Vitalu vya miche vitakavyoongeza kasi ya upandaji miti
Naibu wazir wa Utalii, Mary Masanja akipokea moja ya mti uliooteshwa na mwananchi wilayani Magu kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya upandaji miti kitaifa yaliyofanyika wilayani Magu. Picha|Mariam John.
- Halmashauri zaagizwa kuanzisha vitalu vya miche.
- Hatua hiyo itasaidia kuongeza kasi ya upandaji miti.
Mwanza. Serikali imeziagiza Halmashauri zote nchini kushirikiana na Mfuko wa Misitu Tanzania (Tafu) kuanzisha vitalu vya kuoteshea miche ya miti itakayotolewa kwa wananchi kwa ajili kupanda ili kuhifadhi mazingira.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Utalii, Marry Masanja kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Upandaji Miti ambapo kitaifa imefanyikia katika shule ya msingi Sangani wilayani Magu katika Mkoa wa Mwanza.
Naibu Waziri Masanja ameitaja wilaya ya Magu kuwa miongoni mwa wilaya zinazonyemelewa na ukame hali inayosababisha kuwepo kwa majanga mengi ikiwemo ukosefu wa mvua na uwepo wa mvua zisizotabirika pamoja na upungufu wa kuni na mkaa wa kupikia.
Ameitaja wilaya hiyo kuwa moja ya wilaya ambayo miti yake imekatwa na hakuna jawahi kufanyika juhudi za kuhifadhi mazingira yasiharibiwe zaidi.
“Kwakuwa uhitaji wa miche si Magu pekee kuna haja ya kila halmashauri nchini kuanzisha bustani ndogo ndogo katika ngazi za kata na tarafa ili iwe rahisi kwa wananchi waishio vijijini kupata miche hiyo kirahisi na kwenda kuipanda,” amesema Masanja.
Kwa mjibu wa Masanja, ni vema wakurugenzi kuanza kufanya upembuzi yakinifu na kutenga bajeti kwa ajili ya kuanzisha bustani hizo lakini kuainisha maeneo ya upandaji miti yanayofaa ya umma au binafsi.
Pia Naibu Waziri huyo amesisitizia watendaji kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi ya umuhimu wa kupanda miti na kuitunza na kwamba wasipitishe mifugo kwenye maeneo hayo.
Awali, Mbunge wa Jimbo la Magu Desderia Kiswaga alikiri wilaya hiyo kukumbwa na ukame kutokana na ukosefu wa miti na kuwaomba wananchi wilayani humo kuwa na desturi ya kupanda miti walau minne mbele ya nyumba zao au kwenye mipaka ya mashamba yao.
“Leo Magu ni ukame kwa sababu miti yote imefyekwa hali inayosababisha kukosekana kwa mvua, maji ya visima kukauka, ukosefu wa kuni za kupikia, hivyo ni vyema tukajenga utamaduni wa kulinda na kutunza mazingira kwa kupanda miti,” amesema Kiswaga.
Kauli ya Mbunge huyo haipishani na wakazi wa wilaya hiyo ambao walikiri kukosekana kwa mvua katika misimu mingi iliyopita na chanzo kikubwa ikiwa ni ukosefu wa miti.
Mwenyekiti wa kijiji cha Sangani, Juma Kabadi amesema kukosekana kwa mvua kumesababisha watu kukata miti ya asili ovyo.
“Serikali imetukumbuka kwa kutuletea miti ambayo tutahakikisha tunaitunza ili kulinda na kutunza mazingira na kujiepusha na majanga yanayoweza kutokea,” amesema Kabadi.
Hatahivyo, Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kali amesema toka uhamasishaji wa zoezi la upandaji miti kwa wananchi lianze mwaka huu, mkoa wa Mwanza umefanikiwa kupanda miche ya aina mmbalimbali zaidi ya milioni 3.2.
Amebainisha changamoto zinazowakumba ni wafugaji wa ng’ombe kulisha miti hiyo lakini pia wananchi kutokuwa na elimu ya kutosha ya utunzaji wa mazingira.
“Na leo kwenye kilele cha upandaji miti mkoa wa Mwanza umefanikiwa kupanda miti zaidi ya 6,000 na zoezi hili litakuwa endelevu,” amesema Kali.