Namna wananchi wanavyowadhibiti viongozi ‘wapigaji’ Kanda ya Ziwa

July 14, 2021 9:35 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Kufuatilia kwa ukaribu mapato na matumizi ya fedha zao.
  • Kushiriki kikamilifu katika miradi ya kijamii na mikutano ya vijiji.
  • Viongozi waongeza uwajibikaji na uwazi kwa kuhofia “kupigwa chini”.

Geita. Licha ya kuchangia michango ya maendeleo katika kijiji chao, kwa wakazi wa Kijiji cha Shenda mkoani Geita, ilikuwa ni ngumu kufahamu mwenendo wa mapato na matumizi.  

Viongozi wa kijiji chao walikuwa hawawasomei mara kwa mara taarifa hizo muhimu katika kuongeza uwazi na uwajibikaji katika masuala ya maendeleo wakati wa mikutano.

Maisha hapa yalikuwa kawaida tu, viongozi wakitaka walikuwa wakisoma mapato na matumizi na wasipotaka maisha yaliendelea pamoja na kuwa walitakiwa kisheria kufanya hivyo kila baada ya miezi mitatu.

Kutokuwepo uwazi na uwajibikaji katika mapato ya serikali yao ya kijiji kulichochea mianya ya ubadhirifu, jambo lililowakatisha baadhi kushiriki katika shughuli za maendeleo.

“Zamani hela zilikuwa zikipigwa na hapakuwa na maendeleo kama haya,” anasema Saila Macheku (28), mkazi wa Kijiji cha Shenda wilayani Mbogwe akibainisha kuwa wananchi walikuwa nao hawafuatilii taarifa hizo.

“Kwa sasa upigaji hamna tunasimamia hadi shilingi ya mwisho ili tupate maendeleo,” anaongeza Saila huku akitabasamu na kueleza kuwa mafanikio hayo yamekuja baada ya kuwadhibiti viongozi wabadhirifu wa fedha za wananchi.

Furaha ya Saila inatimilika kwa sababu miradi inayoanzishwa kijijini hapo ikiwemo ujenzi wa zahanati na maji inakwenda vizuri bila kuwepo kwa changamoto za upotevu wa fedha walizochanga wananchi.

Saila na wakazi wengine wa kijiji hicho kilichopo kata ya Masumbe wilayani humo wanafurahia matunda ya uwepo wa uwazi na uwajibikaji wa rasilimali za umma ikiwemo mapato yanayokusanywa kwenye miradi ya kijiji na michango ya wananchi.Jengo la zahanati ya kijiji cha Shenda wilayani Mbogwe ambalo limejengwa kwa nguvu za wananchi baada ya kupata mwamko wa kuhoji mapato na matumizi ya fedha wanazochanga. Picha| Gift Mijoe.

Hata hivyo, haikuwa rahisi kwa wakazi hao kujenga jamii yenye uwazi na uwajibikaji hasa kwa viongozi wanaowaongoza. 

Uwezo huo wa kuhoji ni matokeo ya mafunzo ya uraghabishi yaliyowajengea uwezo wa kujiamini na kutambua haki zao kama raia.

Mafunzo hayo yaliyotolewa kwa nyakati tofauti kuanzia mwaka 2016 na mashirika ya Tamasha na Twaweza wilayani humo, pia yaliwawezesha wananchi hao kupata elimu ya kuwasimamia viongozi wao na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya vijiji ili kujiletea maendeleo.

Mkazi wa Kijiji cha Shenda Fedson Kimanki anayejishughulisha na kilimo anasema elimu hiyo imemfanya kila mkazi wa kijiji hicho kuwa mraghabishi kiasi cha kusaidia kuwafurusha viongozi “waolikuwa wanapenda kupiga pesa” na kuwaweka wawajibikaji. 

Miongoni mwa utaratibu unaotumika katika serikali za mitaa kuongeza uwazi wa rasilimali za umma ni viongozi kusoma mapato na matumizi kila baada ya miezi mitatu na kuwashirikisha wananchi katika kila hatua ya utekelezaji wa miradi ya kijamii. 

Kwa sasa karibu kata zote 17 za Halmashauri ya Mbogwe zimeongeza kiwango cha uwajibikaji kwa kufuata taratibu za mikutano ya mara kwa mara na kusoma mapato na matumizi. 

Maarifa hayo yamesaidia kuongeza kasi ya wananchi kujiletea maendeleo hasa katika kujenga miradi ya kijamii kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii kama maji, shule na zahanati ili kuboresha maisha yao bila kuisubiri Serikali.

