Maoni mchanganyiko kupanda nauli za mabasi, daladala Tanzania

May 2, 2022 3:53 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Latra yatangaza kupanda kwa nauli zitakazoanza kutumika baada ya siku 14.
  • Madereva, wamiliki wa mabasi, daladal kicheko.
  • Wananchi wasema nauil hizo zitawaongezea ugumu wa maisha.

Dar es Salaam.  Muda mfupi baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) kutangaza nauli mpya za mabasi ya mijini maarufu daladala na mabasi ya masafa marefu, Watanzania wametoa maoni yao kuhusu nauli hizo mpya huku baadhi wakisema zinaenda kuzidisha ukali wa maisha kwa mwananchi wa kawaida.

Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Gilliard Ngewe akitangaza nauli mpya leo Aprili 30, 2022 amesema nauli hizo mpya zitaanza kutumika baada ya siku 14.

Amesema kwa mabasi ya mjini kuanzia kilomita 0 hadi 10 nauli itakuwa Sh500 badala ya 400 na nauli ya Sh450 itakuwa ni 550.

Ina maana kuwa kwa watu wanaotoka kituo cha Makumbusho kwenda Posta au Kariakoo jijini Dar es Salaam watalipa Sh500. 

“Kwa kilomita 30 nauli itakuwa 850 badala ya 750 na kwa kiliometa 35 nauli itakuwa 1,000 na kwa huku kwa upande wa kilometa 40 nauli itakuwa 1,100,” amesema Ngewe.

Amesema kwa hesabu hizo za usafiri wa mjini, nauli wanayotozwa wanafunzi haijabadilika ambapo itaendelea kuwa Sh200.

Akizungumzia nauli za mabasi ya mkoani, amesema daraja la kawaida kwa kwa kilometa 1 imeongezeka kwa asilimia 11.9 kutoka Sh36 kwa kilometa moja hadi Sh41.

“Kwa daraja la kawaida mtu anayetoka Dar es Salaam kwenda Arusha alikuwa akilipa Sh22,700, sasa atalipa Sh26,700. Ukienda daraja la kati alikuwa akilipa Sh32,800, sasa alipa Sh36,700,” amesema Ngewe akisema hiyo ni nauli kwa mtu anayepitia Chalinze na kuongeza kuwa,

“Kwa daraja la kati imeongezeka kwa asilimia 6 abiria mmoja atalipa Sh56.88 kwa kilometa kutoka Sh53.”

Akitolea mfano mwingine, amesema kwa safari ya Dar es Salaam kwenda Mwanza, daraja la kawaida nauli ilikuwa Sh42,600, sasa ni Sh47,200. Daraja la kati, nauli ilikuwa Sh61,400, sasa itakuwa Sh65,100.

Wakizungumza na Nukta Habari, baadhi ya wakazi wa Mwananyamara na Makumbusho jijini Dar es Salaam, wamesema kutangazwa kwa bei mpya za nauli kutazidisha ugumu wa maisha kwa mwananchi wa kawaida.

“Maisha yanazidi kuwa magumu, sisi wananchi ndiyo tunaumia na hizo bei. Bei za vitu zimepanda, sasa wameamua kupandisha na nauli, wametuweza kweli,” amesema Ahmed Juma, mkazi wa Mtaa wa Mchangani.

Mkazi mwingine wa Makumbusho, John Kimweri amesema amepokea kwa masikitiko makubwa tangazo la Latra kwa sababu linaenda kuongeza bajeti yake ya usafiri ambayo haikuwepo katika mahesabu yake.

“Hii siyo sawa kwa kweli, bidhaa zote zinapanda, maisha yanazidi kuwa magumu, hakuna ahueni. Tunaoimba Serikali itutazame raia wake na itupunguzie ugumu wa maisha,” amesema Kimweri.

Wakati baadhi wakilalamika kuhusu bei hizo mpya, kwa madereva wa daladala leo watalala na tabasamu kwa sababu hesabu zao zitaanza kusoma vizuri kwa mabosi wao.

Kondakta wa daladala inayofanya safari zake kutoka Makumbusho kwenda Buza, Eliakimu Kidawa amesema sasa watapata ahueni na faida wataiona kwenye biashara ya daladala.

“Kaka, mafuta yamepanda bei, sasa kwa nini nauli zisipande? Hii ni furaha kwetu maana wengine tulitaka tuache kabisa hii kazi kwa sababu ilikua hailipi,” anasema Kidawa wakati akishusha abiria katika kituo cha Mwananyamala Sokoni.


Zinazohusiana: 


Hata hivyo, baadhi ya madereva wamesema bado viwango vipya vilivyotangazwa havitakuwa na matokeo mazuri katika kipato wanachopata kwa siku kwa sababu ongezeko lake siyo kubwa kama walivyotarajia.

Dereva wa daladala, Emmanuel Mbutiro amesema, “ kweli zimepanda lakini naona zilitakiwa zipande zaidi ya hapo kwa sababu gharama za usafiri zimeongezeka sana, hatuna jinsi sasa.”

 

Sababu ya kupanda kwa nauli 

Hivi karibuni wamiliki wa vyombo vya moto na madereva walitoa maoni yao wakitaka wapandishe nauli za magari kwa sababu ya kupanda kwa bei za mafuta.

Baada ya kupitia maoni ya wadau wa usafiri, Latra imekuja na bei kikomo ili kukidhi mahitaji ya wadau hao.

Kwa mujibu wa bei mpya za rejereja zilizotangazwa Aprili 5, 2022 na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) bei petroli jijini Dar es Salaam imepanda hadi kufikia Sh2,861 kwa lita kutoka Sh2,540 iliyokuwa ikitumika Machi 2022 ikiwa ni ongezeko la Sh321. 

Ewura ilieleza kuwa bei mpya kikomo za rejareja za dizeli kwa Aprili 2022 iliyoingizwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam kuanzia Aprili 6 ni Sh2,692 kwa lita ikiwa imepanda kwa Sh289 kutoka Sh2,403 ya sasa.

Mkurugenzi wa Petroli wa Ewura, Gerald Maganga aliwaambia wanahabari jijini Dodoma Aprili 5 kuwa kupanda kwa bei hizo kumesababishwa na kubadilika kwa bei za mafuta katika soko la dunia na kuongezeka kwa gharama za usafirishaji wa mafuta duniani kulikochagizwa na vita ya Urusi na Ukraine.

Kupanda kwa bei za petroli, dizeli na mafuta ya taa kulitegemewa kutokana na vita inayoendelea sasa kati Urusi na Ukraine ambayo imetatiza mifumo ya usafirishaji nishati hizo duniani. Urusi ni mmoja wa wazalishaji wakubwa wa mafuta duniani.

Enable Notifications OK No thanks