Kikosi kazi: Mchakato katiba mpya uanze baada ya uchaguzi mkuu 2025
Wajumbe wa Kikosi Kazi cha kuratibu Maoni ya Wadau wa Demokrasia ya Vyama vingi vya Siasa wakimsikiliza Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan alipokua akizungumza nao mara baada ya kupokea Taarifa yao Ikulu Jijini Dar es Salaam leo Machi 21, 2022. Picha| Ikulu.
- Ni Kikosi Kazi cha Kuratibu Maoni ya Wadau wa Demokrasia ya Vyama Vingi vya Siasa.
- Chasema hakuna muda wa kutosha ndani ya kalenda ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
- Rais Samia asema kiendelee kuratibu na kije na mapendekezo ya kina.
Dar es Salaam. Kikosi Kazi cha Kuratibu Maoni ya Wadau wa Demokrasia ya Vyama Vingi Vya Siasa kimependekeza mchakato wa Katiba Mpya uanze baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 huku Rais Samia Suluhu Hassan akiridhia kuwa mchakato huo uwe kwenye mpango wa muda mrefu.
Mwenyekiti wa kikosi kazi hicho, Profesa Rwekaza Mukandala ameeleza leo Machi 21, 2022 Ikulu jijini Dar es Salaam kuwa mapendekezo yao yametokana na sababu kuu nne ikiwemo kukosekana kwa muda wa kutosha ndani ya kalenda ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Prof Mukandala amesema kuna haja ya kuanisha Dira ya Mpya ya Maendeleo ya mwaka 2063 kwanza, ambayo ni muhimu katika kutoa mwelekeo wa katiba mpya.
Amesema pendekezo hilo pia limezingatia umuhimu wa kutoa fursa kwa marekebisho ya sheria ya uchaguzi na sheria ya vyama vya siasa ambapo kwa sasa, Serikali na wadau wameanza mchakato wa kutengeneza kanuni zitakazosimamia mikutano ya vyama vya siasa.
“Mwisho kuna haja ya kutoa fursa ya kutosha kufanyia kazi masuala ya muda wa kati ikiwa ni pamoja na kuanisha dira mpya ya Maendeleo,” amesema Prof Mukandala.
Kikosi kazi hicho kinajumuisha wajumbe 24 kutoka makundi mbalimbali kwenye jamii wakiwemo wawakilishi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini na wasomi.
Kumekuwa na maoni tofauti juu ya upatikanaji wa katiba mpya huku baadhi ya watu wakipendekeza mchakato huo uanzie ilipoishia rasimu ya Jaji Joseph Warioba na wengine wakishauri uanze upya.
Wadau wengine kikiwemo Chama cha ACT-Wazalendo kimeshauri kuundwa kwanza tume huru ya uchaguzi itakayohakikisha kunakuwa na uchaguzi huru na wa haki kisha suala la katiba mpya lifuate.
Mtazamo huo wa ACT-Wazalendo umekuwa ukikosolewa na baadhi ya vyama kikiwemo cha kikuu cha upinzani cha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Soma zaidi:
Katika hotuba yake, Rais Samia amesema anakubaliana na kikosi kazi hicho kuwa suala la katiba mpya liwe kwenye mpango wa muda mrefu.
“Kwanza tukayafanyie kazi maboresho yote haya tuliyoyasema, tuyafanyie kazi kipindi hiki cha muda wa kati halafu huko mbele tuone je kuna haja ya kurekebisha katiba yetu?
Pengine kutakuwa na haja si kwa kuandika mpya (bali) kurekebisha baadhi ya maeneo na hata kama tutaandika mpya lakini kazi kubwa imeshafanywa kwenye maboresho haya ambayo tumeyafanya. Kule ni kwenda kuingiza tu kwenye ile katiba,” amesema Rais Samia.
Juma lililopita Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliwaambia wanahabari jijini Dar es Salaam kuwa chama hicho kitaendelea na ajenda yao ya katiba na tume huru ya uchaguzi kama ilivyokuwa awali.