Waliofariki ajali ya ndege Ziwa Victoria wanaagwa leo
- Zoezi laongozwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Dar es salaam. Miili ya watu 19 waliopoteza maisha katika ajali ya ndege iliyotokea jana inaagwa hii leo katika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Albart Chalamila shughuli ya kuagwa kwa miili hiyo itaongozwa na Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ambaye amemuwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.
Baada ya kukamilika kwa zoezi la kuwaaga miili hiyo itakabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya taratibu za mazishi.
Ndege hiyo yenye namba PW 494 ya kampuni ya Precision Air ilikuwa imetokea jijini Dar es Salaam ikiwa na watu 43 wakiwemo abiria 39, wahudumu wawili na marubani wawili ilianguka katika Ziwa Victoria umbali wa mita 100 kabla ya kutua uwanja wa ndege wa Bukoba.
Waliofariki ajali ya ndege Precision Air wafikia 19, Serikali yaagiza uchunguzi
Taarifa iliyotolewa na Shirika la Ndege la Precision Air imefafanua kwamba waliookolewa katika ajali hiyo ni watu 24 na waliopoteza maisha ni 19 na kufanya idadi ya watu wanaohusishwa kuwa ndani ya ndege kuwa 43
Awali kulikuwa na mkanganyiko wa idadi rasmi ya abiria waliokuwepo ndani ya ndege hiyo ambapo ilielezwa waliokolewa ni 26 na waliofariki ni 19 na kufanya jumla ya watu 45 tofauti na idadi iliyotajwa awali.
Latest
