Kikosi kazi chapendekeza utendaji wa tume ya uchaguzi kuhojiwa mahakamani

October 21, 2022 10:38 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Hatua hiyo itaongeza uwajibikaji wa watendaji wake.
  • Chapendekeza wajumbe wa tume kuteuliwa na kamati maalum. 

Dar es Salaam. Kikosi Kazi cha Kuratibu Maoni ya Wadau wa Demokrasia ya Vyama Vingi vya Siasa nchini Tanzania, kimependekeza mambo mbalimbali yatakayosaidia kuboresha utendaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ikiwemo wajumbe wake kuteuliwa na kamati maalum.

Mwenyekiti wa kikosi kazi hicho, Profesa Rwekaza Mukandala ametoa mapendekezo hayo leo, Oktoba 21, 2022 Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akiwasilisha mapendekezo ya kikosi hicho kwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema baada ya kikosi hicho kufanya kazi kwa miezi 10 kikichambua maoni mbalimbali ya wadau, kinapendekeza kuwa NEC iwe huru pasipo kufuata amri au maagizo ya mtu yoyote, idara yoyote ya Serikali, maoni ya chama chochote cha siasa, taasisi  au asasi yoyote nchini.

Hata hivyo, Prof Mukandala amependekeza kuwa utendaji wa NEC  kuhojiwa na mahakama ya juu ili kuhakikisha kunakuwa  na uwajibikaji kwa wajumbe wake.

“Utendaji wa tume uruhusiwe kuhojiwa kwenye mahakama ya juu pale itakapoanzishwa ili kuongeza uwajibikaji wake,” amesema Mukandala.

Rais Samia Suluhu Hassan akipokea Ripoti ya Kikosi Kazi kuhusu Uratibu maoni ya wadau wa Demokrasia ya Vyama vingi vya Siasa kutoka kwa Mwenyekiti wa Kikosi Kazi hicho Profesa Rwekaza Mukandala, Ikulu Jijini Dar es Salaam Oktoba 21, 2022. Picha| Ikulu.

Uteuzi wa Tume ya Taifa ya uchaguzi 

Kikosi kazi hicho kimependekeza uwepo wa kamati ya uteuzi wa wajumbe wa NEC itakayoundwa na wajumbe kutoka Tanzania bara na Zanzibar.

“Kuwe na kamati ya Tume ya taifa ya Uchaguzi itakayokuwa na wajumbe wafuatao: Jaji Mkuu wa Tanzania ambaye atakuwa ni mwenyekiti, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kutoka Tanzania Bara na Zanzibar,” amesema Mukandala.

Wajumbe wengine waliopendekezwa kwenye kamati hiyo ni pamoja na  Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu, wajumbe wawili watakaoteuliwa na Jaji Mkuu wa Tanzania baada ya kupendekezwa na chama cha wanasheria  kutoka Tanganyika na Zanzibar.

“Angalau wajumbe wawili  wa kamati ya uteuzi wawe wanawake,” ameongeza Mukandala.

Kwa sasa, Rais ndiye mwenye mamlaka ya kuteua wajumbe wa tume.Ili kuwezesha uwajibikaji wa tume, kimependekeza uhuru wa kugombea nafasi ya wajumbe kwa Mtanzania yoyote mwenye nia.

Mukandala amesema sifa za nafasi ya mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa tume zianishwe kisha kamati ifanye usaili kwa walio wasilisha maombi ya kutaka kuwa wajumbe na kupeleka majina kwa Rais ili yapendekezwe.

“Rais atachagua majina ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi miongoni mwa majina yaliyowasilishwa kwake na kamati ya uchaguzi,” amesema Mukandala.

Matokeo ya uchaguzi wa Rais yahojiwe mahakamani

kikosi kazi hicho kimependekeza matokeo ya uchaguzi wa Rais yahojiwe kwenye mahakama ya juu itakapoanzishwa.

“Kwa kifupi ni kwamba tumeyapokea na tutayafanyia kazi. Lakini ni muhimu wananchi wakaelewa kwamba maoni ya kikosi kazi sio amri kwa serikali kwamba ni lazima tukafanya kama ambavyo kikosi kazi kimesema,” amesema Rais Samia Suluhu Hassan. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW