Vituo zaidi ya 500 kutoa chanjo ya Corona Tanzania

July 30, 2021 3:03 pm · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Itatolewa katika vituo 550 katika mikoa yote.
  • Itakua ni hiari na bila malipo.
  • Makundi matatu wakiwemo watumishi wa afya kupewa kipaumbele.

Mwanza. Serikali inatarajia kuanza kutoa chanjo Corona (Uviko-19) kuanzia Agosti 3 mwaka huu katika vituo 550 katika mikoa yote ya Tanzania Bara kwa makundi maalum yaliyopewa kipaumbele kwa sasa wakiwemo watumishi wa sekta ya afya.

Makundi mengine ambayo yatapewa kipaumbele ni watu wazima umri kuanzia miaka 50 na kuendelea na watu wenye magonjwa.

“Kwa kuwa chanjo zilizopokelewa kwa sasa hazitoshelezi walengwa wa makundi yote nchini, makundi mengine yatapata chanjo katika awamu inayofuata, mara zitakapowasili,” amesema Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Profesa Abel Makubi. 

Prof Makubi amesema wizara yake imeanza kufanya usambazaji wa chanjo za UVIKO-19 katika mikoa yote nchini, huku ugawaji ukizingatia taarifa ya visa vya wagonjwa, idadi ya walengwa kwa kundi la kipaumbele pamoja na idadi ya chanjo zilizopo kwa sasa.

“Kama ambavyo Serikali imekuwa ikieleza, uchanjaji kwa  makundi yote nchini ni wa hiari au huru kwa kila mwananchi,” amesisitiza Katibu Mkuu huyo. 

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Profesa Abel Makubi (kulia) akionyesha vifurishi vya chanjo ambavyo vimeanza kusambazwa mikoani. Picha| Wizara ya Afya.

Jinsi ya kupata chanjo hiyo

Wananchi wote walengwa, wanaotaka kuchanjwa kwa hiari yao, wanatakiwa kufanya mambo yatuatayo kujihakiki kama wapo ndani ya makundi matatu (3) ya walengwa kwa sasa.  

“Kuandaa kitambulisho cha Kazi, NIDA, leseni ya udereva, mpiga kura,  

pasi ya kusafiria au kitambulisho chochote kinachotambulika kisheria,” amesema Prof Makubi katika taarifa yake iliyotolewa leo Julai 30, 2021.

Pia wanatakiwa kufanya “booking” ya siku ya kuchanjwa kwa kutumia simu na kompyuta kupitia kiunganishi cha https://chanjocovid.moh.go.tz  au kwa kwenda moja kwa moja kwenye kituo na kujisajili kuanzia Jumatatu Agosti 2, 2021 na kujaza fomu ya uhiari wa kuchanjwa.  

Wizara imeagiza waganga wakuu wa mikoa na wilaya nchini nzima kuhakikisha matayarisho yote muhimu  ili ifikapo Agosti 3 utoaji wa chanjo uweze kuanza katika vituo vilivyoainishwa katika mikoa.

Katika zoezi hilo wananchi walioasajiliwa katika mfumo wa Taifa wa chanjo watapatiwa cheti baada ya kuchanjwa  huku Serikali ikipiga marufuku hospitali yoyote  ya umma na binafsi kulipisha wananchi gharama yoyote.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW