Simulizi ya mcheza ngoma aliyeng’atwa na nyoka zaidi ya mara 10

April 6, 2022 5:35 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni Thobias Gwende, mwalimu na mcheza ngoma za asili Mwanza.
  • Anatumia dawa asili kuondoa sumu ya nyoka mwilini.
  • Ataja mambo ya kuzingatia ili usidhurike na nyoka wakati wa kucheza naye.

Mwanza. Ni mwalimu maarufu na mashuhuri wa ngoma na muziki wa asili. Ana uwezo kucheza karibu kila ng’oma ya makabila mbalimbali Tanzania.

Licha ya umahiri wake wa kucheza na kufundisha jinsi ya kucheza ngoma, ni mtaalam pia wa kucheza na nyoka katika shughuli mbalimbali za kijamii yakiwemo matamasha ya utamaduni. 

Hivyo ndivyo unavyoweza kumtambulisha, Thobias Gwende, mkazi wa jijini Mwanza ambaye ni nguzo muhimu ya kuendeleza utamaduni wa Kitanzania.

Pamoja na umaarufu wake wa kucheza ngoma za asili hasa Kanda ya Ziwa, Gwende (42) amewahi kung’atwa na nyoka zaidi ya mara 10 katika nyakati tofauti wakati akitoa burudani hiyo kwa watu. 

Gwende ambaye anapendelea zaidi kucheza ngoma aina ya Bucheyeye na Bugobogobo za kabila la Wasukuma anasema matukio hayo ni ajali za kawaida ambazo alizapata wakati akitimiza majukumu yake.

“Hadi sasa, nina alama za vidonda vya kung’atwa na nyoka sehemu mbalimbali za mwili wangu kwa zaidi ya mara 10,” anasema Gwende ambaye alianza kucheza ngoma zinazohusisha nyoka mwaka 1999.

Kisa cha kwanza cha kung’atwa na nyoka wake aliyekuwa mpole na rafiki yake kilikuwa mwaka 2002 katika moja ya tamasha la ngoma mkoani hapa.

Gwende akiwa katika moja ya shughuli ya kucheza na nyoka. Licha ya kuwa mwalimu wa kufundisha jinsi ya kucheza na nyoka, amekuwa aking’atwa na nyoka anaocheza nao. Picha| Thobias Gwende.

Kilichofanya ang’atwe ni kuwa alikosea kumshika nyoka aina ya chatu wakati wa kucheza na hivyo kumshambulia mkononi.  

“Nilikosea kumshika badala ya kumshika kichwani nilimshika shingoni ambapo alijikunja na kufanikiwa kuning’ata kwenye mkono,” anasema mwalimu huyo wa ngoma za asili ambaye ni nadra kumkosa katika matukio makubwa ya utamaduni na sanaa.

Gwende anawakilisha changamoto wanazopitia watu wanaocheza na nyoka ambao hukutana na madhira mbalimbali ikiwemo vifo vinavyotokana na kucheza na nyoka.

Anasema tangu wakati huo, amekuwa makini wakati akicheza na nyoka lakini amekuwa akishambuliwa na nyoka anaocheza nao. 

“Tabia za nyoka huwa zinabadilika, kuna siku anaweza kuwa mpole siku nyingine anakufanyia tukio lolote,” anasema Gwende na kuongeza kuwa akiona hivyo hujihami mapema ili asiharibu burudani mbele za watu.

Mambo mengine yaliyochangia kijana huyo ang’atwe na nyoka ni kukidhi matakwa ya watu wanaohudhuria burudani ya ngoma ambao wamekuwa wakiomba kuonyeshwa namna nyoka anavyong’ata na kutoa sumu mdomoni.

“Hilo nalo linachangia inabidi umbane nyoka ili afanye unavyotaka,” anasema Gwende na kubainisha kuwa hilo nalo limekuwa likisababishwa ashambuliwe na nyoka mwilini na kupata majeraha madogo madogo yasiyo na madhara makubwa.


Soma zaidi: 


Licha ya kung’atwa na nyoka zaidi ya mara 10, anasema majeraha ambayo ameyapata siyo ya kumsababishia kifo au ulemavu na amekuwa akitumia dawa za asili ili kuondoa sumu mwilini na kujihami endapo nyoka atamng’ata.

“”Nyoka anapokung’ata hutakiwi kumtoa mwache hadi amwage sumu yake na baada ya kumwaga sumu yake hudondoka sasa kinachofanyika wachezaji wote wa ngoma  wa nadawa za kutoa sumu,  dawa hiyo ikishawekwa ndani ya dakika 15 maumivu na sumu yote inakuwa imetoka mwilini na unaweza kuendelea na shughuli zako,” anasema Gwende.

Hata hivyo, inashauri kuwa unapong’atwa na nyoka ni muhimu kuwahi kufika katika kituo cha afya ili kupata matibabu ya haraka kabla sumu ya nyoka haijaleta madhara mwilini.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kung’atwa na nyoka mwenye sumu kali kunaweza kusababisha kupooza ambako kunaweza kumzuia mtu kupumua, kumsababishia maradhi ya kutokwa na damu, matatizo ya figo yasiyoweza kutibika na kuharibu mishipa ambayo inapelekea ulemavu wa maisha na kukatwa viungo. 

Shirika hilo limeongeza kuwa kung’atwa na nyoka ni moja ya magonjwa yaliyopuuzwa (NTDs)  ambayo athari zake ni kubwa na mbaya kuliko inavyodhaniwa.  

Waathirika wakubwa ni watu wanaofanya kazi katika sekta ya kilimo na watoto huku maeneo yaliyoathirika na kuwa hatarini zaidi ni Afrika, Asia na Amerika ya Kusini hasa vijijini.

WHO imesema ili kupunguza idadi ya vifo na ulemavu utokanao na kung’atwa na nyoka ni muhimu kuziwezesha na kuzishirikisha jamii, kuhakikisha kuna matibabu salama na yenye ufanisi, kuimarisha mifumo ya afya na kuongeza ushirika, uratibu na rasilimali za kupambana na zahma hizo.

Licha ya mwalimu huyo wa ngoma kukumbuna na matukio ya kung’atwa a nyoka, pia amekuwa akishuhudia wenzake wengine wakidhurika na mnyama huyo wakiwa katika shughuli zao.

Gwende anasema kucheza ngoma na nyoka ni kazi kama kazi zingine ambayo anaitegemea kwa muda mrefu kumuingizia kipato cha kutunza familia na kuendesha maisha yake binafsi. 

Kwa sasa Gwende anaongoza kikundi cha ngoma cha Buyeye ambacho kimekuwa kikitoa burudani za nyimbo na ngoma katika shughuli mbalimbali.

Unataka kufahamu kwanini nyoka hutumiwa kwenye ngoma? Nini cha kuzingatia wakati wa kucheza na nyoka ili usidhurike? Nyoka anatunzwaje? Kufahamu hayo na mengine ungana nasi katika makala inayofuata hapo kesho.

Enable Notifications OK No thanks