Ahueni: Mahakama inayotembea yaanza kupunguza gharama za kesi Tanzania
- Inapunguza gharama za usafiri kufata haki na kufungua kesi.
- Ni mkombozi kwa watu ambao hawana mahakama katika maeneo yao.
Mwanza. Watanzania wametakiwa kuchangamkia fursa ya kutumia mahakama inayotembea (Mobile Court) ya Tanzania kwa sababu inasaidia kuokoa fedha ambazo wanazitumia kufungua mashauri ya kesi na gharama za usafiri kutafuta haki zao.
Mahakama hiyo iliyoanzishwa mwaka juzi iko chini ya Mahakama ya Tanzania ambapo imekuwa ikizunguka katika maeneo mbalimbali nchini hasa yanayokabiliwa na upungufu wa majengo ya mahakama.
Mratibu wa mahakama inayotembea, Moses Ndelwa amesema mahakama hiyo inasaidia kuokoa fedha za wananchi ambazo wanazitumia kwa usafiri kwa ajili ya kufuata huduma za mahakama.
“Mtu mmoja anaweza kuokoa kiasi cha Sh300,000 kwa shauri moja na kuwa wananchi wanatakiwa kutumia zaidi mahakama hizo zinazotembea kwa kuwa zina huduma zote,” amesema Ndelwa wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 17, 2021 jijini Mwanza.
Amewataka wananchi wanapoona mahakama hiyo ikipita katika maeneo yao wafungue kesi zao na wale ambao kesi zao zinaendelea katika mahakama mbalimbali ili kupata haki kwa haraka.
Mathalani, mashauri 1,208 yaliyofunguliwa katika mahakama hiyo ndani ya siku 30 zilizopita yamesikilizwa na kutolewa uamuzi nchini ambapo kati ya hayo 520 yalitoka mkoa wa Mwanza.
Mkazi wa Mkoa wa Mwanza, Claudia Masese ni Mwananchi aliyefika leo kwenye mahakama hiyo kupata huduma amekiri kuwa inasaidia kupunguza gharama pamoja na muda wa kupanga foleni ikilinganishwa na mahakama za kawaida.
Kwa mujibu wa Ndelwa ambaye pia ni Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama Kanda ya Mwanza, tayari watu 13,668 wamenufaika na mahakama hiyo tangu ilipoanzishwa mwaka 2019.
Mahakama hiyo kwa sasa inafanya kazi maeneo ya mijini na kwamba imejipanga kwenda vijijini ili kuwasogezea wananchi huduma hiyo hasa katika maeneo ambayo hayana mahakama ikiwemo Butiama mkoani Mara, Gairo (Morogoro), Chamwino mkoani Dodoma.
Asilimia 38 ya kesi zinazofungulia katika mahakama hiyo ambayo ipo kwa ngazi ya mahakama ya mwanzo, wilaya na mkoa, kwa mujibu wa Ndelwa zinahusu madai ya talaka kwa wanandoa.
Latest
