Mapinduzi mapya kamera za simu janja

November 19, 2021 3:50 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni ugunduzi wa teknolojia ya “under screen cameras”.
  • Teknolojia hiyo inaificha kamera ndani ya simu.
  • Lakini bado ufanisi wake siyo mzuri, wagunduzi kuiboresha zaidi.

Dar es Salaam. Najua siko peke yangu ambaye napenda skrini ya simu yangu iwe skrini tu bila kuingiliwa na kitu kingine chochote. Siyo kamera, siyo batani ya seezi (fingerprint)! Skrini kuanzia mwanzo wa kona moja hadi kona nyingine.

Hata hivyo, kwa miaka ya nyuma ilikuwa haiwezekani simu kuja na srini ya mbele bila kamera. Zipo chache zilizojaribu kuificha kamera na kuileta kwa muundo wa kuchomoza (pop up camera) ikiwemo Samsung Galaxy A80, OnePlus 7 Pro, Oppo Reno 10x Zoom na LG Wing.

Kwa mtazamo wangu kama mtumiaji wa simu janja, pop up camera ni nzuri lakini kuna kitu ambacho hakinipatii amani kwa kamera kuchomoza kila nikitaka kupiga picha, ikivunjika je? Maana katika upigaji picha kuna mengi.

Teknolojia mpya ya “Under Display Camera (UDC)” huenda ndiyo suluhisho la yote. Kamera ambayo imetengenezwa ndani ya skrini.

Kama umetumia baadhi ya simu ambazo teknolojia ya seezi ipo ndani ya skrini unaweza kuelewa jinsi gani teknolojia ya UDC imewekwa.

Kamera ya mbele haionekani kabisa. Utahitaji juhudi za ziada kuiona. Picha| GadgetMatch.

Mwanzo wa UDC

Teknolojia hii ilianza na simu aina ya ZTE’s Axon 20 ambayo kwa mujibu wa baadhi ya wadau wa teknolojia, kamera ya simu hiyo “ilikuwa mbaya”.

Axon 20 iliingia sokoni na teknolojia hiyo na haikua na muingiliano wa kitu chochote kwenye kioo cha ckrini ya simu.

Awali, watengenezaji wa simu walijaribu kuiweka kamera kwa muundo wa Hole-punch kama ilivyo  kwa teknolojia ya  “Honor V20, pop-up, Water drop, Sliding screen na Notch screen” ambayo inatumika kwenye simu zote za Apple kuanzia iPhoneX.

Mwanzo wa UDC kwa Axon 20 haukuwa mzuri, kamera yake iliripotiwa kuwa na uwezo usioridhisha na sehemu iliyowekwa kamera hiyo iliripotiwa kutokuwa nzuri.

Mwaka huu, kampuni ya Samsung iliingia “mkenge” baada ya kuitoa simu yake ya Galaxy Z Fold 3 na kamera ya UDC lakini ikiwa na matatizo yale yale ya Axon 20.

Hata hivyo kukosea ndiyo kujifunza. 


Soma zaidi


Waliolielewa somo wakaingia sokoni

Hivi karibuni, kampuni ya kutengeza simu nchini China, Xiaomi Inc ilitazama teknolojia hiyo kwa jicho tofauti. Iliingiza sokoni simu ya Mix 4 yenye UDC baada ya kuwekeza takriban Sh177 bilioni kuiboresha teknolojia hiyo kuhakikisha haipiti na kasoro.

ZTE nao walirudi sokoni na ZTE’s Axon 30 ikiwa imeboreshwa kamera kuliko mtangulizi wake, Axon 20.

Simu ya kwanza kuwa na teknolojia ya UDC ilionyesha sehemu kamera hiyo ilipofichwa. Picha Geek tech online.

Bado teknolojia inahitaji marekebisho

Kwa kuwa ni simu tatu tu hadi sasa ambazo zinatumia teknolojia hii, utafiti wa kuiboresha bado unaendelea.

Matoleo ya mwaka huu ni bora kuliko mwaka jana lakini haizifanyi kamera hizi kuwa kamera bora sokoni hasa kwa wapenda picha za mbele (selfie).

Mchambuzi wa masuala ya teknolojia kutoka Shirika la Habari la The Verge, Sam Byford amesema Samsung, Xiaomi na ZTE wamechukua maamuzi mazito ya kuharibu ubora wa kamera kwa kutafuta muonekano mzuri wa skrini.

Hata hivyo, kwa wasiopenda kamera ya mbele, huenda wakawa hawana shida. 

Byford amesema picha nyingi anazopiga mtu zinaweza kutumika lakini changamoto inakuja pale mtu anapotaka kuitumia kamera kwa mazingira mubashara mfano simu za video na kurekodi video. 

“Ukiangalia kwa makini unaweza kuona ya kuwa kamera inatumia nguvu nyingi kuleta matokeo,” amesema Byford.

Mimi na wewe hatujui teknolojia hii itafikia  wapi lakini kadri tunavyoishi, huenda hii ndiyo ikawa kesho kwa simu janja.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW