Corona: Rais Museveni hajapelekwa Ujerumani kutibiwa

June 28, 2021 11:45 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Amezushiwa kuwa amepata Corona na amepelezwa Ujerumani kutibiwa.
  • Habari hizo hazina ukweli bali ni uzushi.
  • Serikali ya Uganda haijatoa taarifa yoyote kuhusu hali ya rais huyo.

Mwanza. Baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuzushiwa kuwa ameamuru uvaaji wa barakoa iwe suala la lazima na siyo hiari Tanzania, wapotoshaji wameenda mbali zaidi na kumzushia Rais wa Uganda, Yoweri Museveni kuwa ameambukizwa Corona na kukimbizwa nchini Ujerumani kupata matibabu.

Hata hivyo, hakuna taarifa rasmi iliyotolewa na Serikali ya Uganda kuhusu afya ya Rais Museveni na kama amepelekwa nje ya nchi kwa matibabu. Hivyo habari hizo zinazosambaa mtandaoni ni uzushi na hazina ukweli wowote.

Habari hiyo ya uongo dhidi ya Museveni aliyekaa madarakani zaidi ya miaka 30 imetengenezwa kupitia akaunti feki ya Twitter ya shirika la habari ya NTV Uganda na kusambazwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii ikiwemo WhatsApp.

Habari hiyo inaeleza kuwa Rais huyo amepata maradhi ya Corona na kukimbizwa nchini Ujerumani kupata matibabu huku ikisema daktari wake binafsi, Dk Monica Musenero amethibitisha. 

Nini ukweli wa Habari hiyo?

Habari hiyo haina ukweli kwa sababu imetumia akaunti feki ya NTV Uganda na tayari chombo hicho cha habari kimekanusha kuripoti taarifa hiyo huku kikiwataka wananchi kuipuuza kwa sababu siyo yao. 

 Kutokana na umuhimu na nafasi ya aliyonayo Rais Museveni, vyombo vya habari vya ndani na kimataifa vingekuwa vimeripoti habari hiyo, lakini habari hiyo haijaripotiwa na vyombo vya habari.

Aidha, Serikali ya Uganda na taasisi zake hazijatoa taarifa yoyote kuhusu Rais kuugua na anaendelea na shughuli zake za kikazi kinyume na uzushi unaosambazwa dhidi yake. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW