Wazazi wawe walimu wa kwanza wa maadili kwa watoto
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk Thomas Rutachunzibwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye maadhimisho ya kupinga matumzi ya dawa za kulevya yaliyofanyika jijini Mwanza. Picha | Mariam John.
- Wataalam wa afya wasema itasaidia kupunguza matumizi ya dawa za kulevya.
- Watoto walioathirika watakiwa kupelekwa kwenye vituo vya afya kwa ajili ya kuanza kiliniki ya matibabu.
Mwanza. Wazazi wametakiwa kushiriki katika malezi ya watoto wao ili waweze kukua katika maadili yatakayosadia kupunguza matumizi ya dawa za kulevya wakiwa wakubwa.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk Thomas Rutachunzibwa amesema wazazi wamekuwa chanzo cha watoto wengi kujiingiza kwenye vitendo viovu vikiwemo matumizi ya sigara na dawa za kulevya.
“Zipo njia zinazochangia watoto wajiingize kwenye matumizi ya dawa za kulevya mojawapo ni pale mzazi anapomtuma mtoto kwenda kumuwashia sigara au kwenda kumnunulia sigara.
“Wakati umri unapoenda kifikra anajua sigara sio jambo mbaya na halina athari hivyo analazimika kuanza kutumia akiwa mdogo na kusababishia athari,” amesema Dk Rutachunzibwa katika maadhimisho ya kupinga matumizi ya dawa za kulevya jijini Mwanza, Julai 1, 2022.
Amesema familia ina mchango mkubwa katika kuhakikisha wanadhibiti vitendo vya matumizi ya dawa hizo kwa watoto wao huku akiwataka wazazi ambao watoto wao tayari wameathirika kuwapeleka kwenye vituo vya afya kwa ajili ya kuanza kiliniki ya matibabu.
Awali Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari wa Kupinga Matumizi ya Dawa za Kulevya (Ojadact), Edwin Soko amesema chama hicho kinatoa elimu kwa jamii iweze kutambua athari zinazotokana na matumizi ya dawa hizo.
Pia wanawasaidia wale walioathirika kupata huduma stahiki ili waweze kurejea katika hali zao za kawaida.
Amesema zipo athari nyingi zinazowakumba watumiaji wa dawa hizo ikiwemo mtumiaji wa dawa hizo anakuwa kwenye hatari ya kuambukizwa ugonjwa wa Ukimwi.
“Pia mtumiaji wa dawa za kulevya anaweza kuathirika kiuchumi kwa kuwa kila fedha atakayoipata badala ya kufanya maendelea ataipeleka kwenye dawa za kulevya halikadhalika mwanafunzi atashindwa kuendelea na shule,” amesema Soko.
Meneja mradi wa Kituo cha Methadone na Mratibu wa afya ya akili kutoka hospitali ya Mkoa wa Mwanza, Sekou-Toure, Dk Eunice Masangu amesema athari za dawa za kulevya zinaweza kuwa za moja kwa moja au zisiwe na kuwa kimwili ni kupata magonjwa kama vile kifua kikuu, homa ya ini A na C na Ukimwi.
Dk Masangu ameainisha athari zingine ni pamoja na kufanya maamuzi yasiyo sahihi, hisia potofu , magonjwa ya akili, sonona na kuchanganyikiwa.