Mchauno: TikTok yaipiku Facebook kwa ‘downloads’

August 10, 2021 12:25 pm · Clifford
Share
Tweet
Copy Link
  • TikTok yaongoza kwa kupakuliwa na watu wengi.
  • Kwa Julai imepakuliwa mara milioni 63.
  • Mabadiliko ya sera na Uviko-19 vyachangia.

Dar es Salaam. Wakati wamiliki wa mitandao ya kijamii wakiendeleza ushindani kupata wafuasi wengi, mtandao wa wa TikTok umetajwa kuwa ndiyo unaongoza kwa sasa kupakuliwa na watu wengi duniani.

Programu tumishi (App) ya TikTok ambayo hutoa fursa kwa watu kutengeneza na kusambaza video fupi umeipiku Facebook ambayo ilikuwa ndiyo inaongoza kwa kupakuliwa zaidi na watu kwa programu zisizo za michezo (non-gaming app).

Mtandao wa Tiktok ndiyo unaoongoza kwa kupakuliwa zaidi ya mara milioni 63 duniani huku ukiipiku Facebook ambayo kwa sasa unashika nafasi ya pili kwa kupakuliwa mara milioni 52 kwa mujibu wa takwimu za mwezi Julai mwaka 2021 zinazotolewa na  Sensortower

Nchi ambazo app hiyo ilipakuliwa zaidi mwezi uliopita ni China kwa asilimia 15 ikifuatiwa na Marekani kwa asilimia 9.

Mwezi Juni, Facebook ilishika nafasi ya kwanza ambapo ilipakuliwa mara milioni 53.

Instagram, WhatsApp na Messenger ni kati ya mitandao mitano ambayo imepakuliwa mara nyingi zaidi duniani kwa mwezi Julai.

Tiktok inayomilikiwa na kampuni ya ByteDance, imekua maarufu kutokana na watumiaji wake wanaweza kutengeneza video fupi na kushirikisha watu mtandaoni.

“Watu hutumia muda mwingi Tiktok kuliko YouTube nchini Marekani na Uingereza” amesema Chuzen Kin, Meneja Masoko wa App Annie, Kampuni inayojihusisha na masoko ya programu tumishi alipoongea na tovuti ya Nikkei Asia.

Apps zingine ambazo zimepakuliwa zaidi ni pamoja na Snapchati katika nafasi ya sita, Zoom, Telegram, CapCut na Google Meet.

Mitandao ya kijamii iliyopakuliwa mara nyingi zaidi duniani. Picha Unsplash

Huenda mafanikio ya TikTok yamechangiwa na janga la Uviko-19 ambapo yamechochea matumizi ya kijamii badala ya watu kukutana, hivyo kufungua fursa ya kutengeneza maudhui ya video ili kuonekana na watu wengi duniani.

Licha ya TikTok kupakuliwa zaidi, bado kuna mjadala kuhusu usalama wa taarifa za watumiaji wake huku.

Mwaka 2020 aliyekuwa Rais wa Marekani, Donald Trump aliiamrisha Tiktok kufunga ofisi zake nchini Marekani kwa kile alichodai ilikuwa inaisaidia China kudukuwa taarifa muhimu za nchi yake.

Licha ya marufuku hiyo ya Donald Trump, umaarufu wa mtandao huo ulioanzishwa 2017 ulikuwa maradufu hali iliyosababisha programu tumishi hiyo kupakuliwa mara nyingi katika bara la Ulaya, Amerika Kusini na Marekani.

Mwanzoni mwa mwaka 2021 mtandao wa WhatsApp ulitangaza kwamba unaazimia kushirikisha baadhi ya taarifa za watumiaji wa mtandao huo pamoja na Facebook. 

Licha ya WhatsApp kuwahakikishia watumiaji usalama wa taarifa zao, baadhi ya watumiaji walihamia katika mitandao mingine.

Telegram ambayo inashika imeshika nafasi ya nane kwa kupakuliwa, pia imefaidika na ongezeko la watumaji kutokana na sera zake za usiri kwa watumiaji. 

Watumiaji wa Telegram wanaweza kutuma jumbe ambazo zinaweza kutoweka baada ya kipindi fulani kadiri ya matakwa ya aliyetuma ujumbe huo.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW