Fifa yaanzisha kampeni kuwanusuru wenye matatizo ya akili duniani
- Ni baada ya changamoto zinazohusishwa na afya ya akili kuongezeka miongoni mwa wanamichezo.
- Zaidi ya watu milioni 200 wanakabiliwa na changamoto za afya ya akili ikiwemo msongo wa mawazo na kiwewe.
Dar es Salaam. Wakati idadi ya watu wanaopata matatizo ya akili ikiongezeka duniani, Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) limeanzisha kampeni maalum kwa ajili ya kujenga uelewa na kuwasaidia watu kuwa na afya bora ya akili.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), msongo wa mawazo unaathiri zaidi ya watu milioni 260 duniani kote huku nusu ya visa vya afya ya akili huanza pale mtu anapokuwa na umri wa miaka 14.
Rais wa FIFA, Gianni Infantino amesema kampeni iliyopewa jina la “ReachOut ni muhimu katika kuongeza uelewa wa watu kuhusu mazingira au dalili za afya ya akili na hivyo kuibua mjadala ambao unaweza kuokoa maisha.
Infantinoa amesema azma ya FIFA kwa mwaka 2020-2023 ni kufanya mpira wa miguu uwe kwa ajili ya jamii utakaosaidia watu kuondokana na mambo yanayochangia kuharibika kwa afya ya akili.
Mkuu huyo wa FIFA amesema msongo wa mawazo na kiwewe vinaathiri idadi kubwa ya watu duniani kote na vijana wako hatarini zaidi hivyo ili kuzuia hali hiyo, mjadala wa kifamilia, marafiki au wataalamu wa afya ni muhimu.
FIFA imeainisha vitu vya kusaidia mtu kuwa na afya bora ya akili i pamoja na kuzungumzia hisia zako, kuwasiliana na watu na kuwajali wengine. Picha| Persekutuan Mendaki.
Kampeni hiyo itaendeshwa kupitia chaneli za FIFA na kusambazwa kupitia vyombo vya habari na vyama shirika 211 vya shirikisho hilo la mpira wa miguu.
Changamoto za afya ya akili pia zinahusishwa na kujiua, ambako kunashika nafasi ya nne kama sababu ya vifo miongoni mwa vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 29.
UN imesema, hali ya watu wenye msongo wa mawazo na kiwewe inazidi kuwa mbaya zaidi hivi sasa wakati wa COVID-19 kwa sababu watu wanashindwa kupata matibabu, ajira zimepungua na wanatengwa.
“Kadiri COVID-19 inavyoendelea kutikisa, ni muhimu kuliko wakati wowote ule kupatia umuhimu afya ya mwili na akili. WHO ina furaha kubwa kushirikiana na FIFA katika kampeni hii ya #ReachOut na inahamasisha watu kuzungumzia afyaya akili,” amesema , Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dk Tedros Ghebreyesus wakati uzinduzi wa kampeni hiyo jana.
Kampeni hiyo inatekelezwa na FIFA, WHO na Jumuiya ya Nchi za Kusini Mashariki mwa Asia (ASEA) itaongeza uelewa wa watu kuhusu afya ya akili.
Latest