Kiwanda kinachopambana kuondoa taka mtaani, kuhifadhi mazingira

December 11, 2021 7:01 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kiwanda cha urejelezaji taka za plastiki kilichopo Arusha.
  • Kimetoa fursa ya ajili kwa vijana kulinda mazingira.
  • Serikali, wadau wasema kasi kudhibiti taka iimarishwe.

Mwanza. Huenda kasi ya ukataji wa miti kwa ajili ya utengenezaji madawati, viti na meza ukapungua, baada ya wabunifu kubuni njia ya mbadala ya kupata ,malighafi za samani hizo.

Mwongozo wa upandaji na utunzaji wa miti Tanzania uliotolewa na Wakala wa Mbegu za Miti Tanzania (TTSA) uliotolewa mwaka 2017, unaeleza kuwa misitu imefunika hekta zaidi ya milioni 48 ya ardhi ya Tanzania.
Hata hivyo, misitu hiyo iko hatarini kutoweka kutokana na kasi ya ukataji miti kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwemo nishati ya kupikia na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Taifa ya Takwimu za Mazingira ya mwaka 2017 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), kiwango cha ukataji miti kinakadiriwa kuwa ni hekta 372,000 kwa mwaka.

Hofu hiyo ya kutoweka kwa misitu ndiyo imewaibua Juma Shabani na wenzake 13 kuanzisha kampuni ya Greenventure Tanzania iliyopo mkoani Arusha kwa ajili ya kufanya shughuli za urejelezaji wa taka za plastiki ili kutengeneza bidhaa mbalimbali.

Shabani ambaye ni meneja oparasheni anasema lengo la kiwanda hicho ni kuhakikisha taka zote zitokanazo na plastiki zinaondoka mitaani ili kuweka mazingira safi na salama.

Akizungumza na Nukta habari, Shabani anasema walianza shughuli hiyo mwaka 2015 baada ya mmoja wa waanzilishi wa kiwanda hicho, Edgar Edmund kushuhudia mafuriko yaliyotokea jijini Dar es Salaam na kusababisha nyumba nyingi kuanguka.

Sababu kuu ya nyumba hizo kuanguka ilibainika ni kutokana na taka hizo kuziba kwenye mitalo ya maji na kusababisha maji kushindwa kusafiri.

“Tulifikiria kuwa tunaweza kufanya kitu kupitia hizi taka zinazoonekana mtaani na kutengeneza kitu kingine ambacho kina manufaa kwa jamii,” anasema Shabani.

Baada ya makubaliano hayo hatua za kutafuta eneo kwa ajili ya shughuli hizo ulianza, kisha vikanunuliwa vifaa vya kusaga taka hizo na kuzigandisha kwa ajili ya kutengeneza bidhaa mbambali.

Miongoni mwa vifaa vinavyotengenezwa kupitia taka za plastiki ni madawati, mbao, viti na sturi kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na ofisini.

“Kwa mara ya kwanza baada ya kuanza uchakataji tulitengeneza dawati, dawati hilo lina uwezo wa kuishi miaka 500, tuliona ni jambo la busara kwa kuwa litasaidia katika kutatua changamoto za uhaba wa madawati kwa wanafunzi,” anasema Shabani wakati wa maonyesho ya wajasiriamali jijini Mwanza hivi karibuni.

Taka hizo huchambuliwa na kusagwa vizuri katika mashine maalum kabla ya kutengeneza bidhaa maalum. Picha| Greenventure Tanzania.

Taka hizo zinatoka wapi?

Kiwanda hicho kimeajiri zaidi ya vijana 130 ambao shughuli yao kuu ni kuokota taka katika maeneo tofauti ikiwemo hotelini, barabarani na majalalani na kuziwasilisha kiwandani kwa ajili ya uchakataji.

Uondolewaji wa taka hizo kwenye majalala, mito na maziwa zinasaidia kupunguza athari ambazo binadamu wanaweza kukutana nazo. Mathalan, taka hizo zinazotupwa baharini au ziwani zinaweza kuathiri samaki waliomo na kisha hao samaki wanaovuliwa wakiliwa na binadamu madhara yanaweza kutokea.

Kwa siku kiwanda hicho hununua zaidi ya kilo 250 za taka za plastiki na toka kiwanda kianze tani 60 za taka zishakusanywa mtaani na maeneo mengine.


Soma zaidi: 


Mafanikio

Hadi sasa kiwanda hicho kimeweza kuzalisha madawati yanayotokana na taka za plastiki, mbao ambazo watu wanaweza kuzitumia kutengenezea nguzo, sturi na mapambo.

Kwa upande wa madawati, Shaban anasema wametengeneza madawati mengi japokuwa bado hajapata soko la uhakika, na kuwa dawati moja huliuza Sh140,000.

Pamoja na mafanikio hayo, Shabani anakili bado kiwanda kinakumbana na changamoto nyingi ikiwemo bidhaa hizo kutouzika, lakini pia hawajaweza kufikia maeneo mengi kwa ajili ya kuzikusanya taka hizo.


Asasi za kiraia zinasemaje

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika lisilokuwa la Serikali la uhifadhi wa mazingira (Emedo) Editrith Lukungu anasema kuna umuhimu wa kuwasaidia vijana ambao wanafanya kazi ya kukusanya taka za plastiki na kuzalisha bidhaa kwa sababu wana mchango mkubwa wa kulinda mazingira.

“Taka zinazokusanywa ndani ya Ziwa hilo ni kama vile, ndala zilizoisha, mifuko ya plastiki na chupa za plastiki, baada ya kukusanywa kwa taka hizo hutumiwa kwa ajili ya kutengeneza bidhaa kama mapambo, viti, boti na banda linaloweza kutumika kwa huduma za mgahawa,” anasema Lukungu.

Mkurugenzi huyo anasema jamii inatakiwa kubadilirika na kuacha mazoea ya kutupa taka ovyo ambayo licha ya kuchafua mazingira lakini pia zisababisha ardhi isitoe rutuba kwa asili ya ukuaji wa mazao.

“Ni vema kujitengenezea utaratibu wa kuwa na vifaa vya kutupia taka, zoezi hilo likifanywa na kila mmoja litasaidia katika utunzaji wa mazingira,” anasema.

Taka za plastiki ni malighafi muhimu ya utengenezaji samani kama viti na meza kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na ofisini. Picha| Greenventure Tanzania.

Shirika la Mazingira ya Umoja wa Mataifa (UNEP) linaeleza kuwa kila dakika moja, chupa za plastiki za maji zinanunuliwa na kutumiwa mara moja kisha kutupwa huku ni asilimia tisa tu ya taka za plastiki ndiyo zinarejelezwa.

UNEP inapendekeza hatua madhubuti zichuliwe kudhibiti uzalishaji wa chupa na kuweka mifumo itakayohakikisha taka hizo hazileti madhara kwenye mazingira.

Mkuu wa Kitengo cha usafi na mazingira mkoani Mwanza, Ally Salim anasema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kudhibiti taka za plastiki ziharibu mazingira kwa kutoa elimu, kuchagiza teknolojia ya urejelezaji.

Akizungumzia matumizi ya taka hizo katika kutengeneza vifaa mbalimbali kama madawati na mbao, Salim anasema yatasaidia kuondokana na tatizo la ukataji miti ovyo na hivyo kulinda misitu.

“Ni kitu kizuri kinachofanywa kwa kuwa licha ya kusaidia kuboresha mazingira lakini pia kitasaidia katika uhifadhi wa miti na misitu, pia madawati haya yatasaidia kuondokana na tatizo la kununua madawati kila mwaka kutokana na uharibifu,” anasema Salim.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW