Kicheko, maumivu: Panga pangua wakuu wa mikoa Tanzania
- Wakuu wa mikoa saba watenguliwa akiwemo Ally Hapi wa Mara.
- Rais Samia amrudisha tena Albert Chalamila aliyemtumbua 2021.
- Saba wahamishwa vituo vya kazi huku 10 hawajaguswa.
Dar es Salaam. Huenda siku ya leo itakuwa kicheko na maumivu kwa baadhi ya watu baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kufanya mabadiliko ya wakuu wa mikoa kwa kuwabadilisha vituo na kuwateua wapya tisa akiwemo Albert Chalamila aliyepelekwa Mkoa wa Kagera.
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Zuhura Yunus katika taarifa yake iliyotolewa leo alfajiri Julai 28, 2022 amesema Rais Samia amefanya uteuzi wa wakuu wa mikoa wapya tisa, kuwahamisha vituo vya kazi saba na wengine 10 kubakia kwenye vituo vyao.
Wakuu wa mikoa wapya
Nurdin Hassan Babu ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro. Alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Longido mkoani Arusha na anachukua nafasi ya Dk Steven Kagaigai ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Dk Kigaigai aliwahi kuwa Katibu wa Bunge la Tanzania.
Rais Samia amemteua Fatma Abubakar Mwasa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro akichukua nafasi ya Martin Reuben Shigella. Mwasa aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali miaka ya nyuma ikiwemo ukuu wa wilaya na mkoa.
Halima Omari Dendego ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa huku Dk Raphael Masunga Chegeni akipelekwa Mkoa wa Mara akichukua nafasi ya Ally Hapi ambaye ametenguliwa.
Peter Joseph Serukamba aliyewahi kuwa Mbunge wa Kigoma Mjini ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Singida akichukua nafasi ya Dk. Binilith Mahenge ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Soma zaidi:
Taarifa ya uteuzi huo pia inaonyesha Rais Samia amemteua Kanali Ahmed Abbas Ahmed kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara akichukua nafasi ya Brigedia Jenerali Marco Gaguti. Kanali Ahmed alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani.
Kanali Laban Elias Thomas ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ambapo kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma.
Anachukua nafasi ya Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Huku Albert John Chalamila akiteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera.
Chalamila ambaye Juni 2021 aliondolewa katika nafasi ya Mkuu wa Mkoa Mwanza amerudishwa tena kuwa miongoni mwa watendaji wa Rais Samia akichukua nafasi ya Meja Jenerali Mbuge.
Dk Yahaya Esmail Nawanda ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu. Awali alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Tabora mkoani Tabora na amechukua nafasi ya David Kafulila ambaye amewekwa pembeni.
Waliohamishwa vituo vya kazi
Anthony John Mtaka ambaye awali alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma amehamishwa Mkoa wa Njombe huku Queen Cuthbert Sendiga akipelekwa Mkoa wa Rukwa. Alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa.
Waziri Kindamba aliyekuwa Njombe amehamishiwa Songwe.
Rais Samia amemuhamisha Martin Reuben Shigella kutoka Morogoro kwenda Mkoa wa Geita huku Omary Tebweta Mgumba akitoka Songwe kwenda Mkoa wa Tanga.
Adam Kigoma Malima aliyekuwa Tanga amehamishiwa Mkoa wa Mwanza huku Rosemary Staki Senyamule amepelekwa Dodoma akitokea Mkoa wa Geita.
Tangazo:

Wakuu wa mikoa ambao hawajaguswa
Amos Gabriel Makalla anaendelea kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam huku John Vianney Mongella anabaki Arusha.
Wakati huo huo, Mwanamvua Hoza Mrindoko anaendelea na majukumu yake Mkoa wa Katavi na Mkoa wa Manyara utaendelea kuongozwa na Charles Makongoro Nyerere.
Zainab Rajab Telack anaendelea kuwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi, wakati Mkoa wa Mbeya ukiendelea kuongozwa na Juma Zuberi Homera.
Thobias Emir Andengenye anaendelea kuongoza Mkoa wa Kigoma na Sophia Edward Mjema bado ataendelea kukaa Shinyanga.
“Balozi Batilda Salha Burian anaendelea kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora na Abubakar Mussa Kunenge anaendelea kuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani,” amesema Zuhura katika taarifa yake.
Uapiasho wa wakuu wa mkia walioteuliwa utafanyika Ikulu Chamwino, Dodoma Agosti 1, 2022.
Latest