiwa akiondoka na ushindi.
Kabla ya kufungua kesi ya madai kuhusu kuchafuliwa hakikisha madai yako yana mashiko. Picha| Mtandao.
Vitu gani vinaashiria kuwa mtu amechafuliwa?
MANENO YANAYOCHAFUA HADHI YA MTU ( DEFAMATORY WORDS)
Huu ndio mzizi mkuu wa madai ya kuchafuliwa, kauli ambayo imetolewa lazima iwe ina uchafuzi na imelenga kumchafua mtu huyo husika. Kwa lugha nyepesi ni kuwa kauli hiyo haipendezi na hatarishi kwa hadhi ya mtu husika.
Ni kauli ambayo inaweza kuwa ya kuumiza, kukera, kejeli au dharau na ambayo imejaa uongo ndani yake. Mkusanyiko wake una lengo la kuharibu au kushusha hadhi ya mtu ambaye imeelekezwa kwake.
Ni vyema kutambua kuwa kauli hiyo ni ya uongo na haina ukweli wowote, kutoa maoni hakuwezi kuwa kauli ya kuchafua mtu kwa sababu ni maoni ambayo yanaweza kuwa kweli au uongo.
Mdai anatakiwa kuthibitisha kuwa mdaiwa alitoa maneno ya uongo ambayo yanaharibu moja kwa moja hadhi yake mbele ya jamii. Kuchafuliwa siyo tu kunaharibu hadhi ya mtu binafsi inaweza pia kuharibu mpaka bidhaa au biashara ya mtu huyo.
Kwahiyo kabla haujafungua shauri la madai ya kuchafuliwa unapaswa kujiridhidha kuwa kauli ambayo imetolewa ni ya uongo na inalenga kukuchafua.
Soma zaidi:
- Polisi Tanzania yakiri kumshikilia Mwanahabari Kabendera
- Uhamiaji waeleza sababu za kuendelea kumshikilia Mwanahabari Kabendera
- Mwanahabari Erick Kabendera ashitakiwa kwa utakatishaji fedha, uhujumu uchumi
KUMLENGA AU KUMGUSA MDAI
Unaweza kushitaki bila kutajwa? Jibu ni rahisi sana hii haiwezekani. Kauli hiyo lazima imtaje moja kwa moja au imguse mdai pasi na shaka.
Kwa lugha adhimu kuwa lazima atajwe yeye kwenye kauli hiyo na siyo mtu mwingine. Lazima mdai awe ametajwa bila kificho, kushindwa kutajwa kwake kutaharibu msingi mzima wa madai ya kuchafuliwa mbele ya sheria.
Hii ina maana kuwa mdai lazima yeye ndiye awe ametajwa kwenye kauli za kuchafuliwa. Kwa mfano Gazeti moja liandike ‘ Imebainika kuwa Hamza Lule sio Mwansheria ni tapeli tu” hapa Hamza Lule ametajwa moja kwa moja kwenye kauli hii , hivyo basi inampa haki ya moja kwa moja kufika mahakamani na kufungua madai ya kuchafuliwa sababu ametajwa.
Ikiwa mdai hajatajwa moja kwa moja kwenye kauli hiyo basi hawezi kusimama mbele ya mahakama tukufu na kudai fidia ya kuchafuliwa.
KUCHAPISHWA ( PUBLICATION)
Kauli lazima iwe imechapishwa, ikiwa na maana kuwa kauli hiyo imefika kwa mtu au watu au kwa jamii inayowazunguka. Kuchapishwa hapa siyo lazima iwe gazetini au kwenye chombo cha habari.
Kile kitendo cha habari hiyo kuweza kuwafikia watu wengine na kuelewa kuwa mtu fulani ndiye kachafuliwa kwa njia yoyote ya habari, basi inatosha kukamilika kwa uchapishwaji wa habari husika mbele ya macho ya sheria.
Hapa inamaanisha kuwa taarifa husika imefika kwa watu wengine na wameweza kuelewa ujumbe uliobebwa na taarifa yenyewe pasi na kutumia nguvu katika kuelewa taarifa husika.
Uchapishaji ukiwa umetokea basi unatosha kumpa nguvu mdai kuweza kuwasilisha na kukazia kwenye madai yake ya fidia ya kuchafuliwa pasi na shaka yoyote, kushindwa kuthibitisha uchapishwaji wa taarifa husika unadhoofisha kesi nzima.
Usipojipanga vizuri katika kesi ya kuchafuliwa utajikuta katika wakati mgumu kwa sababu mahakama inapokea ushahidi wa uhakika. Picha| Mtandao.
KUPATA HASARA
Je ni lazima niwe nimepata hasara? Jibu ni ndiyo ili uweze kudai fidia ya kuchafuliwa lazima uwe umepata hasara kutokana na kauli ambayo imewasilishwa kwako na mdaiwa.
Hasara hiyo kwa kiasi kikubwa inategemea na hadhi yako ambayo unayo kwenye kazi , biashara au taaluma yako. Kuweza kuthibitisha hasara ambayo umeipata inakua ni njia nzuri kwa mahakama kuweza kutoa amri ya fidia ambayo unastahili kulipwa kutokana na kuchafuliwa kwako.
MWISHO
Ili kuepusha hasara ambazo hazina msingi ni vyema kuhakikisha unazingatia vipengele tajwa hapo juu kabla ya kukumbana na kadhia ya kesi yako kufutwa na kulipa gharama za kesi.
Imeandaliwa na Hamza Yusufu Lule,
Wakili wa Mahakama kuu na Mahakama za chini
Kwa msaada wa kisheria wasiliana nami kupitiaTwiter@Hamzaalbhanj
Namba ya simu 0717521700
Latest