Mambo yanayowakwamisha wenye vipaji vingi
- Kuwa na vipaji vingi ni baraka lakini inawezakuambatana na changamoto zinazoweza kukurudisha nyumakimaisha.
- Unatakiwa kuwa na mipango madhubuti ya kudhibiti vipaji vyako ili vikusaidie kiuchumi.
- Tafuta ajira za muda mfupi kama kianzio cha kukusanya mtaji ili uhudumie vipaji vyako pale unapokuwa kwenye hatua ya chini.
Kati ya watu unaowafahamu, huenda kuna mmoja ambaye anauwezo wa kufanya vitu vingi kwa urahisi bila kutumia nguvu. Unaweza kuwa ni wewe, rafiki yako na hata ndugu yako.
Mtu huyo anaweza kuwa mcheza mpira, mwana muziki, na pia mbunifu wa mavazi kwa wakati mmoja. Vyote hivyo hafanyi kwa kubahatisha, anafanya kwa ueledi wa kutosha kiasi cha kuwashangaza wengi.
Vipaji vyao haviishii hapo. Utastaajabishwa siku moja kuwakuta wakifanya mambo mengine kwa ubora wa hali kama vipaji vyao vingine. Ni vipaji vingi ndani ya mwili mmoja.
Hata hivyo, baadhi yao hukutana na changamoto ya kushindwa kung’amua ni kipaji kipi kipaumbele kuliko kingine na namna wanavyoweza kutengeneza majina na kunufaika na vipaji husika.
Siku za hivi karibuni, nilipata nafasi ya kuongea na watu ambao wamefanya kazi na vijana wa aina hiyo.
Kati ya watu nilioongea nao ni wapiga picha wanaofanya kazi na watu wenye talanta mbalimbali, wakufunzi wa vijana na vijana ambao kushona, kuimba, kupiga gitaa angali ni wahandisi sio tatizo.
Watu hawa wamebainisha changamoto ambazo watu wenye vipaji vingi wanapitia.
Kuwa na vipaji vingi ni baraka lakini ukishindwa kuvidhibiti, vitakukwamisha. Picha| Pinterest.
Kutaka kufanya kila kitu kwa wakati mmoja
Kwa kuwa kila kitu kinafanyika kwa urahisi, kugusa kila kitu ni jambo ambalo mtu mwenye vipaji vingi anafurahia. Atataka kuimba, kuchora, kucheza, kufanya kazi, vyote kwa wakati mmoja.
Hata hivyo, Kwa mujibu wa Mpiga Picha kutoka K15 Photos, Emanuel Feruzi kutaka kufanya kila kitu kwa wakati mmoja kutampotezea mtu dira. Ili kubaki kwenye reli, Feruzi anashauri kutenga muda kwa ajili ya kila kitu unachokifanya.
“Unaweza kuanza na kuimba. Ukaupa muziki mwezi mmoja na kisha kuangalia umekua kwa kiasi gani. Kama haujaridhika, jiongezee muda kwenye muziki hadi uridhike na maendeleo yako,” ameshauri Feruzi.
Mtaalamu huyo wa picha na Tehama amesema mpango mkakati utamsaidia sana mtu mwenye vipaji vingi.
Kushindwa kulitambua jambo wanaloliweza zaidi
Licha ya kuwa na vipaji vingi, kuna kimoja kati ya vyote ambacho unakifanya vizuri kushinda vingine. Inaweza kuwa ni kuchora, kuimba na hata kufanya mawasilisho ya kiofisi.
Baadhi ya watu wenye vipaji wanashindwa kufahamu kati ya vipaji vyao, ni kipi ambacho wanakiweza zaidi na ni kipi ambacho kinanaweza kuwaingizia vipato.
Mbunifu wa majengo, mchoraji, mjasiriamali wa chakula na mwanamuziki, Sise Christopher amesema baada ya kutambua kuwa muziki ndio kipaji kikuu, ameweka mifumo ya kuhakikisha anapata fedha kwa ajili ya kukuza vipaji vingine.
“Huwa naimba sehemu mbalimbali ikiwemo kwenye harusi na shughuli binafsi ili kujiingizia kipato,” amesema Christopher.
Kukosa muda wa kuendeleza vipaji hivyo
Baadhi ya watu walio na vipaji, wameajiriwa kwa taaluma zao. Mfano mtu ambaye ni mzuri kwenye kucheza muziki ameajiriwa kama daktari, mwanamuziki ameajiriwa kama meneja na kadhalika.
Jambo hilo kwa baadhi linawanyima fursa ya kukuza vipaji vyao na hivyyo kushindwa kuvifanyia kazi ama kuviendeleza.
Erick Maleza ni Mhandisi, mwanamuziki, mbunifu wa bidhaa za ngozi na anapika pia. Kwake, amesema silaha kubwa ni kupata muda kwa ajili ya vipajji vyake licha ya kuwa na ratiba inayobana.
Erick amesema siku zote kuna muda wa ziada hivyo kuutumia muda huo kwa ajili ya kuendeleza kipaji chako itakusaidia.
Umewahi kujiuliza furaha ya moyo wako ipo wapi?katika vipaji vyote ulivyo navyo, jitahidi kufahamu moyo wako unafurahia kipi zaidi. Picha| Daniel Joram.
Kushindwa kuusikiliza moyo wako
Licha ya kuwa na vipaji vingi, moyo nao una sauti katika maisha yako. Ni moyo wako ndio utakaokupatia furaha na kiu ya kujifunza kitu pale unapohitaji.
Mkufunzi wa waajiriwa na waajiri, Moses Samora amesema siku zote kitu ambacho kinakuletea furaha zaidi unapokifanya ndiyo kitu kinachoweza kuwa wito wako duniani.
Wakati nikizungumza na Samora juu ya changamoto hizo, Mkufunzi huyo alinitumia video ambayo funzo lake ni;” zawadi kubwa unayoweza kujipatia ni kutafuta kitu ambacho unakifanya bila kinyongo na ukifanye. Siku zote hautokuwa kazini bali utakuwa katika uwanja wa michezo.”
Samora amesema hatua hiyo ni ngumu kuifikia kwani vipo vikwazo vingi ikiwemo fedha na juhudi kubwa za kukua lakini ukifikia kilele cha hatua hiyo utafurahia maisha yako.
Funzo la kubaki nalo
Licha ya kuwa na vipaji vingi ni muhimu kuhakikisha kuwa unatengeneza mifumo kwa ajili ya kupata fedha kutokana na vipaji hivyo. Feruzi aliniambia, unaweza kuwa na ajira ya muda (part time job) ambayo inaweza kukusaidia kukuza vipajj vyako vingine kwa kununua vitendea kazi na kujiendeleza.
Latest