Bahati ya mtende: JKT yawarejesha jeshini vijana wa kujitolea
- Ni waliochaguliwa kujiunga na jeshi hilo mwaka 2020/21.
- Walirejeshwa nyumbani mwezi Februari mwaka huu.
- Wanaotakiwa kurudi jeshini ni wale wenye elimu ya darasa la saba na elimu ya kidato cha nne.
Dar es Salaam. Unaweza kusema ni bahati ya mtende baada ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kuwataka baadhi ya vijana wa kujitolea waliochaguliwa kujiunga na jeshi hilo mwaka 2020/21 kuripoti tena jeshini baada ya kurejeshwa nyumbani mwezi Februari mwaka huu.
JKT ilisitisha kwa muda mafunzo ya kujitolea mwaka 2020/21 yaliyotarajiwa kuanza robo ya kwanza ya mwaka huu na vijana wote waliochaguliwa kuripoti kwenye kambi za JKT kwa ajili ya kuhudhuria mafunzo hayo waliamuliwa kurejea majumbani mpaka watakapotaarifiwa tena.
Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Charles Mbuge katika taarifa yake iliyotolewa leo Aprili 30, 2021 amewataka baadhi ya vijana hao kuripoti kwenye makambi ya jeshi hilo tena.
“Vijana wanaotakiwa kuripoti makambi ya JKT waliyokuwa wamepangiwa hapo awali ni wale wenye elimu ya darasa la saba na elimu ya kidato cha nne,” amesema Jenerali Mbuge katika taarifa yake.
Wanatakiwa kuripoti makambini kuanzia Mei 7 hadi 14, 2021.
Soma zaidi:
- Hakuna kulala wahitimu kidato cha sita mwaka 2020
- Kujiunga mafunzo ya JKT siyo ajira: Mwinyi
- Serikali yaeleza sababu JKT kusitisha mafunzo ya kujitolea 2020-21
Vijana wenye elimu ya kidato cha sita, ngazi ya cheti, stashahada, shahada na wale wenye taaluma ya uhandisi wataendelea kusubiri majumbani hadi hapo utaratibu mwingine utakapotangazwa.
Mafunzo yanayotolewa na JKT kila mwaka yamekuwa yakiwapatia vijana stadi za maisha, uzalendo na ujuzi wa uzalishaji mali kwa ajili ya kuchangia katika ujenzi wa Taifa.
Hivi karibuni, vijana wengine 854 ambao ni sehemu ya vijana 2,400 waliokuwa wameahidiwa ajira na Hayati Rais John Magufuli walifurushwa jeshini kutokana na kufanya maandamano ya kudai ajira ya kwenda Ikulu ili kumuona Rais Samia Suluhu.
Vijana hao walikuwa wameahidiwa mwaka jana na Hayati Rais Magufuli ya kuandikishwa jeshini baada ya kushiriki katika ujenzi wa Ikulu mpya ya Chamwino mkoani Dodoma.
Latest