Mbinu za kuondoa harufu mbaya kwenye gari yako

October 13, 2021 12:31 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kwa kutumia vitu vya jikoni ikiwemo mkaa na siki.
  • Harufu inaweza kusababishwa na maji kuingia kwenye gari au sehemu za ndani ya gari yako kuwa na uvundo.
  • Usiifiche harufu mbaya kwa kutumia manukato. Hakikisha unaiondoa kwanza.

Dar es Salaam. Siku za hivi karibuni, Gari ya ndugu yangu ilikuwa na harufu fulani hivi isiyofurahisha. Tukiwa nyumbani, tulifanya kila njia kuiondoa lakini hatukufanikiwa.

Tuliosha gari lote nje na ndani na hata chini, tumemaliza chupa za pafyumu za harufu nzuri na hata sehemu ya kuoshea magari yaani “car wash” nako tumeenda lakini harufu ile haikuisha.

Ilikuwa hadi jana usiku tuliposogeza kiti, tulikutana na nyanya iliyokuwa imejificha kwenye reli ya kiti cha dereva mbaya zaidi, ilikuwa imeharibika.

Licha ya kuitoa nyanya ile na kuacha gari wazi kwa muda mrefu, harufu kuisha kabisa kwenye gari ilikuwa “mbinde”.

Ilibidi tutafute njia mbadala kwani mchanganyiko wa harufu ya manukato ya gari na harufu ya nyanya iliyooza ilikuwa ni kama jehanamu ndogo. Tulishauriwa kutumia majani ya chai, na vitu vingi lakini ni mbinu moja tu ndio ilifanikiwa. ‘Baking soda’, unga unaotumika kwenye mapishi ya kuoka.

Harufu inaweza kutokana na uwepo wa uvundo kwenye mabomba ya kiyoyozi. Picha iStock.

Sababu zingine za harufu kwenye gari

Kwa mujibu wa tovuti inayoandika masuala ya magari, cars.com, harufu maarufu kwenye magari ni pamoja na jasho, harufu ya kitu kuungua, harufu ya uozo na uvundo. Pia harufu ya hitilafu za umeme na harufu ya gesi.

Harufu hizo zote zinaweza kusababishwa na aidha sababu za kiufundi ikiwemo hitilafu za umeme kwenye gari au injini kutokuwa sawa. Huenda kuna nyanya iliyoharibika kama ilivyokuwa kwetu hivi karibuni.

Cars.com imeandika kuwa, endapo harufu hizo hazitodhibitiwa, inaweza kusababisha changamoto kwenye gari ikiwemo afya.

Unawezaje kuiondoa harufu usiyoipenda kwenye gari yako?

Kulingana na kiwango cha harufu, zipo mbinu unazoweza kutumia kuondoa harufu usiyoihitaji kwenye gari yako. Fahamu ya kuwa, kupulizia manukato hakuondoi harufu bali inaficha tu kwa muda mfupi na huenda pia ikakuongezea harufu mbaya kwenye gari.

Pamoja na ‘Baking soda, iliyofanya kazi kwetu, hizii ni mbinu zingine unazoweza kuangazia pale gari yako inapokuwa na harufu usiyoihitaji.


TANGAZO

Fuatilia habari sauti kutoka Nukta Habari zinazojadili ripoti maalumu na filamu za kila ijumaa. Fuatilia kupitia Anchor, Spotify, au kokote unapopata podcast zako.


Tumia mkaa

Maajabu ya mkaa yameenda mbali zaidi ya kuwa dawa ya kung’arishia meno au kuchujia maji. Mkaa pia unaweza kutumika kufyonza harufu mbaya kwenye gari na sehemu mbalimbali.

Kwa mujibu wa Leith Toyota, unachohitaji ni vipande kadhaa vya mkaa kwenye mfuko na kuviweka kwenye gari yako usiku. Hakikisha umefunga milango na madirisha.

Asubuhi, Hautokuta harufu iliyokuwemo kwenye gari. Usiuwashe mkaa, uweke tu.

Baking Soda

Haiishii kwenye kupikia keki na maandazi tu. Leith Toyota imeandika kuwa, endapo unashughulika na harufu inayotokana na matapishi au matapishi yenyewe, baking soda inatakiwa kuwa chaguo lako la kwanza.

Unachotakiwa kufanya ni kuwa na chupa yenye baking soda na kutoboa matundu kadhaa kwa juu na kisha kuiacha kwenye gari kuondoa harufu. 

Kwa upande wa kuondoa madoa, lowesha sehemu yenya madoa au matapishi na maji kisha nyunyuzia unga wa baking soda na uuache kwa muda. Baada ya saa kadhaa, futa bila kutapakaza au kama ni sehemu kavu isiyo na matapishi, tumia mashine ya kufyonza vumbi (vaccum) kuiondoa baking soda.

Mbali na kutoa harufu mbaya, inasaidia pia kuondoa madoa yanayoweza kuachwa na matapishi kwenye kapeti na sehemu zingine za gari yako.

Unaweza kuweka mkaa kwenye makopo na kuacha makopo hayo kwenye gari usiku wote. Picha| Max.

Siki

Wamombo huiita “vinegar” na ni kiungo moja wapo jikoni. Siki hutumika kuua vijidudu ikiwemo bakteria na kuweka vikwazo visizaliane. Pia inatumika kama kihifadhi asilia (preservative) kwenye vyakula.

Kwa upande wa magari, siki inaweza kutumika kuondoa harufu kwenye gari. Leith Toyota inashauri kumiminia siki kwenye kikombe na kuacha kikombe hicho kwenye gari usiku kucha. 

Mlolongo wa uvukizi (evaporation) utaondoa harufu hata iliyoshindikana kwenye gari lako. Unaweza kujaribu hata kufuta sehemu yenye harufu kama unaifahamu kwa kutumia siki iliyochanganywa na maji. 

Inashauriwa kutokumwaga kimiminika cha siki peke yake sehemu yoyote ya gari yako kwani ina nguvu ya kutosha kuharibu kwa kuacha madoa sehemu za gari ikiwemo kapeti na ngozi. Mara zote, unapoitumia kufuta, changanya na maji.

Lakini kwa kuondoa harufu, weka kwenye kikombe na kiache kikombe hicho kwenye sehemu ambacho hakitadondoka.

Nakukumbusha tena na hata Leith imeandika, usitumie “air fresheners” kuficha harufu mbaya ya kwenye gari lako,  tumia tu pale unapokuwa na uhakika wa kuwa harufu mbaya kwenye gari yako haipo kabisa.

Jaribu njia moja na tuambie kama imekufaa. @NuktaTanzania.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW