Nyota ya amani inapogeuka mtego kwa watafutaji
- Ni simulizi ya binti Fiona katika filamu ya Filamu ya “The Princess Switch”.
- Anapewa kibarua kuitafuta nyota ya amani ili awe huru.
Dar es Salaam. Wanasema muda una uwezo wa kumbadilisha mtu. Wengine wameenda mbele zaidi na kusema ya kuwa, muda huo huo una uwezo wa kumbadilisha muovu kuwa mwema kama malaika.
Huenda usemi huo ukawa ni kweli kwa mwanadada Fiona Pembroke ambaye awali alikuwa mbinafsi, muovu na asiye na punje ya nia njema.
Kabla ya kwenda mbele zaidi, nianze kwa kukuweka sawa kuwa hiki ni kisa kilichopo katika filamu ya “The Princess Switch”. Filamu hii ni muendelezo wa filamu mbili zilizopita. “The Princess Switch” I&II na sasa nisehemu ya tatu.
Ili uelewe kinachoendelea, filamu hii ilianza na binti wa kawaida aliyekuwa na duka la kuuza keki, Stacy DeNovo ambaye maisha yalimkutanisha na binti mfalme, Lady Margaret Delacourt ambaye alitamani maisha ya kawaida walau kwa siku moja tu kwani maisha ya ufalme yalikuwa yamemchosha.
Baada ya wawili hao kukutana, Margaret alimshawishi kubadilishana maisha na Staicy kwa muda. Yote hayo yaliwezekana kwa sababu wawili hao walifanana kwa kila kitu. Wakiwa kwenye maisha mapya, Staicy alidondoka kwa mpenzi wa Margaret, Mwana Mfalme Prince Edward huku Margareth akidondoka kwa huba na rafiki wa karibu wa Staicy, Kevin.
Maisha yaliendelea na ikabidi hata baada ya mabinti hao kurudishiana nafasi zao, Margaret abaki na Kevin huku muokaji Stacy akiingia kwenye maisha ya kifalme kwa kuwa mke wa Prince Edward.
Sehemu ya pili tunakutana na binamu yake na Margaret, Lady Fiona Pembroke ambaye alitaka kufanya mapinduzi kwa binamu yake ili achukue kiti kama Malkia wa ardhi ya Montenaro lakini hakufanikiwa na hivyo kupata adhabu ya kifungo cha nje.
Sasa turejee kwenye sehemu ya tatu
Ni msimu wa sikukuu na Malkia Margaret pamoja na Binti Mfalme Stacy Wyndham wanaandaa sherehe ya Krismasi ya kimataifa huku uongozi mkuu wa Kanisa Katoriki huko Vatican ukiwakabidhi “Nyota ya Amani”, (Star of Peace) ambayo kwenye filamu hiyo inaaminika ilimilikiwa na Mtakatifu Nicholas.
Hata hivyo, mara baada ya nyota hiyo kufikishwa kwenye ardhi ya Montenaro, inaibiwa na watu wasiojulikana.
Malkia na binti mfalme pamoja na familia nzima wanakubaliana kutouambia uongozi wa Vatican kwanza hadi juhudi za kuipata zishindikane.
Margaret hajui chochote kuhusu wizi na hivyo hivyo Stacy. Tena, hata waume zao wote hawana rekodi zozote za uhalifu hivyo anayebaki kama msaada ni mmoja tu, binamu yake na Margaret, Lady Fiona Pembroke.
Kwa kuanza, wazo la kumuamini Fiona kwenye misheni hiyo linapingwa na kila mtu katika meza majadiliano lakini wote wanaishia kukubali kuwa ndiyo msaada pekee hivyo hamna namna bali Fiona aletwe mezani.
Baada ya kuombewa ruhusa na Malkia, Pemborke anaruhusiwa kwenda kula sikukuu nje ya kifungo chake huku lengo likiwa ni atumie muda huo kutafuta nyota hiyo. Fiona anakubali na ili kazi hiyo iende sawa, anaomba kumwingiza Ex wake kwenye timu. Ni Peter Maxwell.
Siyo Peter tuu, Fiona anaomba wasaidizi wake wawili, Reggie na Mindy wawe kwenye timu hiyo.
Safari ya kuitafuta nyota ya amani inaanza na inagundulika kuwa nyota hiyo ipo kwenye mikono ya Ex mwingine wa Fiona ambaye ni Hunter Cunard.
Inakuwa kazi rahisi kwani Hunter bado anahisia na Fiona na anapomuona tu, anamwalika kwenye “party” ambayo itafanyika siku chache kabla ya Krismasi jambo ambalo ni taa ya kijani kwa Fiona na timu yake kuingia kwenye hekalu la Hunter.
Soma zaidi
- Zawadi pendwa kwa “mshua” msimu wa sikukuu
- Njia sahihi za kusafisha jiko la umeme
- Zifahamu aina za kamera na matumizi yake
Wito wa kubadilishana nafasi
Mazoezi ya kunyata, sarakasi na kushuka kamba ili kupita nyenzo za ulinzi za hekalu la Hunter yanaanza na mazoezi hayo yanabainisha ya kuwa Fiona inabidi aungane na timu ya wizi hivyo inahitaji mtu mwingine aingie kama Fiona kwenye party aliyoalikwa.
Kwa kuwa kuna sura tatu zinazofanana takriban kila kitu, inabidi malkia Margaret achukue nafasi ya kuingia kwenye sherehe kama Fiona ili Fiona akamilishe misheni ya kuiiba nyota ya amani akisaidiana na Peter, Reggie na Mindy.
Stacy akiwa amebaki kukaimu nafasi ya Malkia, anapokea simu ya kuwa Fiona anahitajika mara moja kurudi alipokuwa akitumikia kifungo chake tena bila kukosa kwani kamati ya nidhamu nayo imewasili kusikiliza mashtaka yake. Njia pekee iliyobaki ni Staicy kuwa Fiona.
Haya sasa. Margaret ni Fiona, na Staicy naye ni Fiona na Fiona mwenyewe pia ni Fiona vile vile. Tuna Fiona watatu hivyo ombi ni kuwa kila kitu kiende sawa.
Baada ya kashi kashi kuisha, na wizi wa nyota kufanikiwa, Margaret na Staicy wanamgojea Fiona arudi na nyota ya amani aliyoiiba.
Loooh! Wote wanabaki mdomo wazi pale begi alilobeba Fiona akidhani amebeba nyota ya amani lina mpira wa kikapu ndani na nyota ya amani haipo.
Nyota ipo wapi? Nani amewachezea mchezo?, wapo tayari kueleza ukweli kwa uongozi wa Vatican ya kuwa nyota ya Mtakatifu Nicholas imeibiwa?
Fuatilia filamu hii kupitia Netflix au popote unapotazama filamu zako.