Ina maana gani bei ya petroli, dizeli kupanda Tanzania?

December 2, 2021 8:38 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Bei za mwezi Desemba zimepanda kwa bei tofauti.
  • Itawaongezea watumiaji wa mafuta gharama za ziada.
  • Serikali yasema inachukua hatua kupunguza bei.

Dar es Salaam. Wamiliki wa vyombo wanamaliza mwaka 2021 kwa maumivu baada ya bei ya petroli na dizeli kupanda kwa viwango tofauti kwa mwezi Desemba, hivyo kuwafanya watoboe zaidi mifuko yao kuipata nishati hiyo.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), bei ya rejereja ya mafuta ya petroli yanayopitia Bandari ya Dar es Salaam kwa mwezi Desemba imepanda hadi Sh2,510 kwa lita moja.

Bei hiyo imepanda kutoka Sh2,439 kwa lita moja iliyotumika mwezi uliopita wa Novemba. Hiyo ni sawa na ongezeko la Sh71 kwa lita moja ambayo wamiliki wa vyombo vya moto watakayolipia kupata nishati hiyo ikilinganishwa na mwezi uliopita.

Mafuta yanayopitia Bandari ya Dar es Salaam hutumiwa hasa katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.

Ongezeko la bei ya petroli limeshuhudiwa pia katika Bandari ya Mtwara (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara) ambapo mafuta hayo yamepanda hadi Sh2,525 kwa mwezi Desemba kutoka Sh2,478 kwa lita iliyotumika mwezi uliopita.

Kwa Bandari ya Mtwara, petroli imepanda hadi Sh2,569 kwa lita kutoka Sh2,455 kwa lita iliyotumika Novemba 2021 ikiwa ni ongezeko la Sh114.  Mafuta hayo hutumiwa na wananchi wa Mtwara, Lindi na Ruvuma.

Kupanda kwa bei ya petroli kunamaanisha kuwa wanunuzi wa nishati watalazimika kuongeza bajeti ya mafuta ikilinganishwa na waliyotumia mwezi uliopita, hivyo kuwaongezea gharama za maisha.

Huenda pia kiasi hicho cha fedha wanachoongeza kwa kila lita moja wangekielekezwa katika matumizi mengine ikiwemo kufanya maandalizi ya sikukuu za mwisho wa mwaka ikiwemo mwaka mpya wa 2022.

Madereva wa maroli ni miongoni mwa watu wanaoathirika bei ya mafuta ikipanda. Picha | Isakwisa Mbyale.

Ewura katika taarifa yake imeeleza kuwa kupanda kwa bei ya mafuta nchini Tanzania kumechangiwa na ongezeko la nishati hiyo katika soko la dunia na hivyo kuathiri bei za ndani.

Hata hivyo, bei ya mafuta inatarajia kushuka katika siku za hivi karibuni kutokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa duniani ikiwemo kuongeza kiasi cha mafuta kinachouzwa katika soko la dunia.

“Kulingana na mwenendo wa bei za mafuta katika soko la dunia, bei za mwezi Novemba 2021 zimeanza kushuka. Kwa kuwa bei za soko la dunia zinaakisiwa katika soko la hapa nchini baada ya miezi miwili, unafuu wa bei za soko la dunia ulioanza kujitokeza katika mwezi Novemba 2021 unatarajiwa kuonekana katika soko la hapa nchini katika bei za mwezi Januari 2022,” imeeleza Ewura.

Maumivu hadi kwa watumiaji wa dizeli

Wakati wa watumiaji wa petroli wakiugulia maumivu ya kupanda bei, hali hiyo pia haitawaacha salama watumiaji wa dizeli kwa sababu huko nako bei imepanda kwa viwango tofauti.

Kwa mujibu wa bei kikomo za Desemba zilizotangazwa na Ewura jana Desemba 1, 2021, bei ya dizeli inayopitia Bandari ya Dar es Salaam imeongezeka hadi Sh2,392 kwa lita kutoka Sh2,243 kwa lita ya mwezi Novemba.

Hiyo ina maana kuwa watumiaji watalipa Sh149 kwa lita moja ikilinganishwa na bei waliyokuwa wananunulia mwezi uliopita. 

Ongezeko hilo la bei ya dizeli iliyopitia Bandari ya Dar es Salaam ni zaidi ya mara mbili ya ongezeko la bei ya petroli ambayo ni Sh71 kwa lita moja.

Katika Bandari ya Mtwara, dizeli imepanda kutoka Sh2,279 kwa lita mwezi Novemba hadi Sh2,423 kwa lita huku inayopitia Tanga, bei yake imepanda hadi Sh2,413 kwa lita kutoka Sh2,245 kwa lita. 

“Kwa mafuta ya taa, bei itakuwa Sh2,235 kwa lita kwa Dar es Salaam na bei za bidhaa hiyo kwa mikoa yote nchini zimekokotolewa kwa kujumuisha gharama za usafirishaji mpaka miji husika,” imesema Ewura.

Baadhi ya watumiaji wa magari jijini Dar es Salaam, wamesema kuendelea kupanda kwa bei ya mafuta, kunawaumiza kwa sababu kunaongeza gharama za maisha hasa kuelekea mwisho wa mwaka.

“Ninatumia Sh300,000 kila mwezi kununua petroli kwa ajili ya gari yangu, bei ikipanda zaidi itabidi niache gari nyumbani maana hali haiko sawa,” amesema Jamal Hussein, mkazi wa Mapinga mkoani Pwani.

Dereva wa malori wa jijini Dar es Salaam, John Mkwaja ameiomba Serikali kuliangalia suala hilo na kutafuta namna ya kushusha bei hizo ili kuwapunguzia maumivu ambayo yamedumu kwa muda sasa.

Hata hivyo, Ewura imesema, “Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la dunia na kufanya kila linalowezekana ili kuepukana na madhara yanayoweza kujitokeza katika mnyororo mzima wa uchumi hapa nchini iwapo bei zitaongezeka kwa kiwango kikubwa.”

Pia, itaendelea kufanya marekebisho yatakayohitajika katika tozo na kodi mbalimbali za Serikali. 

Kuepusha madhara ya ongezo hilo la bei za mafuta katika uchumi na maisha ya wananchi, mwezi Julai 2021, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, aliagiza hatua madhubuti zichukuliwe kwa lengo la kupunguza bei za mafuta ili wananchi waweze kununua mafuta kwa bei nafuu.

Baadaye Oktoba 2021 Waziri wa Nishati, January Makamba, alipunguza tozo na ada zinazotozwa na taasisi za Serikali katika bidhaa za mafuta na kupanga kununua bidhaa za mafuta moja kwa moja kutoka kwa wasafishaji wa mafuta (refineries) kwa lengo la kuendelea kupunguza bei za bidhaa za mafuta hapa nchini. 

Pamoja na hatua hizo, Serikali inashirikiana na wafanyabiashara wa mafuta hasa wale wanaouza mafuta kwa jumla kwa lengo la kuhakikisha bidhaa za mafuta zinaendelea kupatikana kwa bei nafuu.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW