Corona: Masharti mapya kuingia bungeni Dodoma

August 18, 2021 11:02 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Watakaoruhusiwa ni wale wenye shughuli za kiofisi tu.
  • Hiyo ni tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Uviko-19.

Dar es Salaam. Wakati vikao vya kamati 14 za kudumu za bunge zikianza jijini Dodoma leo, Ofisi ya Bunge imesema wanaoruhusiwa kuingia  bungeni ni wageni wanaofika kwa shughuli za  kiofisi ili kuepusha mkusanyiko wa watu na maambukizi ya Uviko-19.

Taarifa iliyotolewa na uongozi wa bunge Agosti 17, 2021 imesema kuwa kulingana na uwepo wa maambukizi ya corona nchini  watakaoruhusiwa kuingia bungeni ni waandishi wa habari waliosajiliwa kwa ajili ya kutoa habari za bunge.

Wengine ni wadau watakaohudhuria vikao vya kamati kwa ajili ya  kutoa  maoni ambao wataelekezwa na kamati inayohusika  kabla ya  kikao  cha  kupokea  maoni.

“Serikali kupitia  Wizara  ya  Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee  na  Watoto  imekuwa  ikitoa  elimu na miongozo  mbalimbali  ya  kujikinga   pamoja  na    kuchukua  hatua  katika  kuthibiti  kuenea  kwa maambukizi  ya  virusi  vya  corona, 

“Hivyo  imetoa  tahadhari  katika  vikao   vya  kamati  14  za  kudumu  za bunge  zinazokutana  t18 – 29 Agosti, 2021 kwa sababu  vikao  hivyo   vinahusisha  mkusanyiko wa waheshimiwa  wabunge,  watumishi  wa  Bunge,  watendaji  wa   Serikali,  waandishi  wa  wabari  na wageni  wengine  mbalimbali,” imeeleza taarifa hiyo. 

Aidha  katika  kutekeleza  kwa  vitendo  tahadhari  hizo  za  kiafya   uongozi     wa  bunge  umeweka utaratibu  wa  uendeshaji  wa  vikao  vya  kamati  ambao  ni  kutumika  kwa  kumbi  kubwa saba kwa  ajili  ya vikao  vya  kamati. 

Pia kamati zitakutana  kwa  kupishana  yaani  kamati  saba  ni  kuanzia   saa 3:00 asubuhi –  saa 7:30 mchana  na  kamati  nyingine saba  kuanzia  saa 8:00 mchana mpaka saa 12:30 jioni. 

Pia  kila  kamati  itafanya  vikao  kwa  namna  inayozingatia  muda  uliopangwa  ili  kutoathiri  muda  wa kuanza  kwa  vikao  vya  kamati  nyingine  na  idadi  ya  watendaji  wanaokuja  na  waziri  kwenye  vikao isizidi  maafisa  watano  wa  wizara  kwa  kila  kikao.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW