Waziri Ummy: Homa ya mgunda siyo tishio
- Amesema Serikali imeudhibiti ugonjwa huo ulioibuka mkoani Lindi.
- Haitatoa tena taarifa rasmi kwa umma kuhusu ugonjwa huo.
- Mpaka sasa watu 20 wameugua ugonjwa huo, 3 wakifariki dunia.
Dar es Salaam. Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema ugonjwa wa homa ya Mgunda ulioripotiwa hivi karibuni mkoani Lindi siyo tishio kwa Watanzania kwa sababu Serikali imeudhibiti na haitatoa tena taarifa rasmi kwa umma kuhusu ugonjwa huo.
Waziri Ummy aliyekuwa akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 29,2022 amesema Serikali imefanikiwa kuudhibiti ugonjwa huo na haujaenea sehemu kubwa.
Amesema kutokana na hali hiyo, Watanzania hawapaswi kuwa na hofu kuhusu ugonjwa huo na waendelee na majukumu yao.
“Ugonjwa huu siyo tishio ni ugonjwa tunaoweza kuuchunguza, kuutibu pamoja na kuudhibiti, tunashukuru mpaka leo hatujapokea wagonjwa wapya kwa hiyo hakutakuwa tena na taarifa maalum,” amesema Waziri Ummy.
Tangu Julai 18 hadi 29 mwaka huu wagonjwa 20 wa mgunda wamethibitishwa huku watu watatu wakifariki dunia na hakuna mgonjwa mpya wala anayetibiwa hospitalini, kwa mujibu wa waziri huyo.
Sambamba na hilo Waziri Ummy amewatoa hofu Wananchi na kuwataka wawe huru kutembelea mkoa wa Lindi kwani ni mara chache sana ugonjwa huo kuambukizwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine.
“Nendeni Lindi, Ruangwa wala hakuna shida, mimi mwenyewe nilikuwa Ruangwa kwa sababu siyo ugonjwa mbaya wa kuambukiza kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine ni very rare(ni nadra sana),” ameongeza Waziri Ummy.
Kwa Mara ya kwanza taarifa za uwepo wa ugonjwa huo zilisikika Julai 12, 2022 mara baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuzungumzia jambo hilo alipokuwa katika maadhimisho ya mkutano wa 20 wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu la Kanisa Katoliki Afrika Mashariki na Kati (AMECEA) jijini Dar es salaam.
“Ukilinganisha na mgonjwa mengine kama Ebola, Uviko-19 na Monkeypox, homa hii ina asilimia chache za kuambukiza hivyo wananchi wasiogope,” amesisitiza Ummy.
Soma zaidi:
Jinsi ya kujikinga na homa ya Mgunda
Licha ya ugonjwa huo kutokuwa tishio bado Wizara imeitaka jamii kuchukua tahadhari za kujikinga ikiwemo kuepuka kunywa na kugusa maji yaliyochafuliwa na wanyama wenye maambukizi,cudongo au chakula cha wanyama wenye maambukizi.
Tahadhari nyingine ni kunywa maji safi na salama yaliyochemshwa na kutibiwa, pamoja na kuchukua hatua za mapema za kufika kwenye kituo cha afya endapo utajihisi una dalili za ugonjwa huo ambazo ni pamoja mwili kuchoka, homa, kuvuja damu na kichwa kuuma.
“Dalili nyingine ni macho kuvilia damu, kuumwa misuli, mwili kuwa wanjano kutoka damu puani kukohoa damu na kusikia kichefuchefu,” ameongeza Waziri Ummy.
Aidha wizara imewataka wananchi kutoa taarifa za wagonjwa wanaoonyesha dalili za ugonjwa huo katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Pia amewasisitiza waganga wakuu wa mikoa na wilaya kufufua timu za ufuatiliaji wa magonjwa na tetesi za magonjwa majumbani na kuhakikisha mgonjwa anapelekwa kituo cha afya, kupimwa na kugundua ugonjwa kwa haraka.
Latest
