Hiki ndiyo kituo cha habari za corona Facebook kinachokuepusha na “mafamba”
- ‘Coronavirus (Covid-19) information Center’ inapatikana kwa watumiaji wote wa mtandao huo wa Facebook duniani.
- Pia inatoa takwimu za ugonjwa wa corona kwa kila nchi.
Katika kuhakikisha watu wanapata taarifa sahihi zinazohusu ugonjwa wa corona mtandao wa Facebook umetengeneza akaunti maalumu inayotoa taarifa kuhusu ugonjwa huo sambamba na taarifa za chanjo ya ugonjwa huo unaozidi kuutesa ulimwengu.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linabainisha kuwa hadi Juni 14, 2021 kulikuwa na visa vya ugonjwa wa virusi vya corona (Covid-19) milioni 175.4 huku watu takriban milioni 3.8 wakiripotiwa kupoteza maisha tangu maradhi hayo yaibuke mwishoni mwaka 2019 nchini China.
Kupata taarifa hizo kwenye Facebook, utahitajika kuingia kwenye kituo maalum cha habari za ugonjwa wa virusi vya corona” kinachojulikana kwa kimombo kama ‘Coronavirus (Covid-19) information Center’ kinachopatikana kwa watumiaji wote wa mtandao huo wa Facebook duniani.
Mtumiaji anaweza kupata kituo hicho kwa kutafuta katika ukurusa wake wa Facebook kwa jina “Coronavirus (Covid-19) information Center” kisha anaweza kuona taarifa mbalimbali ikiwemo jinsi ya kujikinga na ugonjwa huo. Mbali na kukisaka, kuna baadhi ya nyakati kituo hicho cha mtandaoni huonekana iwapo ukurasa wako utakuwa umetawaliwa na habari za corona.
Akaunti maalumu ya Facebook ‘Coronavirus (Covid-19) information Center’ inayotoa taarifa kuhusu ugonjwa huo sambamba na taarifa za chanjo ya ugonjwa huo unaozidi kuutesa ulimwengu.Picha Facebook
Vilevile katika kituo hicho unaweza kuona habari za chanjo ya corona kutoka taasisi mbalimbali za kitaifa na kimataifa kama WHO na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Wizara ya Afya Tanzania zikiwa na maelezo ya chanjo na jinsi gani zinatengenezwa na kabla ya kutengenezwa hatua zipi zinachukuliwa kabla ya kupelekwa kwa wananchi.
Pia kituo hicho, ambacho ni kama ukurasa wa kawaida wa Facebook, kina maelezo kuhusu madhara ya chanjo ‘ side effects’ ili kuwaondoa watu hofu na kupunguza habari za uzushi wakati huu wa janga la Covid-19.
Kituo hicho cha ‘Coronavirus (Covid-19) Information Center’ pia unatoa takwimu za ugonjwa wa Corona kila siku kwa kila nchi zikiwemo data za wagonjwa wangapi wameathirika na ugonjwa huo, wangapi wamepona na vifo vingapi vimetokea.
Iwapo umetatizika na ukweli wa habari kuhusu Covid-19 ukiwa ndani ya Facebook, kituo hicho ni muhimu kupitia mara kwa mara kwa ajili ya kupata taarifa za msingi ili kupata taarifa sahihi za ugonjwa wa corona na kupunguza usambazaji wa habari za uzushi.