Mfumuko wa wanaume mabachela: Sababu ni nini?
- Uhitaji wa mahusiano yenye afya kwa wanawake unaongezeka.
- Jambo hilo linawaacha wanaume wasiotaka kubadilika kubaki bila wenza.
- Wanaume wanashauriwa kuzingatia wapenzi wao kabla hawajaachwa.
Huenda mwanaume haihitaji kuwa na mwenzi ili kuwa na furaha lakini stadi mbalimbali za wanasaikolojia ikiwemo ya Greg Matos wa nchini Marekani zinaonyesha kuwa wanaume huwa na furaha zaidi pale wanapokuwa na mwenza.
Hata hivyo, kuongezeka kwa vigezo vya kimahusiano vinavyowekwa na wanawake imekuwa ni sababu ya baadhi ya wanaume kuwa mabachela kwa muda mrefu au kuchelewa kuingia katika mahusiano.
Hali huwa mbaya, pale baadhi ya wanaume kukosa sifa za kuendelea kuchuana na wanaume wenye vigezo ambavyo wanawake wameviweka ili kuwa na mahusiano yanayojenga.
Kwa mujibu wa Matos, hivi karibuni elimu kwa wanawake juu ya kuchagua mahusiano yenye afya imeshika kasi. Wanawake wanahitaji mwanaume ambaye anapatikana kihisia, mwenye kutenga muda kwa ajili ya mpenzi wake na mwenye kumpenda kwa dhati.
Wadau wengine akiwemo Stacey Lloyd anayeandikia jarida la Brides anasema wanawake pia wanaangalia uaminifu, heshima na hulka ya uchekeshaji kidogo.
Kwa muktadha huo, endapo mwanaume hana sifa hizo, huenda akakabiliwa na vipindi vifupi vya mahusiano ama kumkosa kabisa mwenza wa ndoto yake.
Teknolojia yabadilisha upepo wa mahusiano
Kutokana na changamoto hizo hapo juu, ushindani wa wanaume kutafuta wenza umeendelea kuongeza, jambo linawafanya kutumia teknolojia mbalimbali ili kutimiza malengo yao.
Kwa baadhi ya vijana wa miaka 25 hadi 45 hutumia mitandao ya kutafuta wenza yaani “dating apps” ili kukabiliana na changamoto za vigezo vinavyowekwa na wanawake.
Mbali na mitandao ya kijamii inayofahamika, yaani Instagram Twitter na Facebook, apps kama Tinder, Match na Bumble zimekuwa sehemu ya vijana wanaotafuta mahusiano ya muda mrefu na mfupi kujipatia mahitaji yao.
Hata hivyo, tovuti ya takwimu ya Statista imeainisha kuwa mitandao hiyo ina wanaume wengi zaidi kuliko wanawake na hivyo kuwaacha wanawake wakiwa na uwanda mpana zaidi wa kuchagua wenza wao kuliko wanaume.
Kwa takwimu za mwaka 2021, asilimia 75 ya watumiaji mtandao wa Tinder, walikuwa wanaume. Hii ni sawa na kusema, kwa kila watumiaji 10 wa mtandao huo basi takriban nane ni wanaume.
Jambo hilo huenda linadhihirisha hali halisi iliyopo mtaani ya wanaume kujiimarisha kisaikolojia na kiuchumi ili kupata wenza wa ndoto zao.
Wanaume washauriwa kubadili mtazamo
Baadhi ya watalaam wa mahusiano wameshauri wanaume kubadilisha mtazamo kuhusu mahusiano na kufahamu wanawake wanataka nini kuliko kupambana kutafuta pesa pekee.
Kwa mujibu wa utafiti kuhusu mahusiano uliofanywa mwaka 2012 na Chuo Kikuu cha Sydney Magharibi, ukubwa wa pochi sio kitu pekee wanawake huangalia kwa mwanaume wanayempenda.
Mambo huenda mbele zaidi kufikia kazi inayoingiza kipato hicho ikiwiana na muda anaokuwa huru.
Mbali na kuwa na pesa, mwanaume unahitajika kuwa na muda na mpenzi wako na kumsapoti kihisia.
Matos anashauri wanaume kuwekeza katika kujifunza mbinu za kuwasiliana na wenzi wao, jambo ambalo familia nyingi haziwafundishi watoto wa kiume siku hizi.
Maoni haya yametolewa na mwandishi wa habari na mtaalam wa mawasiliano, Rodgers George. Maoni haya siyo msimamo wa Nukta
Latest