‘Chungu’ ya chupa za plastiki za rangi Tanzania
Chupa za plastiki za rangi hasa nyeusi hutumika kuhifadhia vinywaji vya kuongeza nguvu (energy drinks) zimekuwa zikizagaa maeneo ya mijini ikiwemo Dar es Salaam jambo ambalo linazidisha uchafuzi wa mazingira. Picha| Suleman Mwiru.
- Uzagaaji wa chupa hizo wazidi kuongeza uchafuzi wa mazingira jijini Dar es Salaam.
- Waokota chupa za plastiki walalamika kukosa pesa kutokana na chupa hizo kukataliwa na viwanda vya urejelezaji.
- Serikali yaagiza kuwekwa mfumo mzuri wa kuzirejeleza.
Dar es Salaam. Issa Emmanuel, akiwa Mwananyamala, jijini Dar es Salaam anasubiri mzigo wake wa chupa za plastiki upimwe ili aweze kujipatia pesa yake, baada ya kuzunguka mitaani kuziokota tangu alfajiri.
Issa ambaye kazi yake ya kuokota taka za mifuko na chupa za plastiki na vyuma chakavu ni moja ya watu muhimu kwenye jamii wanaoendeleza kazi ya kupunguza chupa za plastiki mtaani kwa kuziokota na kuziuza kwa ajili ya matumizi mengine (Recycling).
Hata hivyo, Issa ambaye anaishi Mwananyamala bado hajafaidika kikamilifu na kazi hiyo kwa sababu siyo chupa zote za plastiki anazookota mtaani zinakubaliwa na wananunuzi.
‘’Hii ni hela, roho mimi inaniuma nikizikuta, na ni nyingi, nikivuka kwenye mtaro nazitamani ni nyingi kweli kweli,” anasema Issa kwa masikitiko.
Chupa za plastiki za rangi hasa nyeusi hutumika kuhifadhia vinywaji vya kuongeza nguvu (energy drinks) zimekuwa zikizagaa maeneo ya mijini ikiwemo Dar es Salaam jambo ambalo linazidisha uchafuzi wa mazingira.
Utupaji hovyo wa chupa hizo unasababisha kuziba kwa mitaro, muonekano mbaya wa mitaa, uchafuzi wa vyanzo vya mji ikiwemo mito na bahari. Pia huchangia kuharibu rasimali bahari na vifo kwa viumbe vyake.
“Hizi chupa zikiletwa hapa hazinunuliwi zinakataliwa, sasa unakuta zinatupwa zinazagaa kwenye maji au kwenye mifereji” anasema Maimuna Ibrahimu mkazi wa Tandale jijini Dar es Salaam, ambaye anajishughulisha na uokotaji wa chupa za plastiki.
Kwa mujibu wa Programu ya mazingira ya Umoja wa kimataifa (UNEP), chupa za plastiki milioni 1 kinanunuliwa kila dakika duniani, huku tani milioni 300 za taka za plastiki zikizalishwa kila mwaka, kiasi ambacho kina karibia uzito wa watu wote duniani.
Hali hiyo imesababisha taka za plastiki kutapakaa kwenye mazingira, na kuwa sehemu kubwa ya mabaki duniani, jambo ambalo linazidisha athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo mafuriko na ongezeko la joto.
Athari hizo huenda zinachangiwa na baadhi ya watumiaji wa vinywaji vya kuongeza nguvu kutokuwa na uelewa mzuri kuwa chupa hizo zinaharibu mazingira yanayowazunguka.
‘’Kama hivi kwenye kazi zangu labda kama nimeshanunua barabarani huko natembea nakunywa huwezi kutupa sehemu salama lazima tu utupe barabarani”, anasema Anderson Karim, mkazi wa jijini Dar es salaam ambaye anapendelea vinywaji vya kuongeza nguvu.
Anderson anakiri kuwa licha ya kutupa chupa hizo hovyo, anafahamu kuwa chupa hizo huwa haziokotwi.

UNEP inaeleza kuwa kati ya tani bilioni saba za taka za plastiki ni asilimia 10 pekee ndizo hurejelezwa (recycled), huku mamilioni ya taka hizo yakiishia kwenye mazingira ambapo takribani tani za taka za plastiki milioni 75 hadi 199 zinaishia baharini.
Kwa nini taka za chupa za rangi haziokotwi?
Kwa mujibu wa Issa, awali chupa za plastiki za rangi zilikuwa zikinunuliwa lakini baadaye zikawa hazichukuliwi tena kutokana na baadhi ya waokota chupa kujaza mchanga kwenye chupa hizo ili kuongeza uzito na kupata hela nyingi.
Mfanyabiashara ya kununua taka ikiwemo chupa za plastiki jijini Dar es Salaam, Livan William anasema kuwa wamekuwa hawazinunui chupa za rangi kwa sababu hazipokelewi katika viwanda vya urejelezi ambavyo wamekuwa wakipeleka.
William anasema kuwa wanaochakata chupa za plastiki huwaambia kuwa kuna mchakato wa uzalishaji unaofanyika kiwandani ambao hauitaji chupa hizo.
“Chupa hizi zina changamoto na sisi wafanyabiashara wengi hatuzinunui kwa sababu tukipeleka kiwandani hawanunui kutokana na mchakato wao hauruhusu chupa hizo,’’ anasema William.
Wamiliki wa viwanda vya urejelezaji wa chupa za plastiki wanaeleza kuwa inahitajika teknolojia ya kisasa kzitenganisha chupa za rangi na angavu ambapo kwa Tanzania, teknolojia hiyo bado haijaanza kutumika.
Meneja wa kampuni ya udhibiti taka na urejelezaji (recycling) ya The Recycler Limited, Philipo Steven anasema kuwa uwepo wa teknolojia ndogo unachangia changamoto katika kuchakata chupa hizo katika urejelezaji.
‘’Sio tu chupa hizi za rangi lakini pia kuna aina ya karatasi hapa nchini tunahangaika nazo hazina ufumbuzi kwa sababu hatuna teknolojia inayotosha kuingiza takataka hizi katika mchakato unaoweza kuzalisha bidhaa nyingine”, anasema Philipo.
Zinazohusiana:
-
Mjue Mkunga samaki ambaye yupo hatarini kutoweka
-
Kutana na vijana wanaoipa thamani nyumba yako kwa ‘taka
- Biashara ya hewa ukaa inavyoweza kuokoa mazingira Tanzania
Nini kifanyike?
Kutokana na athari za chupa za plastiki kwenye mazingira, ni dhahiri kuwa juhudi zinahitajika ili kupunguza chupa za plastiki za rangi mitaani kama ilivyofanyika kwenye chupa angavu ambazo hutumika kuhifadhia maji ya kunywa.
Waokotaji chupa za plastiki wameomba kampuni zinazotengeneza chupa hizo kuzibadilisha rangi ili waweze kuziokota na kujipatia kipato, vilevile kupunguza uchafuzi wa mazingira.
Wadau wa mazingira wanashauri kuwa ni vyema kwa makampuni husika kuanzisha mfumo wa kuzikusanya chupa za rangi baada ya kuzitumia ili zitumike tena.
‘’Wanaweza kuwa na sera kuwa mtu akiwaletea chupa hizi wanazinunua, kwahiyo wale watu wangeweza kuzibeba na kuwapelekea,” anasema Philipo.
Licha ya kuwa chupa za plastiki za rangi zinawezwa kurejelezwa kwa teknolojia ya kisasa, waokotaji na wanunuzi wamekuwa wakizikwepa kwa sababu hazipokelewi viwandani. Picha| Suleman Mwiru.
Aidha Serikali imesema kuwa wazalishaji wa vinywaji vinavyohifadhiwa kwenye chupa za plastiki za rangi, wanaweza kuendelea kuzalisha chupa hizo ila wahakikishe kuwa wana mfumo mzuri utakaosadia chupa hizo kufanyiwa urejelezaji.
‘’Niwaelekeze wenye viwanda vyote kama tunavyoona hivi sasa waendelee kuzitumia chupa hizi katika vinywaji vyao…wahakikishe wanafanya kama hivi tunavyoona kwamba hizi chupa zinazalishwa lakini zinarudishwa katika matumizi mengine,” anaagiza Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Selemani Jafo.
Endapo wazalishaji wa chupa za plastiki za rangi watatekeleza maagizo ya Serikali na wenye viwanda vya urejelezaji chupa za plastiki kutumia teknolojia ya kisasa itasaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na chupa hizo.
Benki ya Dunia katika ripoti yake ya Usimamizi wa Taka ya mwaka 2018 inaeleza kuwa wakusanyaji taka wasaidiwe na kupangwa ili kuwa sehemu ya mnyororo wa urejelezaji utakaosaidia kutengeneza ajira na kupunguza athari za uharibifu wa mazingira.
Pia imeshauri elimu itolewe kwa watu kuhusu madhara ya chupa za plastiki kwa mazingira ili kuongeza uwajibikaji wa pamoja katika kudhibiti taka ngumu hasa katika miji mikubwa duniani.
Latest
