Ujumbe kwa vijana kuelekea kongamano la kimataifa la mabadiliko ya tabianchi
Washiriki wakifuatilia warsha ya vijana na mabadiliko ya tabianchi katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) mkoani Pwani. Picha| Mtandao.
- Watakiwa kubuni suluhu dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.
- Jamii iwashirikishe katika mabambano na uwajibikaji.
- Kongamano hilo la COP26 litafanyika Uingereza kuanzia Oktoba 31, 2021.
Dar es Salaam. Wakati kongamano la Umoja wa Mataifa la Mabadiliko ya Tabianchi (COP26) likitarajia kuanza mwishoni mwa wiki hii, vijana wa Tanzania wametakiwa kuchukua hatua madhubuti na kushiriki kikamilifu katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika maeneo yao ili kuifanya dunia kuwa sehemu nzuri ya kuishi.
Kongamano hilo la COP26 linatarajia kufanyika kati ya Oktoba 31 hadi Novemba 12, 2021 jijini Glasgow nchini Uingereza ambapo litawakutanisha wataalam wa mazingira, viongozi wa serikali, mashirika na taasisi binafsi kujadili namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
COP26 ni muendelezo wa mijadala ya kimataifa ambayo inaziunganisha nchi mbalimbali ulimwenguni kutafuta suluhu ya kudumu ya mabadiliko ya tabianchi ambayo ni pamoja na kuongezeka kwa kina cha bahari, joto la dunia, ukame, mafuriko na vimbunga.
Mabadiliko hayo husababishwa na shughuli za asili na kibinadamu ikiwemo ongezeko la viwanda na watu, ukataji wa miti na matumizi ya nishati zisizo rafiki kwa mazingira.
Kutokana na mabadiliko hayo yanayoikumba dunia kwa sasa, wasomi wamewataka vijana kuwa mstari wa mbele kukabiliana na athari hizo ili kujenga mstakabali mzuri wa maisha yao ya baadaye.
Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, David Concar akizungumza Oktoba 24, 2021 katika warsha ya vijana na mabadiliko ya tabianchi katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) mkoani Pwani amesema vijana wana wajibu wa kuwa sehemu ya kutafuta suluhu za kudumu za mabadiliko ya tabianchi katika ngazi ya jamii.
Balozi Concar amesema wakati ni sasa na siyo wakati mwingine kwa vijana wa kila rika kutumia uwezo wao kubuni njia rahisi na za kibunifu ambazo zitasaidia kujiajiri huku wakikabiliana na mabadiliko ya tabianchi ili kujenga mstakabali mzuri wa maisha yao.
“Natoa wito kwa vijana kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kwa kufanya mambo mbalimbali ikiwemo urejelezaji wa taka,” amesema balozi huyo.
Amesema pia vijana wanatakiwa kuchagiza makubaliano ya kitaifa na kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi yafanyiwe kazi kivitendo ikiwemo kupunguza utoaji wa hewa ukaa, ukataji wa miti na uchafuzi wa mazingira ikiwemo matumizi yasiyo sahihi ya plastiki.
Baadhi ya wasomi walioshiriki warsha hiyo ya siku moja wamesisitiza kuwa suala la kupambana na mabadiliko ya tabianchi ni la kila mmoja bila kujali elimu, umri au nafasi aliyonayo kwenye jamii.
Mhadhiri Mwandamizi wa masomo ya urithi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Elgidius Ichumbaki amesema dunia tunayoishi ni lazima tuitunze kwa kuepuka mambo hatarishi yanayotishia uhai wa viumbe na mimea.
“Hakuna sehemu nyingine ya kwenda zaidi ya hapa duniani, kama kuna jambo la kufanya basi ni kushughulika na athari za mabadiliko ya tabianchi,” amesema Dk Ichumbaki.
Amesema vijana ni kundi muhimu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa sababu wana uwezo wa kuleta mabadiliko wakisimama imara.
Meneja Utafiti wa Mazingira na Uratibu kutoka Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Rose Mtui amesema Serikali ya Tanzania imeweka sera, sheria na mikakati mbalimbali kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na imekuwa ikihusisha wadau mbalimbali katika utekelezaji wake.
Amesema kila mtu kwenye jamii wakiwemo vijana wakichukua hatua ya kulinda mazingira itasaidia zaidi kumaliza athari za mabadiliko ya tabianchi.
Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, David Concar, viongozi wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) na wanafunzi wa shule za sekondari Tanzania baada ya kukamilisha warsha ya mabadiliko ya tabianchi. Picha| Mtandao.
Hata hivyo, wadau wengine wameshauri kuwa elimu kuhusu mazingira na mabadiliko ya tabianchi iongezwe zaidi kwenye jamii na kumfikia kila mtu ili kuongeza uwajibikaji katika kuzishinda athari za mabadiliko hayo.
Mwenyekiti wa Chama Chama Cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), Dk Hellen Otaru amesema kuna haja ya kuongeza uelewa kwa vijana kuhusu dhana za mazingira, sayansi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi, jambo litakarahisisha katika kukabiliana na athari za mabadiliko hayo.
Aidha, amesema mifumo ya uzalishaji na uagizaji bidhaa zikiwemo za kilimo uangaliwe upya maana imekuwa ikichangia katika kuharibu ardhi na vyanzo vya maji licha ya kuwa zina umuhimu kwa maisha ya binadamu.
Kongamano la CO26 ambalo ni muendelezo wa mkataba wa Paris wa mwaka 2015 kuhusu mabadiliko ya tabianchi litajikita katika kujadili na kuidhinisha suluhu mbalimbali ikiwemo matumizi ya magari ya umeme, kuachana na makaa ya mawe na ukataji miti usio na tija.
Pia itakuwa ni fursa muhimu ya kujadili na kupata maadhimio ya namna dunia inavyoweza kuwalinda watu wake dhidi ya mabadiliko ya tabianchi ili kuhakikisha wanakuwa na ustawi mzuri wa maisha.
Latest