WHO kuanzisha kituo cha kimataifa cha tiba asilia

March 26, 2022 6:40 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Kitazinduliwa Aprili 2022 nchini India.
  • Kitatumika kufanya tafiti za dawa asilia dunia ili kuboresha maisha ya watu.
  • Kitasaidia kuingiza dawa asilia katika mifumo ya afya kwa utaratibu maalum.

Dar es Salaam. Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) na Serikali ya India leo wametia saini makubaliano ya kuanzisha Kituo cha Kimataifa cha Tiba Asilia (WHO-GCTM) kitakachosaidia kuboresha afya za watu duniani.

Kituo hicho cha maarifa cha kimataifa cha tiba asili kinachofadhiliwa na uwekezaji wa Dola za Marekani milioni 250 (Sh579.7 bilioni) kutoka Serikali ya India ambapo kinalenga kutumia uwezo wa dawa asilia kutoka kote ulimwenguni kupitia sayansi na teknolojia ya kisasa.

WHO katika taarifa iliyotolewa Machi 25, 2022 mjini Geneva, Uswisi imesema karibu asilimia 80 ya watu duniani wanakadiriwa kutumia dawa za jadi. 

Hadi sasa, mataifa 170 kati ya 194 wanachama wa WHO yameripoti matumizi ya dawa za jadi, na serikali zao zimeomba msaada wa WHO katika kuunda ushahidi wa kuaminika na data juu ya matumizi ya dawa hizo na bidhaa zake. 

“Kwa mamilioni ya watu duniani kote, dawa za jadi ni kimbilio la kwanza la kutibu magonjwa mengi,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Ghebreyesus. 

“Kuhakikisha watu wote wanapata matibabu salama na yenye ufanisi ni sehemu muhimu ya dhamira ya WHO, na kituo hiki kipya kitasaidia kutumia nguvu za sayansi ili kuimarisha msingi wa ushahidi wa tiba asilia.”

Tiba asilia inajumuisha maarifa, ujuzi na desturi ambazo tamaduni asilia na tamaduni mbalimbali zimetumiwa kwa muda mrefu kudumisha afya na kuzuia, kutambua na kutibu magonjwa ya kimwili na kiakili.  

WHO imesem dawa asilia pia zinazidi kuwa maarufu katika ulimwengu huu wa sayansi na teknolojia.


Soma zaidi: 


Asilimia 40 ya dawa zilizoidhinishwa zinazotumika leo zinatokana na vitu asilia, jambo linaloangazia umuhimu wa kuhifadhi bayoanuwai na uendelevu, imeeleza WHO.

Mathalan, ugunduzi wa aspirini ulitokana na michanganyiko ya dawa za kitamaduni kwa kutumia gome la mti wa mlonge, kidonge cha kuzuia mimba kilitengenezwa kutoka kwenye mizizi ya viazi vikuu vya mwitu na matibabu ya saratani ya watoto yametokana na maua ya ‘rosy periwinkle’. 

Utafiti ulioshinda tuzo ya Nobel kuhusu dawa ya “artemisinin” kwa ajili ya kudhibiti malaria ulianza na mapitio ya maandishi ya kale ya dawa za Kichina. 

Kituo kipya cha WHO kitaanzishwa Jamnagar, Gujarat, India. Ingawa Jamnagar itatumika kama kitovu, kituo kipya kinaundwa ili kuhusisha na kunufaisha maeneo yote duniani. 

Kituo hiki kitalenga kujenga msingi wa ushahidi thabiti wa sera na viwango vya utendakazi na bidhaa za dawa asilia na kusaidia nchi kujumuisha inavyofaa katika mifumo yao ya afya na kudhibiti ubora na usalama wake kwa athari bora na endelevu. 

Kituo kipya kinazingatia maeneo makuu manne ya kimkakati: ushahidi na kujifunza; data na uchambuzi; uendelevu na usawa; na uvumbuzi na teknolojia ili kuongeza mchango wa tiba asilia kwa afya ya kimataifa na maendeleo endelevu. 

Uzinduzi wa kituo hicho kipya cha kimataifa cha WHO cha dawa za jadi huko Jamnagar, Gujarat, India utafanyika Aprili 21, 2022. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW