Fahamu mfumo jike unaotawala maisha ya tembo
- Tembo jike mzee ndiye kiongozi wa familia.
- Huishi katika koo na ukoo mmoja unaweza kuwa na tembo kuanzia nane hadi 100.
- Huishi miaka 50 hadi 70.
Siyo rahisi kuongelea utalii wa Tanzania bila kuwataja wanyama pori wetu wapatikana katika hifadhi za Taifa hasa wale wa kundi la ‘Big 5’ ambao ndiyo kivutio kikubwa cha watalii.
Simba, tembo, chui, kifaru na nyati ndiyo wanyama wanaounda kundi la hilo na neno hilo liliundwa na wawindaji wakijumuisha wanyama ambao ni wagumu kuwawinda wakiwa mbugani kwa mguu.
Kwa bahati mbaya, tembo ndiye mnyama anayewindwa zaidi na majangili kutokana na uhitaji wa ndovu zake kwenye masoko haramu ndani na nje ya nchi licha ya biashara hiyo kutokomezwa.
Kwa kawaida tembo katika makundi hutawaliwa na ufalme wa kike.
Tembo huishi katika koo na ukoo mmoja unaweza kuwa na tembo kuanzia nane hadi 100. Idadi kubwa ya wanafamilia wa koo hizi huwa ni majike yani bibi, mama, shangazi, dada na mawifi na madume wadogo ambao wote huongozwa na tembo jike mzee.
Makundi ya tembo ambao wanapatikana katika hifadhi ya Taifa ya Nyerere. Tembo hao wamekuwa wakivamia mashamba ya wananchi wa vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo. Picha|Mwaramu Mpunde.
Sifa zinazomtambulisha tembo
Akiwa na uzito usiyopungua tani sita ambao ni sawa na uzito wa gari aoina ya Toyota Coaster iliyobeba abiria ‘levo siti’. Tembo ndiye mnyamapori mkubwa zaidi kuliko wote ardhini na wanapatikana bara la Afrika na Asia tu huku maeneo mengine wakiishi kwa mateka au kwa kufugwa kwenye taasisi maalum.
Tembo wa Afrika wana masikio makubwa kuliko wa Asia. Tembo wa Afrika ana kichwa cha duara mithili ya yai huku tembo wa Asia ana kichwa kilichokaa kama duara pacha kikielekea kufanana na kopa, pia wana manyoya kidogo utosini.
Tembo wa Asia ana mgongo mbonyeo ambao humfanya aweze kutumika na binadamu kama usafiri huku tembo wa Afrika akiwa na mgongo mbinuko.
Mara nyingi tembo dume na jike wa Afrika wana ndovu ila kwa upande wa tembo wa Asia, ni madume pekee ndiyo wenye ndovu.
Afrika tuna tembo wa misituni na wa tambarare ambao ndiyo wenye miili mikubwa zaidi. Wengi wakiwa na urefu wa zaidi ya futi 10 huku binadamu mrefu kuliko wote duniani, Robert Wardlow ana futi nane na inch 11.
TANGAZO: Daima tuko na wewe katika kukupatia habari zinazokuhusu. Wenzako wamejiunga na jumuiya yetu ya Telegram ya @NuktaHabari, wewe unasubiri nini? Unaweza kujiunga kupitia kiunganishi hiki>> https://bit.ly/2TeLWIn

Namna wanavyozaliana
Tembo hubeba ujauzito kwa miezi 22 na huzaa ndama wa tembo mwenye kilo zaidi ya mia. Tembo anapozaliwa, mama yake humfundisha na humfanyia kila kitu, humlisha, humlinda, humuogesha, humkinga na jua na humsaidia kutembea mpaka atakapoweza kujitegemea.
Tembo hunyonyesha ndama wake na pindi pale ambapo hamnyonyeshi basi ndama huyo hunyonya mkonga wake kama vile mtoto mchanga wa binadamu anavyonyonya kidole gumba chake.
Ndiyo maana mara nyingi utaona ndama wa tembo akitembea chini ya tumbo la mama yake.
Kuna tendo la tembo kujipodoa, tendo hili huhusisha tembo kutumia mkonga wake kujimwagia tope na mchanga mgongoni mwake na anaweza pia kumfanyia ndama wake ili kuikinga ngozi yake na jua kali.
Kazi hii ya kulea ndama haifanywi na mama peke yake, kuna mashangazi na dada ambao lazima na wao watie mchango wao kwenye malezi ya huyu kinda ingawa kama ni dume, baada ya kufikia umri wa balehe hutoweka kwenda kujitegemea lakini kama ni jike basi ni nadra sana kuiacha familia yake.
Ndama wa tembo anapokuwa hatarini hupata msaada toka kwa kila mmoja aliyepo karibu na humzunguka kuhakikisha yupo sawa. Mshikamano huu wa tembo unaweza kufanya tembo mmoja kujitoa maisha yake kuokoa ndama au kuokoa kundi zima.
Bila kutofautiana sana na binadamu, tembo huishi miaka 50 hadi 70 na chakula kikubwa kikiwa ni mimea hususan mizizi, nyasi, majani, maua, matunda na matawi malaini na ana uwezo wa kula hadi kilo 150 kwa siku.
Mkonga wa tembo una nguvu ya kukata nyasi na matawi ya miti. Hutumika pia kama pua, kama mkono wa kulia chakula na hata kunywea maji maana mkonga huo unaweza kubeba hadi lita 14 za maji.
Ndovu za tembo hutumika pia kama mikono, hutumika kuchimbia mizizi, kuweka alama kwenye miti kama eneo lake la himaya na pia huzitumia kama silaha wakati wa mapambano.
Tembo akipigana hutumia ndovu, mkonga pamoja na miguu kumkanyaga adui yake pale anapoanguka na anaweza kutumia pembe ya upande mmoja vizuri zaidi ya upande mwingine kama ilivyo kwa mikono ya binadamu.
Tembo dume hupandwa na hasira pale ambapo yupo katika kipindi cha joto alafu anakosa jike wa kumpanda na madume wawili wanaweza kugombania jike mpaka mmoja wapo atakapoibuka kidedea. Mnyama huyu hukerwa pia na kelele, yale masikio makubwa yanasikia sana.
Ni mnyama mpole lakini upole wake una mwisho, majangili na wanyama wawindaji wanalitambua hili, tembo huwa haukimbii ugomvi, yeye humfuata adui yake na kupambana nae.
Tembo wa Asia ana mgongo mbonyeo ambao humfanya aweze kutumika na binadamu kama usafiri huku tembo wa Afrika akiwa na mgongo mbinuko. Picha| David Bebber.
Naweza KUsema tembo ana intelijensia kubwa kuliko wanyama wengine kana kwamba anaweza kutambua muziki, kuhisi huruma, kufurahi, kucheza mchezo ataofundishwa na ana kumbukumbu nzuri sana.
Tofauti na wanyama wengine, tembo anajitambua akijiona kwenye kioo na hawezi kuhisi kuwa ameona tembo mwingine.
Mwanafamilia anapofariki, tembo huomboleza pamoja kwa hisia na majonzi na maombolezo hayo huongozwa na tembo jike ambao ndiyo walio wengi kwenye ukoo, madume hupenda kujiweka mbali na matukio ya kifamilia.
Ndama wa tembo anapompoteza mama yake anabaki kuwa yatima na mashangazi huchukua jukumu zima la kumlea, lakini malezi hayawezi kufanana na ya mama, hivyo nafasi za ndama huyu kutoboa hadi ukubwani zinapungua kwa sababu kwa mujibu wa fisi, ndama wa tembo ana nyama tamu tu.
Una jambo lingine unalolifahamu kuhusu tembo?
Nasibu Mahinya ni mjasiriamali na Afisa Masoko wa soko la mtandaoni la utalii la TenTen Explore nchini Tanzania. Amekuwa mdau muhimu wa shughuli za utalii zinazofanyika ndani na nje ya Hifadhi za Taifa. Unaweza kumpata kupitia tovuti yake ya www.nasibumahinya.com.
Latest