Happiness Mshigwa, mkazi Kijiji cha Kanyegere, Kata ya Bukandwe wilayani humo anasema kutokana na uwazi wa mapato yanayotokana na shughuli za uchimbaji madini kwenye kata yao wamefanikiwa kujenga zahanati ambayo itawaondolea wanawake tabu kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya.

“Hapa tuna wawekezaji wa madini, lakini viongozi walikuwa wanakusanya mapato na hawafanyi chochote, baada ya sisi kuzinduka ndiyo tunayaona maendeleo hata barabara zinatengenezwa kwa wakati,” anasema Happiness (30).

Sehemu ya taarifa ya mapato na matumizi ya miradi ya maendeleo ya kijiji cha Shenda ambayo wananchi walisomewa hivi karibuni kwenye mkutano wa kijiji. Picha| Gift Mijoe.

Namna wanavyodhibiti wizi wa fedha

Licha ya wakazi wa Mbogwe kuhudhuria mikutano ya vijiji na kusomewa mapato na matumizi, wameenda mbali zaidi na kuunda kamati za wananchi ambazo ndani yake zina waraghabishi ambao kazi yao ni kufuatilia kila fedha inayoingia na kutumika. 

“Kila kinachofanyika ninatakiwa kupata taarifa kuhakikisha ni nini kinaendelea lakini tunadhibiti ufujaji wa mali za Serikali, zitumike mahali panapotakiwa,” anasema Paskary Bushoshi ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya Shule ya Msingi ya Muungano iliyopo kata ya Masumbwe wilayani humo.

Pamoja na umakini wa wananchi, bado wako baadhi ya viongozi wanatuhumiwa kwa ubadhirifu hasa kwa fedha zinazokusanywa kwa wananchi. 

Hata hivyo, wananchi wa kata ya Nyakafuru wamegundua njia ya kuwadhibiti viongozi hao kwa kuwahimiza wananchi kuchangia vifaa vya ujenzi vinavyohitajika wakati wa kujenga miradi na kupunguza uchangiaji fedha.

“Wakati wa kujenga hii zahanati yetu (ya kijiji ya Nyakafuru) tulikubaliana wananchi walete saruji, mawe, matofali na vifaa vingine ili hela zisikae kwenye mikono ya watu,” anasema Edward Sakay mkazi wa Nyakafuru.

Mbinu nyingine ambayo pia walifundishwa kwenye darasa la uraghabishi ni kufungua akaunti ya benki na kutunza fedha huko, anasema mkazi wa Nyakafuru, Rebeca Makenza.

“Ili fedha zitoke lazima wananchi walidhie na Mkurugenzi wa Halmashauri apate taarifa ya maandishi kuwa viongozi wanaenda kutoa fedha,” anasema Makenza na kuongeza kuwa utaratibu huo hawakuwa nao hapo awali. 

Hatua hizo zimepunguza vitendo vya rushwa, wizi wa fedha na kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na hivyo kuwawezesha kushiriki katika shughuli za kiuchumi ili kuboresha maisha ya familia.

Viongozi wahofia ‘kupigwa chini’

Viongozi wa halmashauri hiyo nao wameongeza kasi na kutambua dhamana zao kwa kujitenga na kila aina ya ubadhirifu unaoweza kuwawajibisha.

Kwa kuhofia kufurushwa, Diwani wa kata ya Bukandwe wilayani humo, Joseph Kilonja anasema viongozi wengi wanatekeleza majukumu yao.  

Kwa sasa, anasema ni vigumu kumkuta kiongozi wilayani humo “kazubaa” kwa sababu anajua asiposimama na wananchi kwenye uchaguzi hawezi kuchaguliwa tena.

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya Mbogwe, Martha Mkupasi aliiambia Nukta kuwa kila mwananchi katika wilaya hiyo yuko mstari wa mbele katika shughuli za maendeleo, jambo linalowafanya viongozi wasilale na watafute suluhu za matatizo yanayoibuliwa.

“Kwa sasa, hamasa ni kubwa tena wanawake ni wengi kuliko wanaume  kushiriki katika miradi ya maendeleo. Hii inarahisisha kazi ya kuwaletea wananchi maendeleo,” anasema Mkupasi ambaye sasa amehamishiwa Wilaya ya Chato.

Anasema viongozi katika Wilaya hiyo wanatakiwa kuona uraghabishi kama fursa kwa sababu wamewekwa katika nafasi za uongozi kutimiza matakwa ya wananchi. 

Mkazi wa kijiji cha Shenda, Justini Mkali akipanga tofali kwa ajili ya ujenzi wa darasa la Shule ya Sekondari ya Nyakasaluma lilipo kata ya Masumbe. Ujenzi wa shule hiyo umetokana na wananchi kuongeza kasi ya kushiriki katika miradi ya vijiji ili kujiletea maendeleo. Picha| Gift Mijoe.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW