Mbinu za kuongeza ushiriki wa vijana katika ujenzi wa uchumi Tanzania
- Waelimishwe kutokukwepa kulipa kodi kwani ndiyo uskani wa maendeleo ya taifa.
- Serikali iyafahamu makundi yao na itengeneze elimu kulingana na makundi hayo.
- Vijana waamke kuchangamkia fursa zinazowazunguka.
Dar es Salaam. Katika moja ya duka la kuuza vifaa vya kielektroniki maeneo ya Sinza mkoani Dar es Salaam, kijana mmoja alikuwa akiuliza bei ya spika janja.
“Hiyo ni Sh210,000 boss wangu,” alijibu muuza duka huku akiendelea kupanga bidhaa zake dukani humo.
Baada ya dakika mbili tatu za kujishauri, kijana huyo aliirudisha spika ile kwenye boksi na kumrudishia muuzaji.
“Kwani ulikuwa na bei gani bosi” aliuliza muuza duka. “Nilikuwa na Sh150,000,” alijibu mteja.
Kulikuwa na “mabembelezo” ya muda mrefu lakini wawili hao walikubaliana kufanya biashara kwa Sh180,000. Kijana alivuta kibegi chake cha ubavuni na kufungua zipu zake na kisha kuanza kuhesabu noti.
Alimpatia muuza duka na kisha alidai risiti yake. Kwa tabasamu la mshangao, muuza duka alimwambia, “kwa bei hiyo jomba siwezi kukupa risiti labda uongezee Sh5000. Haikuchukua dakika, mteja yule aliondoka bila risiti yake.
Mteja huyo pamoja na mfanya biashara, wamekwepa kulipa kodi ambayo ingesaidia kuipatia Serikali mapato ya kuboresha huduma za kijamii ikiwemo ujenzi wa hospitali, barabara na kugharamia matibabu ya wagonjwa.
Huyo ni mteja mmoja lakini wapo wengi ambao huenda wanapita katika mazingira kama hayo na unaweza kuwa mmoja wao.
Kwa mujibu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan katika mazungumzo yake na vijana yaliyofanyika Juni 15, 2021 Jijini Mwanza, vijana ni nguvukazi inayotegemewa sana kwa maendeleo ya Taifa.
“Uhai, usalama, maendeleo na ustawi wa Taifa lolote duniani linategemea vijana,” alisema Rais Samia katika kongamano hilo.
Kiongozi huyo wa nchi aliwaagiza vijana kuangazia kujiajiri kwani kwa takwimu zilizopo, asilimia 11.4 ya vijana duniani wenye uwezo wa kufanya kazi hawana ajira.
Rais Samia amesisitiza vijana kujiajiri na kutokusubiria ajira za serikalini.
Vijana wanashauriwa kujiajiri na kuingia kwenye mifumo inayowawezesha kulipa kodi. Picha| Single News.
Hata hivyo, yapo mambo mbalimbali ambayo yakifanyika yatasaidia vijana kujiajiri na kuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi.
Samaki akunjwe angali bado mbichi
Ushiriki wa vijana katika ujenzi wa uchumi unaweza kuwa wa nyanja nyingi na kati yake ni kushiriki kwenye kulipa kodi, madeni ya mikopo ya elimu ya juu na kujiajiri ili kuepuka utegemezi.
Mratibu wa mradi wa Kijana Wajibika kutoka taasisi ya masuala ya vijana ya Restless Development, Badru Rajabu ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa, huenda ni muda wa Serikali kuwekeza kwenye utoaji wa elimu ya kulipa kodi kwa vijana.
Jambo hilo linaweza kuanzia kwenye mitaala ya elimu na hata kuwafikia vijana pale walipo.
Endapo elimu ikitolewa mapema, vijana watafahamu umuhimu wa kulipa kodi na hakutakuwa na haja ya kuwashinikiza.
“Kinachotakiwa ni mabadiliko ya tabia miongoni mwa vijana kwani vijana ni wengi na wakikua bila kufahamu umuhimu wa kulipa kodi, watakuwa ndiyo wafanyabiashara wanaokwepa kodi baadaye. Wanasema samaki mkunje walau angali mbichi,” amesema Rajabu.
Hata hivyo, Rajabu pia anashauri kuwepo na uwajibikaji ili vijana wajue kodi zao zinaenda wapi na zinafanya nini.
TANGAZO:

Makundi ya vijana yazingatiwe katika utoaji wa fursa
Mabadiliko ya tabia pia yanaweza kuenda sambamba na kuwatambua vijana kimakundi ili kuifuma aina ya elimu kulingana na maeneo na kiwango chao cha elimu.
Mdau wa mambo ya vijana wa Mkoani Dar es Salaam, Sylvester Mani amesema ni muda wa elimu kuacha kutolewa kijumla na badala yake, itolewe kulingana na makundi ya vijana yalivyo.
Mani ameiambia Nukta Habari kuwa, vijana wapo kwenye makundi mawili. Moja ni kulingana na eneo walilopo na la pili ni kiwango cha elimu hivyo fursa zilizopo hazitakiwi kutolewa kiujumla bali zilenge makundi ya vijana kulingana na vigezo hivyo.
“Tunaweza kujadili umuhimu wa vijana kwenye ujenzi wa uchumi kwa kutengeneza makundi. Kundi la kiwango cha elimu na kundi la kuzingatia eneo walilopo,” amesema Mani.
Kwa eneo walilopo, Mani amesema kuna vijana wa vijijini na mjini ambapo wa mjini wapo vizuri kwenye kuchangamakia fursa za muda mfupi lakini udhaifu wao ni kuendeleza biashara.
Kwa vijana wa kijijini, wengi wanategemea shughuli za kilimo na mzunguko wa fedha kwao ni mdogo.
Kwa ushauri wa Mani, elimu itolewe ikizingatia hali za vijana na fursa za maendeleo zinapokuja, zitolewe zikilenga nguvu na udhaifu wa makundi ya vijana yaliyopo.
Ili vijana wajue kinachoendelea, hawana budi kufuatilia vyanzo vya taarifa muhimu nchini. Chanzo| Youth Talk.
Vijana wafahamu kinachoendelea
Kutokana na ugumu wa maisha, vijana wengi wapo kwenye riadha ya kutafuta mafanikio. Huyu ni mfanya biashara, huyu ni “Mishe town” na kila kijana anafanya lake kuhakikisha mkono unaenda kinywani.
Hali hiyo inawafanya baadhi kupitwa na mambo yanayoendelea nchini ambayo huenda zinaweza kuwemo fursa kwa ajili yao.
Mdau wa Maendeleo Endelevu (SDG’s Champion) ambaye pia ni Mtaalamu wa Diplomasia ya Uchumi mkoani Dar es Salaam, Hilder Gasper ameiambia Nukta kuwa inatakiwa vijana wajue kinachoendelea.
Gasper amesema, vijana wengi hawana uelewa na mikakati ya Serikali, sera za maendeleo na hata mipango ya yake juu ya maendeleo yao.
“Kuna mafunzo ambayo Serikali hutoa tena bure mtu anaweza kuchangamkia nafasi hiyo na kuongeza ujuzi,” amesema Gasper.
Mdau huyo wa maendeleo pia ameshauri vijana kuyafahamu mashirika na taasisi ambazo zinafanya kazi na vijana ikiwemo benki zinazotoa mikopo kwa ajili ya kilimo, mashirika yanayosaidia kampuni changa na miradi inayokuja nchini.
“Kuna miradi inakuja nchini. Vijana wanaweza kuichangamkia wakapata ajira na hata kuanzisha biashara kufuatia miradi hiyo. Wengine wanaweza kuomba hata tenda ya miradi hiyo wakapata hata hela ya chakula,” amesema Gasper.

Ni muda wa kugeuza changamoto za jamii kuwa ajira
Katika jamii, kuna changamoto nyingi ambazo zinaendelea. Magonjwa, ukame na pia ukosefu wa ajira na elimu.
Katika changamoto hizo, Afisa Mawasiliano wa Kampuni ya huduma za kifedha, Brac Tanzania, Jackline Chriss amesema vijana wanaweza kuzigeuza changamoto hizo kuwa sababu ya wao kuingiza kipato kwa kuzitatua.
“Vijana waangazie fursa zilizopo kwenye changamoto za jamii. Kupitia hizo, wanaweza kuzitatua na kutengeneza ajira,”ameshauri Chriss.
Mdau huyo wa maendeleo ameshauri vijana kutokuonea haya mikopo endapo wakiwa na uhakika wa mipango waliyonayo katika matumizi ya mikopo hiyo.
Juhudi za serikali katika kuhakikisha vijana wanashiriki shughuli za maendeleo zimeendelea kuonekana kuanzia katika mitandao ya kijamii, televisheni kupitia matangazo ya kuhamasisha ulipaji wa kosi na vilevile vijana kujiajiri.